C-CEOs FORUM KUWA CHACHU YA UTEKELEZAJI WA DIRA 2050




Na Mwandishi wa OTR - Arusha.


Serikali imesema Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (C-CEOs Forum) 2026, unaotarajiwa kuwakutanisha viongozi kutoka Mashirika zaidi ya 300 ya Umma, pamoja na wawakilishi wa Sekta Binafsi na washiriki wengine zaidi ya 700 kuanzia Septemba 28 hadi 30, 2026, utakuwa jukwaa muhimu la kuimarisha utendaji, tija na mchango wa Mashirika hayo katika utekelezaji wa Dira 2050.

Forum hiyo, inayoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), ni ya nne kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023 na inalenga kuwakutanisha Wenyeviti wa Bodi, Watendaji Wakuu wa Mashirika ya Umma na wadau mbalimbali kujadili namna ya kuongeza ufanisi wa taasisi hizo na kuhakikisha mipango na shughuli zao zinaendana na vipaumbele vya kitaifa vilivyoainishwa katika Dira 2050.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ijumaa, Septemba 25, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, alisema kuwakutanisha viongozi wa Mashirika ya Umma katika jukwaa moja kunatoa fursa ya kujenga uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kuongeza tija na mchango wa Mashirika hayo katika maendeleo ya Taifa.

Amesema ni muhimu Mashirika ya Umma kuhakikisha mipango na shughuli zao zinaendana na malengo ya Dira 2050, ili rasilimali na uwekezaji unaosimamiwa na Serikali uweze kuzalisha matokeo yenye thamani zaidi kwa uchumi na wananchi.

“Tunataka mkutano huu uwe na manufaa yanayoonekana pia nje ya ukumbi wa mikutano, kwa kuwafungulia fursa wafanyabiashara, watoa huduma na wananchi wa Arusha,” alisema.

Mhe. Makalla amesema Arusha ina uzoefu wa kuhudumia mikutano mikubwa ya kitaifa na kimataifa na kwamba Mkoa uko tayari kuwapokea washiriki wa C-CEOs Forum 2026, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mazingira ya usalama, utulivu na ukarimu kwa wageni.

“Watakaohudumia wageni wawe wakarimu ili warudi tena,” amesema, akieleza kuwa ujio wa washiriki zaidi ya 700 utatoa fursa kwa sekta mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo hoteli, migahawa, usafiri, utalii, biashara na huduma nyingine.

Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji mabadiliko katika namna Mashirika ya Umma yanavyotazama utendaji wao, kutoka kwenye kuendesha taasisi na shughuli zake kwenda kwenye kuzalisha matokeo yanayopimika na yenye thamani kwa Taifa.

Kwa mtazamo wake, ufanisi wa juu unapaswa kuonekana katika uwezo wa Mashirika kutumia rasilimali na uwekezaji waliokabidhiwa kwa tija, kujenga ushindani, kuimarisha uimara wa kifedha na kutoa huduma zenye ubora, huku yakichangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi.

“Tunataka Mashirika ya Umma yenye ufanisi wa juu, shindani na imara katika kutekeleza Dira 2050,” alisema Mchechu.

Bw. Mchechu alisema thamani ya uwekezaji wa Serikali katika Mashirika na kampuni zake imeongezeka kutoka Sh67.95 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh92.28 trilioni mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 35.8, hali inayoongeza umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji huo unazalisha matokeo makubwa zaidi.

Alisema matokeo hayo hayawezi kupimwa kwa gawio pekee, bali yanapaswa kuangaliwa kwa upana kupitia tija, ubora wa huduma, ufanisi wa matumizi ya rasilimali, uimara wa kifedha, ubunifu, matumizi ya teknolojia, uwezo wa kushindana na athari ya taasisi katika uchumi.

Kwa mtazamo huo, alisema Mashirika ya Umma yanapaswa kujenga uwezo wa kubadilika kulingana na mazingira ya uchumi, teknolojia na mahitaji ya wananchi, huku uongozi na bodi zikibeba jukumu muhimu la kuweka mwelekeo wa utendaji na uwajibikaji.

“C-CEOs Forum inalenga kuangalia kwa upana zaidi jinsi ya kubadilisha rasilimali na uwekezaji kuwa utendaji na matokeo yenye thamani zaidi,” alisema.

Bw. Mchechu alisema ongezeko la mapato yasiyo ya kodi linalotokana na Mashirika na taasisi zinazochangia kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, linaonesha pia umuhimu wa kuendelea kuboresha utendaji wa taasisi hizo.

Mapato hayo yameongezeka kutoka Sh637.7 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh1.327 trilioni mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 108.3.

Alisema kwa hiyo, mjadala kuhusu Mashirika ya Umma haupaswi kuishia kwenye suala la kiasi cha fedha kinachowasilishwa Serikalini, bali unapaswa kuangalia thamani pana inayozalishwa na uwekezaji wa umma, ikiwemo huduma, ajira, uzalishaji, ubunifu, ushindani na mchango katika uchumi.

Katika mtazamo wake, maeneo hayo yanahitaji uongozi wenye mwelekeo wa kimkakati, utawala bora, matumizi makubwa zaidi ya teknolojia za kidijitali na akili bandia, mifumo endelevu ya upatikanaji wa fedha, pamoja na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Alisema pia Mashirika yanahitaji kuwekeza katika rasilimali watu na ujuzi wa baadaye ili yaweze kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia, kiuchumi na kimazingira, sambamba na kuzingatia masuala ya mazingira, jamii na utawala bora.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

RAIS SAMIA ATAJWA KINARA AFYA YA MSINGI

 


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametambuliwa kuwa kinara katika kuimarisha huduma za afya ya msingi kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana nchini, hususan katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.
Akifungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Aya ya Msingi (IPHC) kwa niaba ya Rais Samia katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Jijini Arusha (AICC), Septemba 9, 2026, Waziri Mkuu amesema mafanikio hayo yameiwezesha Tanzania kutambulika kimataifa, ikiwemo Rais Samia kutunukiwa Goalkeeper Award mwaka 2025 na kuteuliwa kuwa kinara wa Umoja wa Afrika wa huduma za afya ya mama na mtoto mwaka 2026.

Rais Mhe. Dkt. Samia awasili Mkoani Arusha kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA. Amos Makalla mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), tarehe 06 Machi, 2026. Rais Mhe. Dkt. Samia amewasili Jijini Arusha kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika tarehe 07 Machi, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) tarehe 06 Machi, 2026. Rais Mhe. Dkt. Samia amewasili Jijini Arusha kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika leo tarehe 07 Machi, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiangalia Kikundi cha Sanaa cha Maasarie Troupe mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) tarehe 06 Machi, 2026. Rais Mhe. Dkt. Samia amewasili Jijini Arusha kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa 25 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)unaotarajiwa kufanyika tarehe 07 Machi, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC). 

 






Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

NSSF YAIBUKA MSHINDI WA KWANZA NA KUPOKEA TUZO KWA UZINGATIAJI WA SHERIA YA SERIKALI MTANDAO, VIWANGO NA MIONGOZO



Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeibuka mshindi wa kwanza na kutunukiwa tuzo kwa
Taasisi zilizofanya vizuri katika uzingatiaji wa Sheria ya Serikali Mtandao, viwango na miongozo kwa taasisi zilizo katika ngazi ya nne ya ukomavu wa TEHAMA Serikalini.

Tuzo hiyo ilitolewa na Ridhiwani Kikwete, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, na kupokelewa na Bw. Donald Mhaiki, Mkurugenzi wa TEHAMA wa NSSF.

Hafla ya utoaji wa tuzo hiyo ilifanyika wakati wa kilele cha Kikao cha 6 cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha International Conference Centre (AICC), jijini Arusha.

Ushindi huo unaonesha jitihada za NSSF katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA na kuzingatia kikamilifu sheria, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao nchini.

Serikali yazindua Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii na ‘Hifadhi Scheme’ kwa Waliojiajiri

Serikali yazindua Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii na ‘Hifadhi Scheme’ kwa Waliojiajiri

Na MWANDISHI WETU, 
ARUSHA. Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano imezindua Sera ya Taifa ya Kinga ya Jamii pamoja na Mpango wa Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri ‘Hifadhi Scheme’ hatua inayolenga kupanua wigo wa hifadhi ya jamii na kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika mifumo ya kinga ya kijamii.

Uzinduzi huo umefanyika Februari 9, 2026 katika mkutano wa wadau wa sekta ya kinga ya jamii uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Sangu alisema sera hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma jumuishi za hifadhi ya jamii. Aliongeza kuwa tangu 2018, Serikali imefanya maboresho ikiwemo kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kubaki na NSSF na PSSSF ili kuongeza ufanisi wa huduma na ulipaji wa mafao.

Mhe. Sangu alisema maboresho hayo yameongeza idadi ya wanachama. NSSF imeongezeka kutoka wanachama 808,935 mwaka 2020 hadi zaidi ya wanachama 2,213,659 mwaka 2025, huku PSSSF ikiongezeka kutoka 697,677 hadi 899,948. Aidha, thamani ya uwekezaji wa Mifuko imeongezeka kutoka shilingi trilioni 9.36 hadi trilioni 20.14, na jumla ya thamani ya Mifuko kufikia trilioni 24.20.

Kuhusu mpango wa Hifadhi Scheme, alisema hadi Desemba 2025 zaidi ya wanachama 500,000 kutoka makundi mbalimbali yakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali wamejiunga, huku lengo likiwa kufikia wanachama milioni 5.5 ifikapo Juni 2031.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Mary Maganga, alisema Serikali imeipa NSSF jukumu la kupanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa wananchi waliojiajiri ili kuhakikisha sera mpya inaleta matokeo yanayotarajiwa.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, alisema Mfuko unaendelea kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza uandikishaji wa wanachama wapya, na kupanua wigo wa uwekezaji ndani na nje ya nchi, ikiwemo nchi za SADC na Afrika Mashariki.

Bw. Mshomba alisema Mfuko umepata mafanikio makubwa katika Serikali ya awamu ya sita ambapo thamani ya NSSF imeongezeka kutoka trilioni 4.8 mwaka 2021 hadi trilioni 10.4 Desemba 2025, na kuwa imepata ziada kwa miaka minne mfululizo kuanzia 2021 hadi mwaka wa fedha 2024/25, ikivuka lengo la ziada ya shilingi trilioni moja.

Akizungumzia ukusanyaji wa michango, Bw. Mshomba alisema Mfuko umeendelea kuvuka malengo, ambapo mwaka wa fedha 2023/24 ulifikia zaidi ya shilingi trilioni mbili, huku mwaka 2024/25 makusanyo yakizidi trilioni 2.4 na kwamba katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kuanzia 2020 hadi 2025, NSSF imefanikiwa kuvuka lengo la kukusanya angalau shilingi trilioni moja kwa mwaka. 

Bw. Mshomba aliongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. NSSF ina zaidi ya wanachama milioni 2.3 na imejikita kuboresha huduma kupitia TEHAMA na mpango wa miaka mitano unaolenga kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa 2050 na Ilani ya Uchaguzi ya CCM. 




 

TAARIFA KWA UMMA - ZOEZI LA UHAKIKI WA WASTAAFU NA WATEGEMEZI

 TAARIFA KWA UMMA - ZOEZI LA UHAKIKI WA WASTAAFU NA WATEGEMEZI


 

DC MTATIRO ATUNUKIWA SHAHADA YA SABA! APATA UZAMILI WA MASOMO YA AMANI NA USALAMA

 


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, ni miongoni mwa wahitimu waliotunukiwa shahada za uzamili katika mahafali yaliyofanyika Ijumaa, Februari 6, 2026, katika Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika Ngurdoto jijini Arusha.

Katika mahafali hayo, Mtatiro ametunukiwa Shahada ya Uzamili ya Masomo ya Amani na Usalama (Master of Arts in Peace and Security Studies) na kuchaguliwa kuwa msemaji mkuu wa wahitimu wote, ambapo alitoa hotuba kwa niaba yao.

