Na Beatrice Lyimo- MAELEZO
Serikali
ya Zanzibar imeipa kipaumbele sekta ya afya na kutoa huduma za afya
zenye ubora kwa kuwafikia wananchi wote ili kuboresha afya zao kwa
kuzingatia afya bora ni raslimali muhimu kwa maendeleo endelevu.
Afya
ni hali ya ukamilifu kimwili, kiakili, kijamii na kutokuwepo kwa
maradhi. Afya bora ni nguzo na raslimali muhimu katika kuchangia
maendeleo ya mtu binafsi, familia na nchi hususan katika kuleta maisha
bora na kupunguza umaskini.
Kwa
mantiki hii afya inalenga kuwa na ustawi endelevu wa jamii, kwa
kuzingatia mchango wa mtu binafsi kulingana na nafasi, uwezo na fursa
zilizopo katika kuleta maisha bora.
Uhakika
wa upatikanaji wa huduma bora za afya wenye lengo la kuiwezesha jamii
kuwa na uwezo wa kushiriki, kuamua, kupanga na kutekeleza mikakati yao
ya kuwaletea maendeleo katika ngazi mbalimbali.
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kwa dhati
kuimarisha huduma za afya za kinga na tiba na kuendeleza ustawi wa watu
wa Zanzibar kwa kutilia mkazo zaidi wanawake, watoto pamoja na makundi
mengine yanayoishi katika mazingira magumu.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya afya yapo mafanikio kadhaa
yaliyotekelezwa na Serikali katika sekta ya afya baada ya Mapinduzi 1964
ili kuimarisha sekta hiyo katika utoaji huduma kwa wananchi.
Baadhi ya mafanikio hayo ni pamoja na utoaji
chanjo kwa watoto, Wizara kutekeleza mikakati mbali mbali ikiwemo
mafunzo ya utoaji wa chanjo 172 katika wilaya zenye kiwango kidogo cha
chanjo, uchapishaji na usambazaji wa vipeperushi 7,250 na mabango 7,500
kwa jamii na vituo vya afya.
Kwa
upande wa Huduma za Uzazi, Miongoni mwa mbinu zinazotumika katika
kuhakikisha mama wajawazito wanajifungua katika vituo vya afya na
hospitali Wizara imeanzisha mpango maalumu katika wilaya ya Kaskazini B
ili kufikia lengo hilo.
Mpango
huu unatumia wafanyakazi wa jamii wa kujitolea ambao huwatembelea mama
wajawazito majumbani mwao kwa lengo la kuwaelimisha juu ya masuala hayo
ambapo Jumla ya wajawazito 674 wamekwishanufaika na mpango huo tangu
mradi kuanzishwa kwake mwishoni mwa mwezi wa Machi, 2016.
Katika
kutekeleza juhudi za kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga,
Serikali ilifanya mapitio ya muongozo wa kufanya tathmini ya vifo vya
uzazi na watoto wachanga ili kuhakikisha inalinda afya ya mama na mtoto
ambao ndio rasilimali ya taifa.
Huduma
za uzazi wa mpango ziliendelea kutolewa kwa kununua dawa za uzazi wa
mpango na kusambaza katika vituo vya afya Unguja na Pemba kwa msaada wa
Shirika la Kushughulikia Idadi ya Watu Duniani.
Aidha,
kupitia mradi huo, Serikali inaendelea na ujenzi wa mashimo ya kutupia
taka za mazalio katika vituo vinane vya Nungwi, Pwani Mchangani, Uroa,
Uzini na Selem kwa Unguja na Mkia wa Ng'ombe, Tundauwa na Fundo kwa
Pemba. Vile ujenzi wa vinu vya kuchomea taka taka za hospitali vinajengwa katika hospitali za VItongoji, Micheweni na Wete.
Ili
wananchi wawe na afya bora kwa kuwasogezea huduma za afya karibu na
maeneo yao, Wizara ya Afya imeendelea kutekeleza mradi wa kupandisha
hadhi hospitali za vijiji kuwa za wilaya na wilaya kuwa za mkoa kwa
kuimarisha majengo na kuongeza huduma, vifaa na rasilimali watu ili
kutoa huduma za afya stahiki kwa wananchi.
Katika
hatua hiyo, katika ufunguzi wa hospitali ya Abdalla Mzee, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein
aligiza Wizara ya Afya kujipanga na kuhakikisha uwepo wa nguvu kazi ya kutosha itakayowezesha kupatikana huduma masaa yote.
Sanjari
na hilo, Dkt Shein aliwataka viongozi wa hospitali hiyo kusimamia vyema
na kuilinda miundombinu iliyowekwa pamoja na utunzaji wa vifaa ili
iweze kuwahudumia wananchi kulingana na malengo yaliyokusudiwa.
Aidha, Dkt Shein aliwataka wananchi
kutumia kikamilifu fursa ziliopo za kupatiwa huduma za matibabu na
uchunguzi katika hospitali hiyo wakati wote na kuondoa mazoea ya waweze
kuhudumiwa kulingana na utaratibu utakaopangwa na Wizara ya Afya.
Ili
kupunguza gharama za kusafirisha wagonjwa nje ya Zanzibar na nje ya
nchi, Serikali imechukua hatua za makusudi kuipandisha hadhi Hospitali
ya Mnazi Mmoja kuwa ya Rufaa ambapo Wizara
imekarabati jengo la Wodi ya Watoto ulioanza Disemba 2014, na
kutekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Rans iliyopo hapa Zanzibar.
Ujenzi
huo uliogharimu jumla ya Tsh bilioni 2.4 ambapo Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar imechangia Tsh 495,000,000 na fedha zilizobaki zimechangiwa
na Serikali ya Norway kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Haukeland
Bergen cha nchini humo.
Pia kumekuwa na mradi Shirikishi wa Kudhibiti Maambukizo ya Ukimwi, Kifua Kikuu na ambapo katika huduma za Uchunguzi wa VVU, Zanzibar
ina vituo vya utoaji ushauri nasaha na upimaji wa VVU vipatavyo 98
vikiwemo 76 vya serikali, 10 vya Jumuiya zisizo za Serikali, vinne vya
taasisi za dini na vinane vya binafsi.
Hatua hiyo imeifanya Zanzibar kwa mwaka 2015 kuwa na jumla ya watu 101,669 walipatiwa ushauri nasaha na upimaji wa vvu.
Kati yao 48,601 ambao ni sawa na asilimia 48 walikuwa wanawake na 53,068 sawa na asilimia 52 walikuwa wanaume. Kati ya waliopima asilmia 1.2 waligunduliwa na Virusi vya UKIMWI. Vile
vile jumla ya watoa huduma za afya 32 walipatiwa mafunzo msasa juu ya
ushauri nasaha na upimaji wa VVU pamoja na mafunzo msasa kwa watoa
huduma 30 Unguja na Pemba juu ya upimaji na ushauri nasaha kwa watoa
huduma hiyo.
Kwa upande wa huduma za Tiba, wizara imemarisha
tiba na ushauri nasaha ambapo jumla ya kliniki 12 zinatoa huduma na
tiba (8 Unguja na 4 Pemba) kwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU).
Hadi
kufikia mwisho wa mwezi Disemba 2015 jumla ya wagonjwa 8,721 walikuwa
tayari wameshasajiliwa kwenye kliniki hizo, miongoni mwao ni wagonjwa
6,251 sawa na asilimia 71.7 walianzishwa dawa za kupunguza makali ya VVU
(ARVs) wagonjwa waliobaki kwenye dawa mpaka kufikia Machi 2016 ni
3,978.
Kazi
nyengine iliyofanya ni kukusanya sampuli za damu za watoto ambao mama
zao wameambukizwa na virusi vya UKIMWI na kupelekwa Hospitali ya
Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo jumla ya sampuli 171
zimepelekwa katika hospitali hiyo, kati ya sampuli hizo 146 zimetolewa
majibu watoto wawili kati yao waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU.
Katika
jitihada za kuimarisha nguvu kazi ya taifa, Serikali inaendelea
kupambana na tatizo la madawa ya kulevya kwa kupunguza athari kwa vijana
walioathirika na madawa hayo kwa kuwapatia dawa aina ya methadone ili
kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya.
Hatua
hiyo imesaidia jumla ya vijana 168 kuendelea na matibabu hayo katika
kituo maalumu kilichopo katika hospitali ya wagonjwa wa Akili Kidongo
Chekundu ambapo masuala ya utawala Kamisheni inayohusiana na dawa za
kulevya ipo chini ya Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais.
Kwa
upande wa kifua kikuu jumla ya wagonjwa 457 waligundulika kuwa na
ugonjwa huo ambapo wagonjwa 262 wapo Unguja na 195 wapo Pemba. Sambamba
na hilo, jumla ya wagonjwa 193 wamefuatiliwa katika familia zao, watu
667 walipata elimu juu ya kujikinga na maradhi hayo, kati yao wanne
walikuwa na dalili na mmoja alithibitika kuwa na kifua kikuu.
Katika
kupunguza ulemavu utokanao na Ukoma, zoezi la kuwafuatilia watu
walioambukizwa na ugonjwa wa ukoma limefanyika Unguja na Pemba, kwa
lengo la kuwatambua wale ambao wanaweza kufanyiwa urekebishaji wa
viungo.
Katika zoezi hilo, jumla ya watu watano wamepatikana kutoka Wilaya ya Kusini Unguja na wanategemewa kufanyiwa upasuaji.
Aidha,
uchunguzi ulifanyika katika Shehia 15 za Wilaya ya Kusini Unguja,
ambako ugonjwa huu umeenea. Katika uchunguzi huo jumla ya watu 2,275
walichunguzwa, kati yao watu 215 walikuwa na maradhi ya ngozi na watu 40
waligundulika na maradhi ya Ukoma ambapo matibabu stahiki yalitolewa
kwa wale wote waliogunduliwa na maradhi hayo.
WIZARA
ya Afya imeeleza miongoni mwa juhudi zake inazoendelea kuzichukua
katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika ni pamoja na kuwapeleka
wataalamu wake wa fani mbali mbali masomoni ili kuendelea kujenga uwezo
na kuelekea kwenye kujitegemea.Hayo yameelezwa na uongozi wa Wizara
hiyo, huko Ikulu mjini Zanzibar katika kikao maalum kati ya Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na
uongozi wa Wizara hiyo ilipokuwa ikiwasilisha Taarifa yake ya
Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara kwa kipindi cha Julai hadi Septemba
katika Bajeti ya mwaka 2016-2017.
Katika
maelezo yake, Waziri wa Wizara hiyo Mahmod Thabit Kombo amesema kuwa
Wizara bado inaendelea kupata mafanikio makubwa katika kuendeleza
miundombinu yake hasa katika hospitali mpya ya Abdalla Mzee na kuweka
vifaa vipya na vya maabara.
Waziri
Kombo alitumia fursa hiyo kueleza majukumu Makuu ya Wizara hiyo ambapo
pamoja na majukumu hayo Wizara imezingatia Sera, Mipango na mikakari
mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa ikiwa ni pamoja na Malengo ya
Maendeleo Endelevu 2030, Dira ya Zanzibar 2020, Sera ya Afya 2011,
Mpango Mkakati wa III wa Sekta ya Afya pamoja na Utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwak 2015-2020.Uongozi huo pia, ulizipongeza juhudi
za Dk. Shein anazozichukua katika kuwapa maelekezo na ushauri ambao
unaendelea kuwasaidia katika utendaji wao wa kazi.
Katika
suala zima la upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya, uongozi huo
umezipongeza juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kuhakisha Bohari
yake kuu inazo dawa za kutosha.Uongozi huo pia, ulieleza juhudi za
makusudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara hiyo katika uanzishwaji wa
Bima ya Afya pamoja na hatua zilizofikiwa.
Mapema
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein alizipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara hiyo
katika utoaji huduma ya afya kwa wananchi hapa nchini.
Dk.
Shein alieleza haja ya kuendelea na utaratibu wa kuwapa mafunzo
watendaji wa Wizara hiyo katika kada mbali mbali kwa lengo la kuja kutoa
huduma kwa wananchi huku akisisitiza azma ya Serikali kupitia Wizara
hiyo kuendelea kutoa huduma mbali mbali za upasuaji ambazo zitapunguza
gharama za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.
Aidha,
Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kulipa kipaumbele suala zima la
utafiti ndani ya Wizara hiyo huku akisisitiza suala zima la uzalendo na
kueleza kuwa utaratibu wa kuwapeleka watendaji wa Serikali kufanya kazi
Pemba sio adhabu bali ni taratibu za kiutumishi.
Dk.
Shein aliyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Waziri
wa Nchi Afisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyi Makame Mwadini,
mara baada ya kulifungua jengo la wagonjwa wa nje katika Hospitali ya
Kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika
hotuba hiyo, Dk. Shein alisema kuwa huduma bora za afya kwa wananchi
wote bila ya ubaguzi ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo Chama cha ASP kilichoongoza Mapinduzi hayo
katika manifesto yake, kiliweka bayana azma yake ya kutoa huduma za
afya bure bila ya ubaguzi wakati kitakaposhika hatamu za Serikali.
Dk.
Shein alisema kuwa jitihada kubwa zimefanywa na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar katika kipindi cha miaka 52 ya Mapinduzi katika kuimarisha
huduma za afya kwa kutambua kwamba afya bora ni muhimu kwa wananchi ili
waweze kuishi vyema katika kazi ya kuleta maendeleo ya nchi yao.
Alisema
kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika utekelezaji wa mipango na
mikakati ya kuiendeleza sekta ya afya nchini kupitia vitengo na programu
mbalimbali zinazoendeshwa na serikali kwa ushirikiano na washirika wa
maendeleo.
