SERIKALI imeitaka Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Nchini
(PSPTB) kuwachukulia hatua za kinidhamu wanachama wake watakobainika
kuisababishia hasara serikali kwa kuingia mikataba mibovu ya ununuzi
ambayo haina tija kwa taifa.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa nne uliohudhuriwa na wataalamu
zaidi ya 500 wa tasnia ya manunuzi na ugani mkoani hapa mwishoni mwa
wiki, Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, alisema uchumi wa nchi,
umekuwa ukiyumba kutokana na usimamizi mbovu wa manunuzi.
“Wataalamu msikubali hata kidogo kuchafua sifa nzuri ya taaluma
yenu..na kama kuna mtu anakulazimisha kufanya uovu huo kataa.. ukikubali
ni wajibu wa bodi kukuwajibisha,” alisema.
Alisema asilimia 70 ya bajeti ya serikali kila mwaka huenda kwenye
manunuzi, hali inayoonyesha umuhimu wa sekta hiyo, hivyo ni lazima
manunuzi yafanyike kwa kuzingatia maslahi ya taifa.
Mbene alitoa wito kwa PSPTB kuongeza kasi katika usimamizi wa maadili
kwa wanachama wake, ili pamoja na mambo mengine kuleta ustawi na
kuepusha upotevu wa fedha za umma kwa manunuzi ya bidhaa zisizokidhi
viwango.
Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Clemence Tesha, alisema tangu kuanzishwa
kwa bodi hiyo mwaka 2007 kabla ya kukasimu kwa iliyokuwa NBMM hadi sasa
imezalisha wahitimu wa kada mbalimbali wapatao 23,182, sawa na asilimia
47 ya mahitaji yote ya wataalamu hao kwa taifa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment