Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa jengo la utawala la Polisi wilaya ya Longido, kulia kwake ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo na kushoto kwake ni Mkuu wa wilaya ya Longido Bw. Daniel Chongolo.
Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wakati akifungua jiwe la msingi lililowekwa katika ujenzi wa jengo la utawala la Polisi wilaya ya Longido.
Jengo jipya la utawala Polisi wilaya ya Longido ambalo lilizinduliwa na Mkuu wa mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo jana katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha).
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Mkuu
wa mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo amewashukuru na kuwapongeza wadau
mbalimbali wa maendeleo ambao wamejitoa na kuhakikisha wanakamilisha
jengo la utawala la Polisi wilaya ya Longido.
Akizindua
jengo hilo jana, alisema kwamba litawezesha Jeshi la Polisi kufanya
kazi kwa utulivu sambamba na kukabiliana vyema na masuala ya uhalifu
katika wilaya hiyo, na kuongeza kuwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Mkoa anajisikia furaha na fahari kuona wadau
wanashirikiana na kuagiza meneja wa Tanesco wilaya ahakikishe ameweka
mita ya umeme ambapo gharama hizo aliahidi atazitoa yeye mwenyewe.
“Lazima
tuimarishe mipaka na Polisi wawe na vituo vya uhakika vya kufanyia kazi
ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za uhalifu na Jeshi
hilo litaendelea kutumia mbinu shirikishi”. Alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Bw.
Gambo aliwaasa baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji pamoja na
wananchi kutoficha wageni ambao wanaishi nchini bila kufuata sheria na
kuongeza kuwa yeyote atakayegundulika anafanya hivyo atachukuliwa hatua
za kisheria.
“Kila
kiongozi anapaswa kutambua watu wote wanaoishi katika eneo lake na
kuhakikisha mgeni yoyote amefuata sheria na kama akigundua (Anaishi bila
utaratibu) atoe taarifa kupitia kamati za ulinzi na usalama za kata ili
hatua ziweze kuchukuliwa”. Alisisitiza Bw. Gambo.
Akizungumza
katika uzinduzi huo mwenyeji wa shughuli hiyo Kamanda wa Polisi mkoa wa
Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Omari Mkumbo mbali na kuwashukuru
wadau hao, alisema kwamba tukio la uchangiaji na ukamilishaji wa jengo
hilo limeonyesha kwamba wana Longido wana mshikamo wa hali juu.
Kamanda
Mkumbo alisema kwamba wananchi waendeleze mshikamo huo ili kuweza
kuimarisha kituo kingine cha Polisi kilichopo tarafa ya Kamwanga na
kutaja majengo mengine ambayo yanajengwa na kukaribia kukamilika kwa
hamasa ya Mkuu wa mkoa kuwa ni kituo cha Polisi cha Kwa Morombo pamoja
na kituo cha Polisi cha Utalii ambacho ujenzi wake unafadhiliwa na TATO
(Tanzania Tourist Operators).
“Kazi
kubwa ya Jeshi la Polisi ni kuhakikisha uhalifu unakomeshwa na japokuwa
takwimu za matukio ya uhalifu katika wilaya hiyo yapo chini lakini bado
kuna tatizo la madawa ya kulevya aina ya Bhangi na Mirungi hivyo
wananchi endeleeni kutoa ushirikiano kwa askari kwani madhara ya madawa
hayo ni makubwa”. Alisema Kamanda Mkumbo.
Kwa
upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Daniel Chongolo alisema ongezeko la
ukamataji wa madawa ya kulevya umetokana na udhibiti mzuri na kuahidi
kuimarisha zaidi usalama kwa kutumia Polisi na vyombo vingine vya
usalama huku akitoa shukrani zake kwa Kamanda wa Polisi mkoa kwa kutoa
gari ambalo litasaidia kuimarisha ulinzi katika tarafa ya Kamwanga.
Awali
akitoa taarifa ya uhalifu pamoja na mchakato wa ujenzi huo, Mkuu wa
Polisi wilaya ya Longido Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Joswam
Israel Kaijanante alisema kwamba ujenzi huo umegharimu zaidi ya Milioni
80 ambazo zilichangwa na viongozi, askari pamoja na wananchi na kuongeza
kwamba bado jengo hilo halina samani na “Kompyuta , Printer” pamoja na
mfumo wa maji taka ambapo gharama zake ni Milioni 16.
Mchakato
wa ujenzi wa jengo hilo ambao una ofisi tatu ambazo ni za Mkuu wa
Polisi wilaya, Mkuu wa Upelelezi wilaya na Mwendesha Mashtaka wa Polisi
ulianza mwaka 2015 na kukamilika mwezi Julai mwaka huu uliwashirikisha
kikamilifu jumla ya wadau wapatao 20 ambao pia walipewa vyeti vya
shukrani.
0 comments:
Post a Comment