Home » » Utengamano kuimarisha EAC

Utengamano kuimarisha EAC

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), itakuwa imara na endelevu endapo msingi wake utakuwa ni  mtengamano baina ya wananchi wa nchi husika na si wakuu wa nchi husika.
Aidha elimu inatakiwa kutolewa zaidi kwa wananchi juu ya faida na changamoto za EAC jambo litakalowezesha kufikiwa kwa malengo ya kuanzishwa kwa jumuia.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, wakati akifungua Kongamano Kuu la Mwaka la Asasi za Kiraia nchini na kuhudhuriwa na wajumbe toka nchi wanachama wa EAC linalofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Arusha (AICC).
Alisema kuwa muungano wa mataifa haya ni muhimu kwa maendeleo na utafanikiwa tu endapo mchakato wake utaamuliwa na raia wa nchi husika baada ya kupima na kuona watanufaikaje na chombo hicho.
“Mtangamano msingi wake ni wananchi na raia wa Afrika Mashariki wakiumiliki ndiyo utakuwa na afya, kama ambavyo Rais, Jakaya Kikwete amekuwa akisisitiza kuwa maamuzi ya kusonga mbele kwenye mchakato huu yatatokana na wananchi na si viongozi,” alisema Mongela.
Kwa upande wake mtoa mada katika kongamano hilo,  Dk.  Azavel Lwaitama, aliwataka viongozi hapa nchini kuelewa kuwa uwepo wa Tanzania kwenye EAC ni zaidi ya ndoa na talaka kwa kile alichodai kuwa hawana uelewa wa kutosha juu ya mashirikiano yaliyopo baina ya wananchi wa mipakani.
“Tatizo la viongozi wetu hawa wengine sijui  wanatoka Lindi? Hawajui ni kiasi gani wananchi wa mipakani wanashirikiana.
“Kutengamana sio suala la kuoa na kuoana na kupeana talaka bali ni  suala la uwekezaji mpana. Nasikitika hata wabunge wa Tabora ambao wako mpakani hawaelewi hili,” alisema Lwaitama.
Alizitaka  asasi za kiraia kwenda kukusanya maoni ya wananchi hasa maeneo ya mipakani ili sauti za wananchi hao zisikilizwe ijulikane ni kiasi gani wanahitaji EAC huku akitolea mfano wa baadhi ya maeneo ya Tanzania, Uganda na Rwanda kuwa wanatumia lugha moja katika mawasiliano.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Nchini, Deus Kibamba, alisema kuwa endapo  mtangamano wa EAC utabaki kuwa kwa viongozi pekee unaiweka jumuia hiyo kwenye hatari ya kuvunjika kama ile ya awali iliyovunjika mwaka 1977.
Alisema kuwa hiyo inatokana na ukweli kuwa viongozi hao wakigombana kama ilivyokuwa wakati ule Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, walipotofautiana na yule wa Uganda Idd Amini jumuia ikavunjika.
“Tunataka wananchi ndiyo wahusike kwenye mtangamano huu, kwa sasa jambo hili halifanyiki; nchi tano zinaungana tulitegemea madaraka ya nchi wanachama yaanze kuachiwa kidogokidogo na kupelekwa kwenye EAC lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zimeshafanyika katika hilo,” alisema Kibamba.
Alisema kuwa mwaka 2010 Kenya iliandaa Katiba mpya ilitegemewa kuwa watajipunguzia baadhi ya madaraka na kuyapeleka EAC lakini hiyo haikufanyika hata hapa nchini kwenye Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba haijafanyika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, John Ulanga, alisema kuwa mkutano huo wa siku mbili umezishirikisha asasi za kiraia za Tanzania ambapo wamekaribisha asasi nyingine 25 toka nchi wanachama wa EAC ambapo lengo kuu ni kujadili namna ya  kuboresha ushiriki wa wananchi katika utengamano wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa