
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, ni miongoni mwa wahitimu waliotunukiwa shahada za uzamili katika mahafali yaliyofanyika Ijumaa, Februari 6, 2026, katika Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika Ngurdoto jijini Arusha.
Katika mahafali hayo, Mtatiro ametunukiwa Shahada ya Uzamili ya Masomo ya Amani na Usalama (Master of Arts in Peace and Security Studies) na kuchaguliwa kuwa msemaji mkuu wa wahitimu wote, ambapo alitoa hotuba kwa niaba yao.
Amesisitiza umuhimu wa vijana kuendelea kujifunza na kujiongezea maarifa kulingana na nafasi na ndoto zao, akieleza kuwa elimu hiyo inapaswa kuendana na mahitaji ya ujuzi, ushindani wa kimataifa pamoja na vipaumbele vya kimkakati vya maendeleo ya Tanzania ya sasa.
Mbali na shahada hiyo mpya ya uzamili, Mtatiro pia anamiliki Stashahada ya Uzamili ya Sheria kwa Vitendo (Postgraduate Diploma in Legal Practice) pamoja na shahada nyingine tatu za uzamili ambazo ni: Uzamili wa Usimamizi wa Umma Uzamili wa Sera za Umma na Uzamili wa Mawasiliano ya Umma.
Aidha, ana shahada mbili za kwanza ambazo ni:vShahada ya Sanaa katika Elimu na Shahada ya Sheria (LL.B).
Historia ya Uongozi wa Wanafunzi
Akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mtatiro anakumbukwa kwa mchango wake katika harakati za wanafunzi zilizoleta mabadiliko katika usimamizi wa sera za elimu ya juu, hususan eneo la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Katika kipindi hicho, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi wa wanafunzi zikiwemo: Waziri wa Mikopo – DARUSO. Waziri Mkuu – DARUSO na Katibu Mkuu – TAHLISO.
Uzoefu wa Kisiasa na Kitaifa
Mtatiro pia aliwahi kuwa kiongozi mwandamizi wa Chama cha Wananchi (CUF) kati ya mwaka 2009 na 2017, akihudumu katika nafasi mbalimbali zikiwemo: Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria. Naibu Katibu Mkuu – CUF Tanzania Bara na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Taifa.
Vilevile, aliwahi kuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba kwa kuteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Uongozi Serikalini
Kwa upande wa utumishi wa umma, Mtatiro aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mwaka 2019, nafasi aliyohudumu hadi mwaka 2024. Kuanzia mwaka 2024 hadi sasa anahudumu kama Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga.
Mbali na majukumu ya kiutawala, Mtatiro anatambulika pia kama mwalimu, wakili, na mchambuzi wa sera za umma mwenye uzoefu mpana katika masuala ya utawala na maendeleo.
0 comments:
Post a Comment