Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kushoto) akioneshwa
Ramani ya Kijiji cha Ololosokwan na Diwani wa Kata hiyo, Yanick Ndoinyo alipotembelea kijiji hicho hivi
karibuni kuona changamoto za uhifadhi. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha
Ololosokwan, Emmanuel Salteimoi.
Kundi
la mifugo likiwa ndani ya Pori Tengefu la Loliondo, karibu kabisa na mpaka wa
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akizungumza katika
kikao cha wadau wa mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo alichokiitisha katika ofisi
ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo mkoani
Arusha hivi karibuni.
NA HAMZA TEMBA - WMU
............................................................................
Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John
Pombe Magufuli mara tu ilipoingia madarakani mwezi Oktoba mwaka juzi ilitoa
vipaombele vyake kadhaa vya kutelezwa na wizara zake mbalimbali huku Wizara ya
Maliasili na Utalii ikikabidhiwa majukumu mazito matatu ya kutekeleza katika
kipindi cha uongozi wake.
Majukumu hayo yaliyotolewa na Rais Magufuli
wakati wa hotuba yake ya kwanza ya kulihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mjini Dodoma, ni yale ya kuhakikisha kuwa wizara hiyo inakomesha
vitendo vya ujangili, kuongeza mapato ya serikali na kushuulikia utatuzi wa
migogoro ya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi nchini.
Wizara
ya Maliasili na Utalii, imesema kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa malengo yake
ya uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Kuendeleza Utalii pamoja na utekelezaji
wa vipaombele ilivyopewa na Serikali ya awamu ya tano kuwezesha kufikia malengo
hayo yanatimia kwa wakati.
Kwa upande wa utatauzi wa migogoro kwenye maeneo ya hifadhi
nchini, Wizara hiyo imejipanga kuwashirikisha wadau wote wanaohusika na
migogoro hiyo kwa kukaa nao pamoja kwenye vikao vya majadiliano na kuweka
mikakati ya pamoja ya kufikia suluhu ya migogoro hiyo kwa faida ya Serikali na
wadau wote wanaohusika.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi
Ramo Makani alifanya ziara ya kiutafiti katika Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na
Pori Tengefu la Liliondo, lengo kuu la ziara hiyo ikiwa ni kuona uhalisia wa
changamoto zilizopo pamoja na kupata taarifa sahihi kutoka kwa wadau husika,
alifanya hivyo bila ya kujitambulisha kwa lengo la kupata taarifa sahihi
kuhusiana na migogoro hiyo.
Akiwa katika Tarafa ya Loliondo alitembelea kijiji cha
Ololosokwan, Pori Tengefu la Liliondo, sehemu ya mpaka wake na Hifadhi ya Taifa
ya Serengeti na eneo la muwekezaji, kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) na kampuni ya
&Beyond (Kleins Camp).
Akiwa katika eneo hilo alizungumza na viongozi wa kijiji cha
Ololosokwan ambao waliwasilisha changamoto kadhaa ikiwemo ongezeko la mifugo
kutoka nchini Kenya na vijiji jirani hususani wakati wa kiangazi kwa ajili ya
kutafuta malisho na uelewa tofauti wa mpaka baina ya vijiji na Hifadhi ya Taifa
ya Serengeti.
Diwani
wa Ololososkwan, Yanick Ndoinyo alisema uhifadhi umekuwa ukiwanufaisha kwa
kiasi kikubwa kwa kuwa kupitia utalii kijiji hicho hupata fedha taslim zaidi ya
shilingi milioni 300 kwa mwaka kupitia mikataba ya wawekezaji na mgao kutoka
Serikalini.
Pamoja
na mchango huo amesema “wawekezaji wa eneo hili wamekuwa wakitekeleza miradi ya
jamii ambapo wamechimba visima vinne, wamejenga madarasa mawili na kisima
kingine kinajengwa jirani na kata hii, lakini kampuni zote kwa ujumla zinatoa
ajira kwa wanavijiji, kwahiyo kwakweli sisi ni kijiji ambacho tumeona manufaa
ya utalii “
Ndoinyo
alisema fedha hizo zimekuwa zikisaidia kusomesha watoto masikini kuanzia elimu
ya awali hadi chuo kikuu, kusaidia ujenzi wa zahanati na huduma nyingine za
jamii.
Kwa
upande wa kampuni ya Ortello Business
Corporation (OBC) ambao wamewekeza katika pori hilo kupitia Afisa Mahusiano
wao, William Parmat walisema changamoto kubwa inayowakabili ni ya wananchi
kuingiza mifugo katika eneo la uwekezaji jambo linalosababisha uharibifu mkubwa
wa mazingira ikiwemo wanyamapori kutoweka.
Muwekezaji
huyo alisema wapo tayari kuweka makubaliano ya uhifadhi na wananchi pamoja na
kusaidia kujenga miundombinu ya huduma za jamii. Alisema changamoto ya mifugo
imesababishwa na msukumo wa baadhi ya asasi za kiraia kwa wananchi kwamba
Serikali inataka kuchukua pori hilo hivyo waingize mifugo yao kwa ajili ya
kulilinda.
Naibu
Waziri Makani aliuahidi uongozi wa kijiji cha Ololosokwan pamoja na wawekezaji
hao kuwakutanisha wadau wote wanaohusika na mgogoro wa pori hilo kwa ajili
kujadili changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Akiwa kwenye Pori Tengefu la Loliondo na kwenye mpaka wa Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti alishuhudia makundi ya mifugo ikiwa ndani ya pori hilo na
mingine ikizagaa maeneo ya mpakani na Hifadhi hiyo. Alielezwa na Viongozi wa
Wilaya ya Ngorongoro kuwa, mifugo hiyo huingizwa kwa ajili ya malisho wakati wa
usiku kwenye hifadhi ya Serengeti.
Inaelezwa kuwa eneo la Pori Tengefu la Loliondo lina umuhimu
wa pekee katika uhifadhi kwa sababu ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori, mapito
ya wanyamapori na vyanzo vya maji. Kutokana na sababu hizo, eneo hilo linapaswa
kuendelea kuhifadhiwa ipasavyo, kwa kuwa linachangia kwa kiwango kikubwa
kuimarisha mfumo wa ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti.
Siku chache baada ya ziara hiyo ya kiutafiti, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kikazi mkoani Arusha na kuwaagiza viongozi wa
Serikali kukaa pamoja na wadau wanaohusika na migogoro ya ardhi katika Tarafa
ya Loliondo na kuitafutia suluhu ya kudumu.
Baada ziara hiyo ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri Makani
aliendelea na ziara yake katika tarafa ya Loliondo ambayo aliikatisha kupisha
ziara Waziri Mkuu. Mara hii ziara hiyo ikihusisha pia ufuatiliaji wa maagizo ya
Waziri Mkuu aliyoyatoa kwenye ziara yake mkoani Arusha.
Aliwasili Loliondo kwa
ajili ya kuweka mkakati wa kumaliza changamoto ya mgogoro uliodumu kwa zaidi ya
miaka 25 kati ya mwekezaji, wanavijiji, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs),
suala la mifugo, uharibifu wa mazingira na utata wa mpaka wa Hifadhi ya Serengeti
na Loliondo.
Tarehe 29 Desemba, 2016
alifanya mkutano na wadau wanaohusika moja kwa moja na mgogoro wa Loliondo, mkutano
huo ulifanyika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro,
Tarafa ya Loliondo, Kupitia mkutano huo aliunda kamati maalum ya kutafuta
suluhu ya kudumu ya mgogoro huo.
Kamati hiyo inahusisha
taasisi za serikali, asasi za kiraia, viongozi wa dini, wazee wa kimila
(Leigwanan), viongozi wa vijiji, wajumbe wa kamati teule ya vijiji 15 ya mpango
bora wa matumizi ya ardhi na uendelezaji wa uhifadhi na wawakilishi wa wanawake
na vijana. Aliunda pia kamati ya kuandaa kanuni za kundesha vikao vya kamati
hiyo.
Naibu Waziri huyo
aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro,
Rashid Mfaume Taka akateuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.
“Kamati ya kanuni itumie
muda wa wiki mbili hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2017 iwe imeshakamilisha
rasimu ya kanuni ili tarehe 18 Januari, 2017 tuzipitie, tuzijadili na
kuzipitisha. Hatua itakayofuata ni mawasilisho ya taarifa mbalimbali kutoka kwa
wadau pamoja na majadiliano”, alisema Makani.
Aliagiza pia taarifa
mbalimbali za kamati zilizowahi kushuulikia mgogoro huo miaka ya nyuma na
mapendekezo yake pamoja na taarifa mbalimbali za sheria za uhifadhi na vijiji
kwa ajili ya kusaidia majadiliano hayo ziwasilishwe.
Kikao hicho kilikubaliana
kazi hiyo ifanyike ndani ya miezi mitatu hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2017 iwe
imekamilika na muafaka upatikane kwa ajili ya kuishauri Serikali namna bora ya kumaliza
mgogoro huo.
Wadau wote walikubaliana
kushiriki vikao vya majadiliano huku wengine wakipongeza hatua iliyofikiwa na
Serikali ya kutaka kumaliza mgogoro huo, hata hivyo Naibu Waziri Makani alitoa
angalizo kwa wadau hao; "Kuna watu humu ndani na hata nje ambao hawataki
tumalize migogoro Loliondo, nitoe rai kwao, waache chokochoko.
“Wafikishiwe salamu,
tutawabaini, tutawakamata na kuwashitaki kwa kosa la kukwamisha jitihada za
Serikali kuwaletea wananchi maendeleo yao, Wananchi muone umuhimu wa jitihada
za Serikali kumaliza changamoto hii na kutuunga mkono”, alisema Makani.
Akizungumza katika
mkutano huo, mchangiaji mmoja ambaye hakutambulisha jina lake alisema “Eneo
hili Loliondo lenye kata saba na vijiji 15 lilikosekana dawati la pamoja, kwa
mfumo huu tutaenda mbele, Taasisi nyingi zimekuwa zikipotosha umma kuhusiana na
taarifa za Loliondo, tutashukuru kuona tunapata muafaka kupitia kamati hii
iliyoundwa leo”
Changamoto ya Mgogoro wa
Pori Tengefu la Loliondo ni mkwamo kwa maendeleo ya wananchi wa Loliondo na
Taifa kwa ujumla, Kila mwananchi wa Loliondo ana nafasi kubwa ya kuhakikisha mgogoro huu unafikia tamati kwa
kushirikiana na Serikali na wadau wengine. Kila mmoja atimize wajibu wake
mgogoro huu utakuwa historia na Loliondo itakua salama na kupiga hatua
kimaendeleo.
0 comments:
Post a Comment