Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Agosti 5 mwaka huu, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba
wanatarajiwa kuanza kukutana tena mjini Dodoma kujadili rasimu ya
mabadiliko ya Katiba.
Kikao cha Bunge hilo, kinatarajiwa kufanyika kwa
takriban siku 60 na baadaye rasimu ya katiba iliyojadiliwa itapelekwa
kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura.
Mchakato wa kupatikana Katiba Mpya kwa sasa
umekumbwa na sintofahamu hasa kutokana na wajumbe kutoka kundi la Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa ) ambalo linaundwa na viongozi wa upinzani
kuamua kususia vikao na kurudi kwa wananchi.
Hata hivyo, wanasiasa na wanataaluma mbalimbali
wamekuwa wakitoa maoni nini kifanyike ili kunusuru mchakato huu na pia
wamekuwa wakitoa maoni mbali mbali .
Luteni mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ), mkuu wa wilaya wa zamani na mbunge, Lepilali ole Molloimet ni
mmoja wa wanasiasa wakongwe ambaye katika mahojiano na Mwananchi
anazungumzia mambo mengi.
Molloimet ambaye aliongoza wilaya mbalimbali nchini, ana yapi ya kusema kuhusu Katiba Mpya na hali ya kisiasa nchini?
Swali: Tanzania ipo mchakato wa kupata Katiba Mpya
na sintofahamu zimeukumba mchakato je, unadhani kuna upungufu gani
katika mchakato huu mzima.
Jibu: Mimi naamini upatikanaji wa wajumbe wa Bunge
hili haukuwa sahihi hasa kwa kuwashirikisha wabunge wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano na wenzao kutoka Baraza la Wawakilishi.
Ilipaswa Bunge hili liwe na uwakilishi tofauti,
wajumbe wateuliwe na wananchi kutoka kila wilayani ambao wangeweza
kuingia bungeni bila misimamo ya vyama vyao na lengo lao kubwa liwe ni
kusaidia kupata Katiba Mpya na siyo sasa kusababisha migongano.
Swali: Unadhani wapo wajumbe wenye upungufu na ambao hawakustahili kuwamo kwenye Bunge hilo.
Jibu: Ndiyo, wapo wabunge ambao waliiingia bungeni
kwa kuzingatia vyama vyao au urafiki na viongozi ndiyo sababu unasikia
kuna malalamiko mengi. Binafsi, nilidhani wabunge wote wasingekuwepo
kwenye Bunge la Katiba kwani ni chanzo cha mgogoro kwa kuwa baadhi
wanapigania masilahi yao badala ya taifa.
Swali: Moja ya mambo yanayokwamisha mchakato wa
Katiba Mpya ni mapendekezo ya rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya
muundo wa serikali tatu, nini maoni yako
Jibu: Mimi tangu nikipokuwa mbunge wa Monduli, msimamo wangu ni serikali tatu, tena kwa mazingira ya sasa haikwepeki tena.
Wenzetu Zanzibar wamefanya mabadiliko makubwa
kwenye katiba yao, ambayo kimsingi yanalazimisha serikali tatu na
viongozi walikuwa kimya wakati wote sasa hakuna jinsi ni kukubaliana na
maoni ya walio wengi.
Swali: Lakini, waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere na Abeid Karume walipounganisha nchi walikuwa na malengo mema
ikiwamo kuimarisha ulinzi na uchumi ni nini mtazamo wako?
Jibu: Ni kweli wakati ule kulikuwa na tishio la
uvamizi, hasa kwa Zanzibar kupitia baharini, lakini sasa hakuna mambo
kama hayo tena dunia imepiga hatua kubwa za kiulinzi na usalama.
Pia, ni kweli kiuchumi Muungano una mafanikio
lakini, ikumbukwe muungano ni wa watu siyo serikali hivyo, hata serikali
tatu zikiundwa tusitegemea watu kutengana ni kuboresha tu upatikanaji
wa huduma kwa wananchi.
Swali: Chama cha Mapinduzi (CCM) tayari kimetoa msimamo wa kutetea serikali mbili unadhani kuna athari yoyote inaweza kutokea?
Jibu: Mimi pia ni mwanaCCM, nasema msimamo huu una
madhara kwani wananchi wengi wanapinga na tukibaki na msimamo huu,
tujiandae kuwa chama kikuu cha upinzani hivi karibuni.
Tunapaswa kuwasikiliza wananchi na hili ni tatizo,
viongozi wetu wamekuwa hawashauriki, wanawasikiliza marafiki zao tu na
ndiyo hawa wanateuliwa kuwa viongozi sasa.
Leo hii hata Bunge lina baadhi ya watu wa ajabu,
wamepatikana bila kujali sifa, tunashinikizwa kuwa na wabunge wengi viti
maalumu hili jambo lina athari kwani hatupati wabunge bora wanawake,
binafsi nadhani tungewaacha wagombee majimbo kwani wapo wenye uwepo
mkubwa wakigombea huko na watashinda.
Swali: Wewe ulikuwa mbunge kutoka Jimbo la
Monduli, wakati huo kulikuwa na changamoto nyingi katika suala la wa
wafugaji unadhani matatizo yamepungua?
Jibu: Ni kweli wakati ule kulikuwa na changamoto
na baadhi zimepatiwa ufumbuzi lakini hili la wafugaji nadhani matatizo
yao yameongezeka zaidi.
Hivi sasa wamekuwa kama wakimbizi kwenye nchi yao,
wanafukuzwa kila mahali hata walipotoka ardhi yao imetolewa kwa
wawekezaji, sasa Taifa letu wawekezaji ji bora kuliko wananchi wao ndiyo
wanafaidi rasilimali za nchi hii.
Swali:Unadhani nini kifanyike kupunguza matatizo haya ya ardhi?
Jibu: Serikali lazima ipime ardhi yote, itenge
maeneo ya kilimo, ufugaji, huduma za jamii na maeneo ya uwekezaji kwani
kufanya hivyo kutasaidia kupinguza haya mapigano kila kona ya nchi
kugombea ardhi.
Swali: Tangu ulipostaafu nafasi ya ukuu wa wilaya
umekuwa kijijini kwako Longido, ina maana umestaafu siasa na je, hauna
nia kugombea ubunge tena?
Jibu: Hapana, mimi ni mwanasiasa na nitaendelea
kuwa mwanasiasa na wananchi wakiniomba kugombea nitakuwa tayari kwani
wananijua mimi wakati wote nimekuwa mtetezi wao.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment