Imeandikwa na John Mhala, Arusha
ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ) Kanda ya
Kaskazini Kati, Solomoni Masangwa (pichani) amemuonya mbunge wa Siha,
Godwin Mollel (Chadema) kuacha kuhubiri siasa chonganishi kanisani kwa
kuwatukana viongozi waliopo madarakani na kutoa onyo kwa viongozi wa
kanisa hilo kutoruhusu wanasiasa kufanya siasa kanisani.
Kauli hiyo ameitoa juzi wakati wa hafla ya uzinduzi wa kanisa KKKT
dayosisi ya kaskazini kati, jimbo la Arusha Magharibi usharika wa
Kiranyi. Askofu huyo alikerwa na hatua ya mbunge Mollel kujinadi kisiasa
huku akimshambulia Rais John Magufuli bila kujali kuwa mkusanyiko
uliopo kanisani ni waumini wenye itikadi tofauti za kisiasa na kwamba
mahala pale palikuwa sehemu takatifu ya kuabudiwa na siyo jukwaa la
siasa.
‘’Napenda kutoa angalizo kuwa kanisani siyo sehemu ya siasa na
nisingependa kuona siasa ikihubiriwa kanisani tena,” alisema. Mbunge
huyo wa Siha akiwa kanisani hapo alisema ‘’Kuna mwanaume mmoja hapa
Tanzania anajiona yeye ni kidume kuliko wanaume wote ila ajue wapo
wanaume zaidi yake sasa”. Kutokana na kauli hiyo, askofu huyo akasema
“Sijui anamlenga nani bila shaka anamaanisha Rais Magufuli, kauli hiyo
siyo kauli njema sana na inastahili kukemewa na kila mtu”.
Awali mbunge Mollel alisikika akitamka kanisani hapo kwamba nchi hii
imefikia pabaya mwanaume mmoja amekuwa na maamuzi hata kama ni ya
kuhatarisha amani na atambue kuwa akijiona yeye ni mwanaume pekee
akiongoza lakini ajue wapo wanaume zaidi yake na ipo siku wanaume
wengine watavunja ukimya.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment