Home » » Smile kutoa huduma ya mtandao bure

Smile kutoa huduma ya mtandao bure

KAMPUNI ya mawasiliano ya Smile imeahidi kutoa huduma ya mawasiliano, (internet) bure kwa baadhi ya shule za sekondari za serikali ili kuwawezesha wanafunzi kusoma kupitia mitandao.
Meneja Mauzo wa  kampuni hiyo, Deo Ndejembi,  alibainisha hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kwenye hafla fupi ya  uzinduzi wa mtandao wa Smile mkoani hapa.
Alisema shule zitakazonufaika na mpango huo ni zile zenye maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha elimu nchini.
Ndejembi alisema pia mpango huo unalenga kuimarisha huduma za maabara katika shule za sekondari za serikali kwa kuwawezesha wanafunzi kupata taarifa sahihi zilizoko kwenye mitandao mbalimbali, hivyo kwenda sambamba na ushindani wa kielimu katika soko la dunia.
“Mpango huu utazinufaisha zaidi shule ambazo zina maabara pamoja na kompyuta, hivyo hata zile shule ambazo hazina maabara zinatakiwa kuweka mara moja ili ziweze kunufaika na mpango huu,” alisema Ndejembi.
Alisema mpango huo pia utakuwa chachu na motisha kwa shule za kuwa na maabara za kisasa zaidi, ili ziweze kupata teknolojia ya mawasiliano bure jambo alilodai anaamini litaongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kwenye masomo ya sayansi.
Mpango huo wa kutoa huduma za tekonlojia bure tayari umeshaanza kwa shule 10 za jijini  Dar es Saalam ambapo kwa jiji la Arusha shule moja ya Arusha imeshanufaika na mpango huo.
Ofisa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, (TCRA), Innocent Mongi, alisema anaamini kuingia kwa mtandao huo kutasaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi katika jiji  la Arusha.
Alisema mtandao wa Smile wenye kasi zaidi utawawezesha wafanyabiashara wakubwa na wadogo kufanya biashara kutoka katika masoko mbalimbali duniani kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ile ya utalii na madini.
Chanzo;Tanzania Daima
Smile

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa