TAASISI ya Utafiti wa Kahawa Nchini (TaCRI), imezitaka halmashauri
za wilaya nchini kushirikiana na taasisi hiyo kuwawezesha wakulima wa
kahawa kuendesha kilimo bora cha kisasa kitakachowaongezea kipato.
Mtafiti wa Usambazaji Teknolojia na Mafunzo wa TaCRI, Jeremiah Magesa,
alitoa kauli hiyo juzi wakati akizindua kampeni ya ugawaji miche ya
kahawa katika halmashauri ya wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Alisema wakati umefika sasa kwa halmashauri za wilaya nchini kuwekeza
katika zao la kahawa, ili kuongeza kipato cha halmashauri kutokana na
ushuru wa kahawa unaolipwa na wanunuzi sanjari na kuwakomboa wakulima
kutoka kwenye lindi la umaskini.
Magesa aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kwa kuonyesha mfano
kwa kununua miche bora ya kahawa 45,000 yenye thamani ya sh milion
16, kwa lengo la kuigawanya kwa wakulima kama njia moja ya kufufua zao
hilo.
Alizitaka halmashauri nyingine ambazo nazo wakulima wake
wanajishughulisha na kilimo cha kahawa kuiga mfano huo sanjari na
kuendeleza vitalu vya uzalishaji miche bora ya kahawa kwenye maeneo yao.
Awali, Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Chikira Mcharo,
alisema wamedhamiria kushirikiana na TaCRI ili kufufua zao la kahawa
ambalo miaka ya nyuma lilijulikana kama mkombozi wa wakulima mkoani
Kilimanjaro.
Alisema kuwa miche hiyo waliyoinunua wataigawanya kwenye vijiji 26
vilivyoko kwenye kata 26, lengo likiwa ni kuhakikisha wanahamasisha
kilimo cha zao hilo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment