KAMA wewe unadhani huna fedha, basi kuna wengine ambao wamezichimbia
ardhini, tena kwa mamilioni. Benki ya chini ya ardhi iliyosheheni
mamilioni ya fedha, zilizoswekwa ndani ya mifuko myeusi ya plastiki na
kufukiwa mchangani, imechimbuliwa na matrekta ya kutengeneza barabara
jijini Arusha huku noti nyekundu zikitawanywa kila kona na kufanyika
kuwa 'Sadakalawe - Amina,' kwa kila mpita njia ambaye angeweza
kujitwalia fungu.
Ilikuwa ni mshikemshike katika eneo la Mianzini mjini hapa, ambako
kuna mradi mkubwa wa upanuzi wa barabara ya kutoka Mianzini Mataa hadi
Ilkiding'a unaoendelea.
Watu walipigana vikumbo katika harakati za kujineemesha na fedha
zilizokuwa zimetapakaa eneo hilo. Ikiwa imesheheni noti tupu, tena
nyekundu na mpya, kufumuliwa kwa akaunti hiyo ya benki ya chini ya ardhi
pamoja na kuwa neema kwa wapita njia na wakazi wa eneo hilo, kuligeuka
pia kuwa kilio kwa mmiliki wa hazina hiyo, Christopher Akoonay maarufu
kama 'Mmbulu' ambaye sasa amejipatia jina jingine la 'Mabulungutu.'
Akonaay ni mkulima, lakini hasa akijishughulisha na ufugaji wa
ng'ombe wa maziwa. Yeye hudamka asubuhi kukamua mifugo hao na kisha
kusambaza bidhaa hiyo ya maziwa katika maeneo mengi ya jiji katika
kuwauzia wakazi wa Arusha.
Na katika siku ya tukio, Akonaay alikuwa yuko kwenye shughuli zake za
kuwapelekea maziwa wateja wake, ndipo watengeneza barabara walipofika
eneo hilo la Mianzini na tingatinga zao na kuanza kuichimba njia hiyo ya
kutoka Mianzini hadi Ilkiding'a katika kata ya Ilboru, inayotenganisha
Jiji la Arusha na wilaya ya Arumeru.
Ikiwa imejengwa kwa fito na matope, nyumba ya 'Mmbulu' ilikuwa
miongoni mwa zile zilizobomolewa na ni baada ya wamiliki wake, kugoma
kuzibomoa wenyewe ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo.
“Shauri letu tulilipeleka mahakamani kudai fidia kabla ya mradi wa
barabara haujapita hapa,” alisema Akonaay na kuongeza kuwa mara baada ya
kesi yao kutupiliwa mbali na chombo hicho cha sheria, wajenzi
hawakusubiri hata saa moja ipite, bali walikwenda moja kwa moja eneo
hilo na kuanza kazi.
Baadhi ya wakazi wa Mianzini, wakizungumzia suala hilo kwa masharti
ya kutotajwa majina, walisema ni ajabu kwa Mzee Akonaay kuwa na kiasi
kikubwa cha fedha na kuzifukia ardhini huku mwenyewe akiishi kwenye
nyumba duni ya matope.
Lakini Akonaay ambaye kwa sasa anaitwa 'Mabulungutu,' anasema kuwa
alikosa imani na benki maana wakati akifanya kazi serikalini miaka ya
1980, alifungua akaunti na akawa anaweka fedha zake zote benki.
Baada ya kustaafu mwaka 1994 na kuamua kushughulika na ufugaji,
hakuzifuatilia tena fedha zake benki hadi mwaka 2000, ambako alipokwenda
kuangalia fedha zake aliambiwa kuwa kwa sababu akaunti yake haikuguswa
kwa zaidi ya miaka 10, alitakiwa aende Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
kujieleza. Hata hivyo, aliona huo ni usumbufu na kuamua kuanza kuweka
fedha zake nyumbani.
Lakini hii pia ilimtokea puani baada ya mmoja wa ndugu zake
kuzikwapua zote mara baada ya kuzifuma katika vitita vyenye thamani ya
Sh milioni 20 na zaidi. Sasa Akonaay akaja na mkakati mpya wa kuhifadhi
fedha kwa kuchimba shimo katikati ya chumba chake cha kulala,
kilichokuwa upande wa barabara ya Mianzini na kuanza kuweka hazina yake
humo.
Lakini tena, bahati mbaya ikiendelea kumuandama, makatapila ya
wachonga barabara, yakaifukua benki yake hiyo ya ardhini na kutawanya
fedha zaidi ya Sh milioni 35 zilizoishia kuokotwa na wapita njia pamoja
na majirani, ambao kwa hofu hawakupenda hata kulizungumzia sakata hilo.
CHANZO GAZETI LAHABARI LEO
0 comments:
Post a Comment