Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha (SSP) Emmanuel Tille akiongea na
viongozi wa kata ya Moivaro tarafa ya Suye pamoja na askari wa vikundi
vya ulinzi shirikishi wakati wa uzinduzi wa vikundi vinne vya kata hiyo
(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Ikiwa
jeshi la Polisi linaendeleza harakati za kupambana na uhalifu ili
kupunguza matukio ya namna hiyo, wananchi wa kata ya Moivaro tarafa ya
Suye halmashauri ya jiji la Arusha hawapo mbali na jitihada hizo hivyo
kuamua kujitokeza kwa moyo mmoja kupinga uhalifu kwa kuanzisha vikundi
vinne vya ulinzi shirikishi kutoka mitaa ya Ngurumausi, Oldonyommasi,
Moivaro Kati na Shangarao.
Akizindua
vikundi hivyo ambavyo vimewezeshwa na wadau walioongozwa na Jeff Mligha
ambao walijitolea vifaa mbalimbali vya ulinzi zikiwemo tochi, Mkuu wa
Polisi wilaya ya Arusha Mratibu Mwandamizi wa Polisi Emmanuel Tille kwa
niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha alisema kwamba matarajio ya
wananchi katika kata hiyo ya Moivaro ni makubwa na ana imani watakuwa
wanalala na kuamka salama hivyo kuwataka walinzi hao wawe na nidhamu
kwenye kazi yao.
“Kazi
ya ulinzi ina miiko yake; kitu cha kwanza ni nidhamu ya hali ya juu.
Mimi mwenyewe mpaka nafikia hatua hii ni kwa sababu ya nidhamu na
nawataka ninyi muige mfano wangu, ninachosema hapa ni pamoja na kuwahi
kazini, kutunza siri pasipo kuwazunguka wenzako pamoja na kufuata
maelekezo ya wakubwa wa vikundi vyenu” Alisisitiza Tille.
Alisema
japokuwa askari hao wapatao 42 wamepewa mafunzo lakini kupitia Wakaguzi
wa Polisi wa Tarafa na askari kata wataendelea kuwapa mafunzo mara kwa
mara ili waweze kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria, huku akiwaonya
wasijichukulie sheria mkononi.
Aliwataka
wananchi wanapopata taarifa watoe kwa viongozi wa Polisi mara moja ili
ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka na hatimaye kufikia malengo ya
kupunguza uhalifu ndani ya jiji la Arusha, huku akiwataka watendaji wa
kata na Wakaguzi wa tarafa wahakikishe askari wa kata wanakuwa katika
maeneo yao kila siku hali ambayo itawasaidia kubaini maeneo tete.
Akiongea
katika uzinduzi huo Diwani wa kata hiyo Rick Moiro alivitaka vikundi
hivyo kufuata taratibu za kazi na kupambana na uhalifu hasa vijana
wanaojihusisha na madawa ya kulevya aina ya bangi huku akiomba Jeshi la
Polisi litoe ushirikiano wa karibu na vikundi hivyo pindi tu wanapoomba
msaada.
Naye
Afisa Mtendaji wa kata hiyo Bi. Editha Kisangia alisema kwamba mbali na
hali ya uhalifu kuwa ya kawaida katika eneo hilo lakini hatarajii
kutokea kwa changamoto kutoka kwa baadhi ya wananchi kushindwa kuchangia
vikundi hivyo kwani faida wataiona baada ya kuanza kufanya kazi.
Wakaguzi
wa Polisi wanaoongoza tarafa tatu za halmashauri ya jiji la Arusha toka
mwaka 2013 ni pamoja na Frimina Massao tarafa ya Suye, Winibrita Moshi
tarafa Elerai na Shabani Shabani tarafa ya Themi.
0 comments:
Post a Comment