“Nyote
ni mashahidi wa kuimarika kwa huduma za afya katika hospitali na vituo
vytetu vyote va afya... Aidha, kuna ongezeko kubwa la vituo vya afya vya
daraja mbalimbali kiasi kwamba hivi sasa wananchi wa Zanzibar hawawezi
kwenda zaidi ya kilomita tano bila ya kukuta kituo cha afya” alisema Dk.
Shein.
Akieleza
historia ya huduma za afya katika Mkoa wa Kaskani Unguja, Dk. Shein
alisema kuwa kabla ya mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 katika mkoa huo
kulikuwa na vituo viwili tu vya afya ambavyo vilikuwepo Mkokotoni na
Chaani.
Alisema
kuwa katika kipindi cha miaka 52 ya Mapinduzi Mkoa huo hivi sasa una
vituo vya afya 26 ambapo vituo 18 ni vya daraja la kwanza na 7 ni vya
daraja la pili pia, kuna hospitali ya Koteji ya Kivunge ambayo lengo la
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba ni kuipandisha daraja
kuwa hospitali ya Wilaya.
Dk.
Shein alisema kuwa lengo la mradi huo ulioanza mwaka 2012 ni
kuziimarisha huduma za afya katika hospitali zote za Koteji ili
kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.
Aidha,
Dk. Shein alisema kuwa serikali imekusudia kuzisogeza huduma za afya
kuwa karibu zaidi na wananchi ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji kwa
kinamama wajawazito, huduma za uchunguzi kama vile za maabara, “X-ray”
na “Ultra-sound”.
Pamoja
na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani za dhati kwa
shirika lisilokuwa la kiserikali la Uingereza HIPZ, UNICEF na ROTARY
Club kwa kuiunga mkono serikali katika lengo la kuiimarisha hospitali
hiyo.
Dk.
Shein alisema kuwa huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo
zimeimarika sana baada ya serikali kupitia Wizara ya Afya kuongeza
wafanyakazi, vifaa vya uchunguzi wa maradhi na kuongeza aina za huduma
zinazotolewa katika hospitali hiyo.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi juu ya umuhimu
wa kwenda kujifungulia hospitali na kuhudhuria kliniki ili kupima na
kupatiwa ushauri pamoja na kuhakikisha watoto wanapelekwa vituoni
kupatiwa chanjo kwa kuzingatia kampeni ya chanjo kwa watoto
zinazoendeleshwa na Wizara ya Afya.
“Serikali
itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta
ya afya kwa lengo la kuwapatia huduma bora za afya wananchi wote mjini
na vijijini”, alisema Dk. Shein.
Aidha,
Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote kuendelea kusherehekea
maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa amani na
utulivu.
Nae
Waziri wa Wizara ya Afya Mahmoud Thabit Kombo aliwaeleza wananchi
waliohudhuria uzinduzi wa hospitali hiyo kuwa hatua hizo ni miongoni mwa
ahadi za Dk. Shein kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambazo ameziahidi
na sasa anaendelea kuzitekeleza huku akitoa shukurani kwa washirika wa
maendeleo yakiwemo Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kuiunga
mkono Zanzibar.
Nae
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mohemmed Saleh Jidawi amezitaja juhudi
mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali chini ya uongozi wa Dk.
Shein katika kuhakikisha Hospitali za Koteji kuwa za Wilaya na kueleza
kuwa gharama za ujenzi huo ni milioni 461 chini ya ufadhili kutoka kwa
Shirika la HIPZ.
Dk.
Jidawi alisema kuwa lengo ni kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa ya
Wilaya na kulipongeza Shirika la HIPZ kwa kuendelea na juhudi zake
katika kuiimarisha hospitali ya Kivunge kama ilivyofanya kwa hospitali
ya Makunduchi.
Hospitali
hiyo ina uwezo wa kupokea wagonjwa 120 hadi 140 kwa siku mbapo pia
itafanya kazi kwa masaa 24 kwa kutumia mfumo wa kisasa wa kuwaorodhosha
wagonjwa kwa njia ya Kompyuta kwa lengo la kutunza kumbukumbu za
wagonjwa na muda wa kupanga foleni wakati wa kutoa na kupata huduma.
Nao
washirika wa maendeleo wakiwemo wawakilishi wa HIPZ, UNICEF, ROTARY
CLUB pamoja na uongozi wa Mfuko Taifa wa Bima za Afya wameahidi
kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi katika kuimarisha na kutoa
huduma bora kwa wananchi.
Aidha,
washirika hao walieleza kuwa kituo hicho kitakuwa ni mkombozi kwa akina
mama na kutoa shukurani kwa ushirikiano wanayoyapata kutoka kwa uongozi
wa Serikali ya Zanzibar.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment