JAJI Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha juzi alimpa
mamlaka Carren Kindondechi, kusimamia mirathi ya baba yake, Alfred Leo
aliyekuwa akimiliki mali yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 50 jijini
Arusha.
Hata hivyo, uamuzi huo wa Kindondechi ambaye ni raia wa Marekani na
mtoto wa marehemu Leo kusimamia mali hizo, umepingwa na watoto wengine
wawili wa marehemu, Conrad Leo na Allan Leo wanaoishi nchini kwa madai
kuwa Kindondechi na kaka yake, Kelvin Leo hawatambuliki katika ukoo wa
Leo na kisheria hawapaswi kusimamia mali hizo. Kabla ya uamuzi wa juzi
wa Jaji Maghimbi, kesi hiyo iliwahi kufunguliwa na Kelvin ambaye ni kaka
ya Carren kupitia kwa wakili Salim Mushi wa Kampuni ya Uwakili ya
Elite, Juni 24, 2015 na kusikilizwa na Jaji Fatuma Massengi ambaye
aliitupilia mbali kwa maelezo kuwa Kelvin hawezi kusimamia mirathi hiyo
kwa kuwa hana sifa za kisheria kuwa msimamizi wa mirathi hiyo.
Kesi hiyo ilirudishwa katika mahakama hiyo, na Jaji Maghimbi katika
uamuzi wake, alisema Kindondechi ana sifa za kusimamia mirathi ya
marehemu baba yake na sheria inaeleza hivyo kuwa mtoto huyo anaruhusiwa
kisheria kusimamia mirathi. Kutokana na uamuzi huo, Allan na Conrad
wamesema watakata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya Jaji
Maghimbi kwa madai kuwa mahakama moja haiwezi kuwa na maamuzi mawili
tofauti na kuitaka Mahakama ya Rufaa kutengua hukumu hiyo.
Allan alisema mbali ya kukata rufaa ngazi ya juu kutaka kupata
ufafanuzi wa kisheria juu ya jambo hilo, pia wametoa taarifa ya
kusitisha uuzwaji, ukusanyaji kodi wa nyumba za marehemu baba yao na
uendeshaji wa shughuli zote za kibiashara. Awali aliyekuwa Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo ya Maromboso, Simaitoni Joseph katika
uamuzi wake Januari 27, mwaka juu alisema usimamizi wa mirathi unapaswa
kushirikisha watoto wa hapa nchini na wa nje na siyo wa upande mmoja.
Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo mahakamani hapo, mali alizoacha
marehemu ni magari zaidi 18 ya aina mbalimbali, viwanja vitano vilivyoko
Moshono na Sakina, nyumba tisa na za kisasa zilizopo eneo la Uzunguni
na Sakina, hoteli ya kitalii ya Lion na hisa za kampuni ya Lion
International, vyote vinadaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni
50.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment