WATANZANIA wametahadharishwa kuwa makini katika kuingia ubia na
wawekezaji wa kampuni za kutoka nje ya nchi, kwa kuwa wengi wao huwa na
ajenda binafsi za kunufaika wao na kuwaacha wazawa wakiendelea kuwa
maskini.
Tahadhari hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Martin Kariongi,
mkurugenzi wa Kampuni inayojihusisha na miradi ya kusaidia jamii ya
wafugaji wa Kimasai katika wilaya za Longido, Simanjiro na Same ya
Ilaramatak Olkonorei, ambayo pamoja na miradi ya kijamii pia inamiliki
redio ya kijamii ya ORS.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kariongi alisema amelazimika
kutoa angalizo hilo kwa Watanzania na serikali kwa ujumla kwa kuwa ni
sehemu ya wahanga wa jambo hilo kutokana na mgogoro uliopo sasa baina
yake na wabia wenza katika mjumuiko wa Kampuni ya Omasi Group ambayo
inamiliki ranchi ya jamii ya Ormoti iliyopo Terati – Simanjiro, viwanda
vitano vya kusindika maziwa, machinjio ya kisasa Terati, uzalishaji wa
umeme na maji na kiwanda cha mkaa.
Baada ya kufanikiwa kuanzisha makampuni hayo kupitia ubia wa pamoja
na kupata fedha kutoka taasisi ya kijamii ya kutoa misaada ya nchini
Uholnzi ya SHGW kama misaada ya kuimarisha miradi hiyo ya kijamii, hali
ilianza kubadilika kwa wazawa kuonekana ni mizigo kwa Waholanzi hao na
kuanza kuanzisha makampuni ndani ya kampuni kwa siri ili kujimilikisha
miradi hiyo.
“Hayo yote yanatokea kutokana na unyonge wetu sisi Watanzania na
ukarimu kwa kudhani kuwa wawekezaji wote wanakuja hapa nchini kwa lengo
la kusaidia jamii kumbe sivyo, wengine wanakuja kwa malengo maalumu ya
kujinufaisha kupitia mgongo wa wazawa,’’ alisema Kariongi.
Alisema ameshangazwa kuona katika vyombo vya habari matangazo
yakitolewa ya kusitisha ufadhili katika makampuni hayo yanayogharamiwa
na kwa gharama kubwa na kupigia debe kampuni zao binafsi ambazo
walianzisha kwa mgongo wa ubia na kupata misamaha ya kodi.
Alifafanua kama hali imefikia hapo ni bora sasa serikali ikafuatilia
suala hili kwa kina ili kama sheria inaruhusu basi wabia hawa ambao
wamejitenga watozwe kodi stahiki kulingana na sheria za nchi na
wasiachwe kunufaika.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment