Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi
la Polisi mkoani hapa lipo kwenye mkakati wa kuwachukulia hatua
viongozi wote wanaoishi au kufanyia kazi katika maeneo ambayo
yatabainika wananchi wa maeneo yao wanalima bhangi bila wao kuwachukulia
hatua zozote au kutoa taarifa kwa vyombo husika.
Hayo
yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu kamishna (DCP)
Charles Mkumbo alipokuwa anaongea na waandishi wa habari ofisini kwake
baada ya operesheni iliyofanyika katikati ya wiki iliyopita katika
kijiji cha Kismiri Juu, kata ya Uwiro tarafa ya King’ori wilayani
Arumeru,
“Mara
kadhaa tunapofanya operesheni hizo wananchi wa eneo hilo huwa
wanakimbia na kuacha nyumba zao huku viongozi wao kutoonekana kabisa au
kutoa taarifa zozote juu ya uhalifu huo, sasa tutawachukulia hatua kwani
wao ni sehemu ya uwajibikaji katika kuzuia vitendo vya uhalifu”.
Alisema Kamanda Mkumbo.
Katika
operesheni hiyo, jeshi la Polisi lilifanikiwa kupata jumla ya magunia
22 ya bhangi yaliyokuwa yamehifadhiwa katika nyumba za wakazi hao na
kwenye makorongo yanayozunguka kijiji hicho pamoja na kilogramu 80 za
mbegu za mmea huo ambazo zote ziliharibiwa kwa kuchomwa moto.
Kamanda
Mkumbo aliendelea kueleza kwamba, katika operesheni hiyo pia
walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aitwaye Raphael Laizer (33) mkazi
wa Kismiri Juu akiwa na magunia matatu ya bhangi huku taratibu za
kumfikisha mahakamani zikiwa zinaendelea.
Kamanda Mkumbo aliongeza kwa kusema kwamba, imekuwa vigumu kuwakamata watuhumiwa kutokana na jiografia ya eneo hilo ambapo kila kunapokuwa na operesheni askari wanapokwenda, wananchi hao wanawaona kirahisi au kusikia miungurumo ya gari na kisha hukimbilia milimani na kuwaacha wazee na watoto.
“Japokuwa
operesheni hizo ambazo tunazifanya mara kwa mara zimekuwa za mafanikio
lakini changamoto zilizopo ni pamoja na miundo mbinu ya eneo hilo si
rafiki kwa magari hasa uwepo wa milima mirefu na ubovu wa barabara”.
Alifafanua Kamanda Mkumbo.
Operesheni
hiyo iliyofanyika kuanzia saa 12:00 asubuhi mpaka saa 7:30 mchana
ilijumuisha askari wa vikosi na vitengo mbalimbali huku ikisimamiwa na
Mkuu wa Operesheni mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) James
Manyama.
0 comments:
Post a Comment