Amesisitiza umuhimu wa vijana kuendelea kujifunza na kujiongezea maarifa kulingana na nafasi na ndoto zao, akieleza kuwa elimu hiyo inapaswa kuendana na mahitaji ya ujuzi, ushindani wa kimataifa pamoja na vipaumbele vya kimkakati vya maendeleo ya Tanzania ya sasa.

Mbali na shahada hiyo mpya ya uzamili, Mtatiro pia anamiliki Stashahada ya Uzamili ya Sheria kwa Vitendo (Postgraduate Diploma in Legal Practice) pamoja na shahada nyingine tatu za uzamili ambazo ni: Uzamili wa Usimamizi wa Umma Uzamili wa Sera za Umma na Uzamili wa Mawasiliano ya Umma.

Aidha, ana shahada mbili za kwanza ambazo ni:vShahada ya Sanaa katika Elimu na Shahada ya Sheria (LL.B).

Historia ya Uongozi wa Wanafunzi

Akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mtatiro anakumbukwa kwa mchango wake katika harakati za wanafunzi zilizoleta mabadiliko katika usimamizi wa sera za elimu ya juu, hususan eneo la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Katika kipindi hicho, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi wa wanafunzi zikiwemo: Waziri wa Mikopo – DARUSO. Waziri Mkuu – DARUSO na Katibu Mkuu – TAHLISO.

Uzoefu wa Kisiasa na Kitaifa

Mtatiro pia aliwahi kuwa kiongozi mwandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF) kati ya mwaka 2009 na 2017, akihudumu katika nafasi mbalimbali zikiwemo: Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria. Naibu Katibu Mkuu – CUF Tanzania Bara na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Taifa.

Vilevile, aliwahi kuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba kwa kuteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Uongozi Serikalini

Kwa upande wa utumishi wa umma, Mtatiro aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mwaka 2019, nafasi aliyohudumu hadi mwaka 2024. Kuanzia mwaka 2024 hadi sasa anahudumu kama Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga.

Mbali na majukumu ya kiutawala, Mtatiro anatambulika pia kama mwalimu, wakili, na mchambuzi wa sera za umma mwenye uzoefu mpana katika masuala ya utawala na maendeleo.



MAKALLA AIPONGEZA SERIKALI, JKCI YATOA VIPIMO BURE MAGONJWA YA MOYO ARUSHA


Na Pamela Mollel,Arusha 

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha huduma za afya kwa kusogeza huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo karibu na wananchi.

 Anasema uanzishwaji wa Kituo cha Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Arusha Lutheran Centre (Seliani) utawanufaisha wananchi wa Arusha na mikoa ya jirani, pamoja na watalii na wageni watakaoshiriki michuano ya AFCON 2027.

Mhe Makalla anayasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua zoezi la utoaji wa vipimo na matibabu ya magonjwa ya moyo bure, ambapo jumla ya wananchi takribani 1,200 wamenufaika na huduma hizo, huku Serikali ikiahidi kuwawezesha wananchi wasiokuwa na uwezo wanaohitaji rufaa ili wapate matibabu zaidi katika Taasisi ya Moyo ya JKCI jijini Dar es Salaam. 

Aidha, amewahamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, amesema katika Kanda ya Kaskazini, magonjwa ya moyo na magonjwa yasiyoambukiza yameendelea kuonekana kwa kasi, ambapo kupitia programu ya upimaji wa afya, zaidi ya wananchi 3,000 wamejitokeza kupima afya zao. 

Anasema kuwa kati yao, asilimia 9 walibainika kuwa na matatizo ya moyo, huku asilimia 29 wakigundulika kuwa na shinikizo la damu, ugonjwa uliokuwa unaongoza zaidi kwa wananchi wenye umri kati ya miaka 45 hadi 80

Dkt. Kisenge ameongeza kuwa sababu kuu zinazosababisha ongezeko la magonjwa hayo ni kutofanya mazoezi ya mwili, unene uliopitiliza, unywaji wa pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara, pamoja na kutokuzingatia lishe bora, akiwahimiza wananchi kubadili mtindo wa maisha na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kuepuka madhara makubwa ya kiafya.





 

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa