Home » » FAO WATOA DOZI MIL.3.9 ZA CHANJO YA SOTOKA YA MBUZI NA KONDOO

FAO WATOA DOZI MIL.3.9 ZA CHANJO YA SOTOKA YA MBUZI NA KONDOO


WOAH, AU-IBAR kuongeza takribani dozi Mil.6 nyingine

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limeikabidhi Serikali ya Tanzania dozi Mil. 3.9 za chanjo ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo kwenye hafla iliyofanyika leo Julai 16, 2024 wakati wa Ufunguzi wa Warsha inayohusu Ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kwenye eneo la Afya ya wanyama jijini Arusha.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa chanjo hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amelishukuru Shirika hilo kwa msaada huo ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo inaunga mkono mipango ya Serikali kupitia Wizara yake kwa mwaka huu wa fedha ambapo imetenga takribani Shilingi Bil. 28 kwa ajili ya kuendesha zoezi la chanjo ya mifugo nchi nzima.

Prof.Shemdoe ametoa rai kwa Mashirika mengine ya kimataifa na wadau wa Sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika eneo la uboreshaji wa afya ya wanyama ambapo amewaomba FAO kuongeza dozi nyingine za chanjo ili kukidhi idadi ya wanyama waliopo.

“Lakini pia kipekee niwashukuru sana Shirika la kimataifa la Afya ya wanyama (WOAH)  kwani nao wametuambia wapo tayari kutoa zaidi ya dozi Mil.3 huku Shirika la Umoja wa Afrika linaloshughulikia ustawi wa wanyama (AU-IBAR) wakikusudia kutupa zaidi ya dozi Mil.2 kwa hiyo kwa haraka haraka unaweza kuona wadau wetu hawa watakuwa wametupa takribani  dozi Mil.10” Ameongeza Prof. Shemdoe.

Kwa upande wake Mwakilishi wa FAO Bi. Stela Kiambi ambaye ndiye aliyekabidhi chanjo hizo amesema kuwa Shirika lake linatambua kuwa afya bora ya wanyama inachangia afya bora ya binadamu hivyo Shirika lake litaendelea kushirikiana na Wizara kwenye kampeni yake ya kutoa chanjo ya wanyama nchini kote inayotarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa.

Naye Mwakilishi wa kanda ya Afrika Mashariki kutoka  Shirika la kimataifa linaloshughulikia afya ya Wanyama (WOAH) Dkt. Samuel Wakhusama amesema kuwa Shirika lake limeandaa Warsha hiyo kwa kushirikiana na mashirika mengine ili kujadili namna ya kutokomeza magonjwa ya Sotoka na Mbuzi na Kondoo na ule wa kichaa cha Mbwa ifikapo mwaka 2030.

“Tunataka nchi zetu zihakikishe  wanyama wanaouzwa wapo salama kiafya na wale wanaonunua wanyama hao wawe na uhakika na usalama wao na ndio maana tumekutana hapa ili kujadili kwa pamoja Serikali na Sekta binafsi  na kupata suluhu ya kuangamiza magonjwa ya wanyama kwa njia rahisi” Amesisitiza Dkt. Wakhusama.

Warsha hiyo ya kujadili Ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kwenye eneo la Afya ya wanyama imeandaliwa na  Shirika la kimataifa linaloshughulikia afya ya Wanyama (WOAH) na inatarajiwa kuhitimishwa Julai 18, 2024 jijini Arusha.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa