Home » » Vyama vya siasa kufanya mkutano mkubwa Arusha

Vyama vya siasa kufanya mkutano mkubwa Arusha

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini,Jaji Francis Mutungi
 
Vyama vya siasa mkoa wa Arusha vimekubaliana kufanya mkutano mkubwa wa hadhara wa pamoja utakaomaliza tofauti zao kwa lengo la kudumisha amani mkoani humo.
Hayo yalisemwa jana na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali na viongozi wa siasa mkoani Arusha, ulioandaliwa na ofisi ya msajili mkoani hapa.
Jaji Mutungi alisema kuwa lengo kubwa la kufanya mkutano wa pamoja ni kuhamasisha amani kwa ajili ya kuendeleza upatikanaji wa watalii wanaokwenda mkoani hapo kutembelea vivutio mbalimbali.

Alisema kuwa mkutano huo utafanyika katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid na viongozi wa siasa wa mkoani tu ndiyo watakaoruhusiwa kuvaa sare za vyama.

“Lakini kule jukwaani watakakokaa viongozi wa vyama vote vya siasa, kutakuwa na bendera kubwa  za vyama vyote, lengo hapa kuleta ushirikiano katika masuala ya maendeleo na kuhamasisha amani,” alisema Jaji Mutungi.

Alisema Arusha kwa muda mrefu kumekuwa na matukio ya kusikitisha kuanzia makanisa mabomu yanalipuka na baadhi ya mikutano kupigwa mabomu ambayo yanaathiri maendeleo na taifa kwa ujumla kutokana na baadhi ya watalii kuogopa kurudi nchini.

“Mimi nimezunguka kwa baadhi ya hoteli hapa Arusha kujaribu kuongea nao kutokana na mabomu yaliotokea watalii wamepungua au hoteli zimeathirika kiwango gani, wengi waliniambia watalii waliokuwapo wakati haya yakitokea walisema hawatarudi tena,” alisema Jaji Mutungi.

Naye Mkuu wa Mkoa Arusha, Magesa Mulongo, aliwasihi waandishi wa habari kuunga mkono safari mpya ya wanasiasa mkoani humo iliyoanza na siyo kuongeza chumvi katika habari zao ili kuuza magazeti.

Alisema yeye na Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, wamemaliza tofauti zao na sasa wanaweza kukaa meza moja.

Kwa upande wake Lema, alisema kuwa mgogoro wake na mkuu wa mkoa huo, uliisha na sasa wanafanya kazi pamoja.

Aliiomba ofisi ya msajili kutenda haki na vyombo vingine, kwa sababu msingi wa amani ni tunda la haki.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa