Arusha. Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib
Bilal, anatarajiwa kufungua Mkutano wa Kimataifa wa Vyuo vilivyopo
katika nchi za Jumuiya ya Madola Afrika vinavyotoa elimu na mafunzo ya
ufundi (CAPA).
Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Dk Richard
Masika alisema jana kuwa, mkutano huo utakaofunguliwa kesho, utakuwa wa
siku mbili na utafanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC)
uliopo mjini hapa.
Alisema, Tanzania imeteuliwa kuwa mwenyeji wa
mkutano huu wa Novemba, 2013 na umeandaliwa na Taasisi na Chuo cha
Ufundi Arusha (ATC), Chuo cha Usafirishaji Dar es Salaam (NIT) na
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta).
Dk Masika alisema, umoja huo una jumla ya
wanachama 173 ambao ni taasisi zinazotoa elimu na mafunzo ya ufundi kwa
wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na kuendelea katika nchi 18 za
Afrika.
Aidha kauli mbiu katika mkutano huo ni “Nafasi ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Afrika katika kuoanisha walichojifunza
wahitimu (stadi) na mahitaji ya soko la ajira.
Dk Masika alisema, mkutano huo utajikita katika
kujadili masuala mbalimbali ya kuondoa tofauti kati ya mafunzo ya elimu
ya ufundi na mahitaji ya soko la ajira pamoja na kutengeneza fursa za
kukuza ajira kupitia Mfumo wa elimu wenye kuzingatia ujuzi na umahiri.
Pia mkutano huo utajadili changamoto ya mafunzo ya
Elimu na Ufundi katika stadi zinazoibukia na kukuza ujasiriamali kwa
maendeleo endelevu.
Alifafanua zaidi kuwa, watajadili pia maswala ya
utafiti, uvumbuzi na ubunifu katika kuhakikisha vyuo vya elimu na
mafunzo ya ufundi vinakuwa endelevu.
Chanzo Mwananchi
Chanzo Mwananchi
0 comments:
Post a Comment