Imeandikwa na Waandishi Wetu
KATA 43 za Tanzania Bara katika halmashauri 36 mikoa 19, jana
zilifanya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani ulioenda vizuri sehemu mbalimbali
nchini huku matokeo ya awali yakionesha wakati tukienda mitamboni kuwa
wagombea wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wamefanya
vizuri katika kata mbalimbali walizosimama mkoani Arusha.
Wakati CCM kikitamba Arusha, wapinzani wao wakuu, Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilitangaza kujitoa kwenye uchaguzi
huo katika kata tano zilizopo wilayani Arumeru mkoani Arusha jana
alasiri wakati tayari upigaji kura ukiwa unaendelea katika kata hizo.
Kata walizojitoa ni Maroroni, Makiba, Ngabobo, Leguruki na Ambureni.
Wakati Chadema ikitangaza kujitoa kwa madai ya kuwapo kwa fujo,
Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima
alieleza kuwa uchaguzi huo kwa kata zote 43 umekwenda vizuri kwa
asilimia 100.
“Vituo vyote kufikia saa 10.30 jioni hali ilikuwa nzuri na kura
zilikuwa zinahesabiwa. Kumekuwapo na kasoro ndogo, kwa mfano kule Mwanza
kuna vijana wa Chadema walikuwa wakiwazuia watu kwenda kupiga kura
Nyakato. “Dar es Salaam kila kitu kimekwenda vizuri, Lushoto kulikuwa na
mawakala walitaka waruhusiwe bila kuwa na kiapo cha uwakala, lakini
wakazuiwa,” alisema Kailima.
Kuhusu Chadema kujitoa, alisema suala hilo limefanyika kati ya saa 8
na 9, wakati mambo mengine yakiwa yamefanyika, na kuongeza kuwa ni haki
yao, lakini suala la kurudiwa uchaguzi halipo. “Uchaguzi kwa mujibu wa
sheria na kanuni unaweza kurudiwa endapo msimamizi msaidizi wa uchaguzi
ataona kuna vurugu kubwa na hivyo kuchukua hatua za kuiarifu Tume.
Lakini kwa Arusha, hakuna vurugu zozote kubwa zilizotolewa na
msimamizi msaidizi,” alieleza Kailima. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Taifa
wa Chadema, Freeman Mbowe, wamechukua uamuzi huo baada ya kuona rafu
mbalimbali zikifanyika ikiwemo baadhi ya wabunge na viongozi mbalimbali
kukamatwa na kuumizwa sehemu mbalimbali za miili yao.
Alisema wamevumilia kwa muda mrefu huku wakitegemea wenye mamlaka
watatumia busara zao kusimamia utengamano na amani katika jimbo hilo,
lakini wameona ni heri wajitoe tu. “Huu si uchaguzi, ni fujo Arumeru
hakuna uchaguzi, watu wanapigwa na vyombo vya dola vinaangalia tu wala
havichukui hatua sasa nasema wananchi wakiona wanaonewa huko walipo
watafute utaratibu wao kujihami na vipigo,” Mbowe aliwaambia waandishi
wa habari.
Alisema wataendelea kushiriki kwenye kata nyingine 38 zilizobakia.
Wagombea waliotangaza kujitoa ni Dominick Mollel (Ambuleni), Fabiel
Mbise (Leguruki), Emmanuel Salewa (Ngabobo), Joyce Ruto (Makiba) na
Asanterabi Mbise (Maroroni). Ruto, Mollel na Mbise walidai wamejitoa kwa
sababu ya kuzuiwa mawakala wao katika vituo vya kura kwa madai hawana
utambulisho kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elias Mungure alisema katika kata
hizo tano, taratibu nyingi za uchaguzi zimekiukwa na hivyo wameona
hakuna sababu za kuendelea na uchaguzi huo. Alisema wagombea wote jana
waliandika barua rasmi za kujitoa kushiriki uchaguzi huo. Mbunge wa
Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema) na wafuasi wanne walitiwa
mbaroni Kata ya Leguruki wilayani Aremeru kwa tuhuma za kuzuia wananchi
kwenda kupiga kura na kutafuta wananchi wenye umri mkubwa ili wawape
kadi zao za kupigia kura.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha
kukamatwa kwa mbunge huyo na watu wengine wakizuia wananchi kupiga kura
kwa madai hakuna mawakala wa vyama vyao vya siasa. Kata ya Murriet
Arusha, baadhi ya changamoto zilikuwa mawakala kutotambua vituo vyao vya
kupigia kura na wengine kukosa barua za utambulisho wa vyama vyao
katika kata hiyo.
Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Murriet, Suleiman Kikinga alisema
hakuna upungufu wa vifaa vya kupigia kura kwani vilipelekwa mapema
asubuhi katika vituo 41 vya kata hiyo. Mkazi wa Kwa Mrombo, Elias
Bichokora alisema uchaguzi ni mzuri na hali ya usalama ni nzuri ingawa
mwitikio wa wananchi ulikuwa mdogo. Matokeo ya awali yalionesha CCM kuwa
mbele katika kata hiyo.
Wakati Chadema ikijitoa, matokeo yameonesha katika kata hizo za
Arumeru, CCM ilikuwa inaongoza katika vituo vingi ikiicha kwa mbali
kabisa Chadema, hali inayoonesha kuwa itarejesha kata ambazo zilikuwa
zimekwenda upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Mkoani Morogoro,
katika Kata ya Kiroka katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro
ulifanyika jana kwa njia ya amani na utulivu mkubwa.
Katika uchaguzi huo jana, wapigakura walioandikishwa ni 6,295 na
kulikuwa na wagombea watatu, Jamila Mohamed kupitia CCM, Ngozoma Rahim
wa Chadema pamoja na Jastah Mbena wa Chama cha Wananchi (CUF). Msimamizi
wa Uchaguzi wa majimbo ya Morogoro Kusini na Morogoro Kusini Mashariki,
Sudi Mpili alisema hadi saa 10 jioni, wananchi walikuwa wamepiga kura
na kubakia kazi ya kuhesabu kura kwenye vituo na kutarajia kutangazwa
kwa matokeo kabla ya saa mbili usiku.
Kata nyingine iliyofanya uchaguzi ni ya Sofi iliyopo Halmashauri ya
Wilaya ya Malinyi. Mkoani Dar es Salaam, baadhi ya wananchi waliopiga
kura Kata ya Saranga, Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo, wamepongeza
utaratibu uliotumika kutokana na kutokuwepo na foleni. Wananchi hao
walisema wamezoea kwa kawaida katika vituo vya kupigia kura kukuta
msongamano na foleni kubwa, lakini katika uchaguzi huo jana hapakuwa na
foleni vituoni.
Gazeti hili lilipita katika baadhi ya vituo vya kupigia kura katika
kata hiyo kujionea hali halisi. Akizungumza baada ya kupiga kura, mkazi
wa Kimara Stopover, Margareth Nderumakialisema utaratibu ni mzuri na
alipiga kura moja kwa moja bila kukaa foleni. Naye Chande Ligeni wa
Kimara alisema ametumia haki yake ya msingi ya kumchagua kiongozi
anayemtaka na kusema hapakuwa na usumbufu katika vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo, baadhi ya vituo, Shule ya Msingi Mavurunza waandishi wa
habari walizuiwa kutochukua taarifa wala kupiga picha kwa madai
Mkurugenzi hajatoa kibali kwa waandishi. Akizungumzia uchaguzi huo kwa
njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori alisema uchaguzi
umefanyika vizuri na vituo vilifunguliwa asubuhi kuwapa wananchi fursa.
Alisema vituo vipo 129 na hali ya usalama imeimarishwa lakini taarifa
zaidi kuhusu uchaguzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ubungo
ndiye anaweza kuzitoa kwa usahihi. Kata ya Kijichi Wilaya ya Temeke
mkoani Dar es Salaam umefanyika kwa amani ingawa watu waliojitokeza
kupiga kura ni wachache.
Gazeti hili lilitembelea vituo vya uchaguzi na kubaini changamoto
hiyo huku wasimamizi wa uchaguzi na mawakala wakidai wananchi hawaelewi
faida za kupiga kura na hawakushiriki mikutano ya kampeni ya wagombea.
Vyama vilivyoweka wagombea wake katika kata hiyo ni Chama Cha Mapinduzi
(CCM), ACT Wazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), NCCR
Mageuzi, Alliance for Democratic Change (ADC) na Chama cha Wananchi
(CUF).
“Mwamko wa watu kupiga kura ni mdogo, watu waliojitokeza ni wachache
na wanakuja kwa kusuasua hatuelewi tatizo ni nini wakati hali ni ya
utulivu kabisa,” alisema msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha Kijichi A
kilichopo katika Shule ya Msingi Mtoni Kijichi. Alisema wananchi
waliofika kupiga kura walipiga bila usumbufu wowote na hakukuwa na
malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi na pia mawakala wa vyama.
Vituo vya Mgeninani ofisi za Serikali ya Mtaa, wasimamizi wa uchaguzi
na mawakala walisubiri wapiga kura. “Hali ya kituo ni shwari ingawa
tunakaa hata nusu saa hajatokea mtu kuja kupiga kura, mfano kituo chetu
kina majina 432 waliotakiwa kupiga kura lakini mpaka saa tisa hii
waliopiga ni kama 100, alisema Epifania Tembo msimamizi wa kituo namba
tano Mgeninani. Shaban Juma mkazi wa kata hiyo alidai watu waliopiga
kura ni wachache kwa sababu uchaguzi huo unarudiwa mara ya tatu baada ya
madiwani wawili kufariki nyakati tofauti.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment