Desemba 6, mwaka huu Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi aliandika historia kwa kuitisha mkutano wa hadhara wa amani
jijini Arusha ukishirikisha wadau wa siasa, dini na kijamii Arusha
isipokuwa Chadema walioususia dakika za mwisho.
Katika sababu zao kadhaa, Chadema wanadai
kuchukizwa na propaganda zilizosambazwa mitaani vyombo vya chama tawala,
kwamba Chadema sasa maji shingo na hivyo wangetumia mkutano huo
kutangaza kumtambua Meya wa Arusha.
Sikusudii kujadili ushiriki wa wadau katika
mkutano huo, bali ninalenga kujadili nia, lengo, kusudi, dhamira njema
na njia sahihi anayopaswa kufuata Jaji Mutungi katika harakati za
kutafuta na kurejesha amani Arusha.
Kabla ya kufikia hatua ya kuitisha mkutano wa
hadhara wa wadau, Jaji Mutungi alipaswa kujua kiini, sababu na washiriki
wa migogoro
Msajili na timu yake wanapaswa kujifunza, kuelewa
na kubaini kiini na sababu za migogoro, kujua wahusika wa vurugu,
malengo na njia wanazotumia kuyafanikisha.
Anapaswa kujua faida na hasara kijamii, kisiasa na kiuchumi ya migogoro na vurugu hizo kwa makundi yote.
Kwa uchache, madhara yanayoonekana wazi ni pamoja na vifo, ulemavu na kudorora kwa uchumi.
Baada ya kubaini yote hayo hapo juu, Msajili
atafute njia sahihi, bora na ya mwafaka ya kuponya madhara na vidonda
ndugu vya mgogoro huo.
Njia sahihi ni majadiliano ya kina yasiyo na hila
yanayopaswa kusimamiwa na watu waadilifu, wenye nia na dhamira njema,
wanaoheshimika na kukubalika katika jamii na makundi yote.
Hawa wanaweza kuwa viongozi wa dini, wanasiasa au
wa kijamii ambao hawajachafuka wala kujihusisha kwa njia moja au
nyingine na migogoro hii. Watu wa aina hii wapo wengi Arusha na sehemu
mbalimbali nchini na wanajulikana kwa majina na sura.
Kabla ya kuwaleta hadharani mbele ya umma, Ofisi
ya Msajili iratibu vikao na mikutano ya faragha kati kundi moja moja na
wasuluhishi ili kukubaliana kiini, sababu, madhara au faida ya migogoro
na vurugu na njia sahihi ya kurejesha amani Arusha.
Majadiliano haya yanastahili kuanzia katika ngazi
ya kundi moja moja kabla ya kujumuisha makundi yote au kwenye mkutano wa
hadhara.
Wahusika wa migogoro na vurugu Arusha wanaopaswa kujadiliana na
kufikia makubaliano ni pamoja na vyama vya CCM, Chadema, Jeshi la Polisi
na viongozi wa Serikali ya Wilaya na Mkoa wa Arusha ambao hutumia ukada
wa CCM kukibeba chama hicho dhidi ya Chadema.
Msigano wa kisiasa kati ya Chadema kwa upande
mmoja na CCM ikishirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkoa pamoja na
polisi na vyombo vingine vya dola kwa upande mwingine, ndiyo chanzo cha
migogoro na vurugu Arusha.
Mgogoro binafsi, wa kitaasisi au kimasilahi kati
ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo na mbunge wa Arusha, Godbless
Lema nao unastahili kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi kabla ya wawili
hawa kujitokeza hadharani mbele ya umma kuhubiri amani.
Bila kujua kiini, wahusika, hasara (faida), kwa
umma na njia sahihi ya kutibu vidonda vinavyotokana na migogoro na
vurugu za Arusha, kamwe hatutarejesha amani Arusha.
Maandamano na mikutano ya hadhara ya kuhubiri
amani hayatatuletea amani ya kweli Arusha. Amani itapatikana tu pale
wahusika watapojitambua, kujua tofauti zao, kuyaweka hadharani,
kuyajadili, kila upande kukubali kupata na kukosa (win win process),
kusamehe na kurejea msemo wa “yaliyopita si ndwele, tugange yajayo”
+255 766 434 354
Chanzo;Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment