UTENGAMANO
miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC)
umeelezwa kuwa legelege huku ukishindwa kuwashirikisha wananchi,
wataalamu na vyama vya siasa katika mchakato wa uundwaji wake.
Aidha ili kuufanya uwe imara imeshauriwa nchi wanachama kupanua wigo
wa kushirikiana kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ile ya elimu kwa
kuhakikisha wanahuisha na kufanya mifumo yao ya elimu ili ifanane.
Hayo yalielezwa juzi kwa nyakati tofauti na watoa mada kwenye
kongamano kuu la mwaka la asasi za kirai nchini kujadili fursa na
changamoto za utengamano wa EAC uliojumuisha washiriki 25 toka nchi
wanachama wa EAC.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema
mtengamano wa EAC ni legelege, kwani unaegemea masuala dhaifu kama
sarafu, masuala ya kisiasa zaidi jambo alilodai hayawezi kuufanya ukawa
imara kwani ni wa hiari zaidi.
Alisema mtengamano madhubuti ni ule unaotokana na wananchi na sababu
za lazima kama vile masuala ya kiusalama ambao huchangia kuundwa
serikali moja.
Alisema mtengamano wa EAC ni teketeke, kwani unawategemea marais wa
nchi wanachama pekee kuendelea kuwepo huku ukishindwa kuwashirikisha
wananchi, wataalamu hata vyama vya siasa toka nchi wanachama.
Dk. Kitila Mkumbo alisema nchi wanachama zinaweza kuongeza mtengamano
kwa kuamua kuweka viwango vya elimu sawa kwenye nchi zote tano.
Alisema kuwa hiyo itawezesha wanafunzi wa nchi wanachama kuweza
kuhamia kusoma nchi yoyote bila matatizo jambo alilodai kuwa ni afya kwa
mtengamano.
Dk. Kitila alisema kwenye masuala ya lugha ingewezekana walimu wa
Kiswahili kutoka Tanzania wakaenda kufundisha nchi nyingine huku Rwanda
na Burundi ikisambaza wale wa Kifaransa na Kenya na Uganda ikatoa walimu
wa Kiingereza, jambo alilosema kuwa lingesaidia kuongeza kasi ya
mtengamano.
Alishauri nchi wanachama wakarejesha Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki
kilichozinduliwa na Mwalimu Nyerere mwaka 1963, ili kiendelee kuzalisha
wataalamu.
Naye mshiriki wa kongamano hilo kutoka Tanzania, Moses Adam Allan,
alisema lazima mfumo wa elimu uliopo ubadilishwe, ili uwawezeshe
wahitimu kukuza uchumi wa ukanda huu tofauti na sasa ambapo wahitimu
wengi wanarandaranda kutafuta ajira.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment