MKURUGENZI
wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Wakili Jumaa Mhina 'Pijei', baada
ya kula kiapo cha uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam juzi, amesema kazi
kubwa iliyo mbele yake ni kuhakikisha anatatua kero mbalimbali za
wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza katika viwanja vya Ikulu baada ya kula kiapo, Pijei, akiwa
na wakurugenzi wenzake, alisema kuwa, kwa kushirikiana na viongozi
wenzake wa wilaya hiyo akiwemo Mkuu wa wilaya, Daniel Chongolo na Ofisa
Tawala wa wilaya watatekeleza majukumu yao ipasavyo.
"Ninaamini kwa kushirikiana na viongozi wenzangu walioteuliwa hivi
karibuni, tutajitahidi kutatua kero za wananchi wetu," alisema.
Pijei alisema kuwa, uamuzi wa Rais John Magufuli kumteua kuwa mkurugenzi
wa wilaya hiyo, umempe nguvu na kujiamini kuwa, hatamwangusha Rais
Magufuli na wakazi wa wilaya hiyo.
Alisema licha ya wilaya hiyo kukabiliwa na changamoto nyingi
atahakikisha wanatumia fursa mbalimbali kutatua kero hizo wakati wowote.
Wakili huyo alisema kuwa, pia atashirikiana na wenzake kuhakikisha
wanaibua miradi mbalimbali itakayowainua kimapato vijana na akina mama
wa wilaya hiyo.
"Hii wilaya iko mpakani na Kenya, hivyo tutatumia fursa zilizopo kwa
kushirikiana na wananchi kuanzisha miradi itakayowainua kiuchumi,
naamini Longido ina wananchi waelewa na wapenda maendeleo," alisema.
Alisema mara baada ya kuripo katika kituo chake cha kazi, atapata sehemu
ya kuanzia kwani atakuwa amepata ripoti kamili ya wilaya hiyo na hata
kutembelea sehemu mbalimbali.
Wakili Jumaa Mhina 'Pijei' (wa kwanza kulia mbele), akila kiapo cha uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam. |
Wakili Jumaa Mhina 'Pijei' (wa kwanza kulia), akisaini kiapo cha uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam. |
0 comments:
Post a Comment