Arusha. Dalili za amani na usalama Mkoa wa
Arusha zimeanza kuonekana mapema baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa kuwakutanisha viongozi mbalimbali vya vyama vya siasa, dini na
wabunge wa vyama tofauti kujadili changamoto kuu katika suala la amani.
Katika kipindi cha hivi karibuni, Arusha umekumbwa
na vurugu za hapa na pale hali iliyosababisha baadhi kupoteza maisha
katika matukio tofauti likiwamo bomu lililolipuka katika mkutano wa
kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa Chadema eneo la Soweto na kuua
watu 4 na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa.
Katika mkutano uliofanyika jana, ilitolewa kauli
moja ya kuitisha mkutano mkubwa wa amani utakaofanyika Desemba 6 mwaka
huu katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Mkutano huo utawashirikisha wafuasi kutoka vyama
mbalimbali vya siasa, dini tofauti na wale wasio na vyama ambapo katika
makubaliano yaliyoafikiwa kuelekea katika mkutano huo mojawapo ni
washiriki kutovaa sare za vyama vyao.
Akifungua mkutano huo, Msajili Francis Mutungi
alisema kuwa lengo la ofisi yake kuwakutanisha wadau hao ni kutafuta
amani mkoani Arusha.
Alisema kuwa hakuna mtu anayestahili kuipuuza
amani katika Mkoa wa Arusha, ambao unachangia pato kubwa la taifa
hususan katika sekta ya utalii.
Mutungi alisema wakazi wa Arusha wanapaswa
kuzingatia amani katikati ya udini na ukabila. “Ni jukumu la kila
mwananchi kuhakikisha anasaidia kuleta amani katika eneo lake kwa
kushirikiana na viongozi wa serikali na jeshi la polisi,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema kuwa changamoto kubwa katika mkoa wake ni suala la amani.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment