MKUU wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda amesema kuwa serikali haina
mpango wa kuwaondoa wafugaji wa jamii ya kimasai wanaoishi ndani ya
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Aidha amesema serikali itahakikisha inawalinda na kuwapatia kila
kinachostahili kama wananchi wengine, ikiwemo chakula cha msaada.
Ntibenda alisema hayo katika kijiji cha Inokanoka kilichopo wilayani
Ngorongoro na kusema kuwa propaganda zinazoenezwa kuwa serikali inataka
kuwatimua hazina ukweli wowote.
“Nimesema serikali haina mpango wa kuwahamisha wananchi wanaoishi
ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuwa wana haki ya kuishi kwenye eneo
hilo,’’ alisema na kuongeza: “Kutokana na hali hiyo, nimeagiza tani
1,000 za mahindi ziletwe hapa ili kupunguza uhaba wa chakula
unaowakabili.’’
Alisema uvumi unaoenezwa na watu wasioitakia mema nchi unapaswa
kupuuzwa, kwani serikali ya Rais John Magufuli inapenda wananchi wake na
haiwezi kamwe kuwaondoa katika eneo hilo.
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Hashim Mgandila alisema kumekuwa na
kauli zinazotolewa na baadhi ya watu wenye lengo la kugombanisha
wananchi na serikali yao juu ya eneo hilo.
Mgandila alisema kwa kauli iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa juu ya
kuendelea kukaa ndani ya hifadhi kwa wafugaji wa jamii ya kimasai
itasaidia kwa kiasi kikubwa wakazi hao sasa kufanya maendeleo badala ya
kukaa kwa wasiwasi kama watakuwepo ama la.
Akizungumzia upungufu wa chakula, Kaimu Mkuu wa kitengo cha maendeleo
ya jamii wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Kuya Sayaleki alisema
mamlaka imeshaagiza tani 12,000 za mahindi kukabiliana na upungufu wa
chakula kwa wakazi wa ndani ya hifadhi hiyo.
Sayaleki alisema kamwe Mamlaka ya Hifadhi haiwezi kuona wananchi
waliopo ndani ya hifadhi hiyo wakikabiliwa na njaa wakati wana uwezo wa
kutatua tatizo hilo.
0 comments:
Post a Comment