Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na
Lydia Churi-Mahakama
Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji
wengine wamepongezwa kwa kumaliza vizuri kesi za uchaguzi zilizofunguliwa
katika Mahakama Kuu kanda mbalimbali nchini na pia kutenga muda wa kujadili
changamoto zilizotokana na kesi hizo.
Akizungumza na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania leo jijini Arusha, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande
Othman amewapongeza Majaji hao kwa kujitoa katika kusikiliza kesi hizo na
kuzitolea hukumu kesi nyingi kwa kipindi kifupi licha ya kesi chache kubakia
mahakamani.
Jumla ya kesi 53 za Ubunge zilizotokana na Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015 zilifunguliwa katika Mahakama Kuu kanda za Dar es salaam, Dodoma,
Iringa, Mbeya, Moshi, Mtwara na Mwanza. Kanda nyingine ni Shinyanga, Songea,
Sumbawanga, na Tanga. Kati ya kesi hizo, kesi 31 zilimalizika katika hatua za
awali na kesi 22 ziliendelea, mpaka sasa
kesi 19 zimemalizika. kesi tatu bado ziko mahakamani.
Hata hivyo kesi zote 196 zilizotokana na uchaguzi wa
madiwani zilimalizika mapema katika Mahakama
mbalimbali za Hakimu Mkazi nchini. Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu
kufanyika kwa uchaguzi Mkuu nchini, zaidi ya asilimia 94 ya kesi za uchaguzi
zilizofunguliwa kwenye Mahakama Kuu zimemalizika wakati asilimia 100 ya kesi
zote za udiwani zimemalizika.
Aidha, Jaji Mkuu amewataka Majaji hao kuweka mikakati ya
kuhakikisha kasi ya kupunguza kesi mahakamani hasa zile za muda mrefu
inaongezeka ili kupunguza malalamiko yanayotokana na kuchelewa kutoa hukumu na kutopatikana
kwa nakala za hukumu kwa wakati.
Mheshimiwa Chande amewataka Majaji kusimamia suala la
maadili ndani ya Taasisi hiyo ili kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama yao.
Kuhusu suala la Maadili kwa Mahakimu, Jaji Mkuu amesema
wameomba ushauri Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa endapo hakimu atashtakiwa
kwa kosa la rushwa ataondolewa kazini kwa maslahi ya Umma hata kama atashinda
kesi hiyo.
0 comments:
Post a Comment