SERIKALI
imetangaza kuwa kuanzia mwaka wa masomo 2014/15 vyuo vyote vya ufundi
nchini vitaendesha mafunzo ya kozi zenye ithibati ili kuondoa usumbufu
kwa wahitimu.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alitoa
kauli hiyo alipofungua mkutano wa kitaifa wa wakuu wa vyuo vya ufundi
nchini ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na
kufanyika jijini hapa.
Pia alitangaza kuanza kwa mtaala wa Stashahada ya Elimu ya Msingi
ambao utaanza kutekelezwa kwa vyuo vilivyo na sifa kuanzia mwaka wa
masomo wa 2014/15 na kusistiza kuwa atalazimika kutumia polisi kukagua
na kuvifunga vyuo ambavyo wamiliki wake wanashindwa kutekeleza masharti.
“Siku hizi kumeibuka wimbi kubwa la vyuo holela vinavyoendeshwa
pasipo kuzingatia vigezo vilivyowekwa na NACTE. Jamii imeendelea
kuhujumiwa na watu wanaojitafutia fedha kwa njia za mkato, hasa
wanaojitangaza kutoa elimu ya ufundi tena kwa ada ndogo,” alisema.
Aliwaasa wazazi na walezi kabla ya kuwapeleka watoto wao kujiunga na
vyuo vya ufundi wahoji mambo muhimu ikiwa ni pamoja na usajili wa vyuo
hivyo na taaluma za wakufunzi wake ili wawe na uhakika na taalum
inayotolewa kwa watoto wao.
Aliliagiza baraza hilo ikiwa katika kutekeleza agizo hilo watakumbana
na kikwazo chochote, ofisi yake itatoa ushirikiano kuhakikisha tatizo
la kozi zisizotambuliwa linadhibitiwa.
Katibu Mtendaji wa NACTE, Dk. Primus Nkwera, alivitaka vyuo na
taasisi za elimu za ufundi nchini zinazotoa mafunzo bila kusajiliwa
pamoja na wale wote wenye nia ya kuanzisha vyuo vipya kuhakikisha vyuo
vyao vinapata usajili kutoka baraza hilo kwa mujibu wa sheria.
“Baraza linapenda kuwasisitizia wadau wote ikiwamo wazazi, wanafunzi
na umma kwa uiumla kujiunga na vyuo vilivyosajiliwa na Baraza na si
vinginevyo,” alisema.
Alisema matarajio ya soko la ajira ni kuona vyuo vinatoa wahitimu
wenye ujuzi na maarifa yanayokidhi viwango vya utendaji kazi katika
taaluma husika.
Mwenyekiti wa NACTE, Mhandisi Steven Malote, alisema baraza hilo
limeweka mfumo wa Tuzo za Kitaifa za Elimu ya Ufundi ambazo
zimeunganishwa na Tuzo za Kitaifa za Ufundi Stadi (NVA), ili kuwa na
ngazi kumi za Mfumo wa Kitaifa wa Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi
(TVET).
Chanzo;Tanzani Daima
0 comments:
Post a Comment