JESHI
la Polisi mkoani Arusha, linawashikilia watu 25 wanaodaiwa kujihusisha
na matukio ya ulipuaji mabomu katika maeneo mbalimbali akiwemo mume na
mke ambao walikutwa na mabomu saba pamoja na vifaa vyake kutoka nchi za
Ujerumani na Urusi.
Mbali ya wanandoa hao
kukutwa na mabomu hayo, pia Imamu wa Msikiti wa Quba, naye anashikiliwa
na jeshi hilo kwa makosa ya kujihusisha na mtandao wa ulipuaji wa mabomu
jijini Arusha.
Kukamatwa kwa watu hao
na mabomu yaliyokuwa tayari kulipuliwa, kumetokana na msako unaoendelea
kufanywa na jeshi hilo baada ya kupewa taarifa kutoka kwa raia wema.
Akizungumza na
waandishi wahabari jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
(DCI), Isaya Mngulu, alisema watu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti
ila mabomu hayo yamepatikana eneo la Sombetini.
Alisema kupatikana kwa
mabomu hayo, kunatokana na taarifa kutoka kwa raia wema ambapo Julai 21
mwaka huu, saa mbili usiku, polisi walivamia nyumbani kwa Bw. Yusuph Ali
na mkewe Bi.Sumaia Juma ambao walikutwa na mabomu yaliyotengenezwa
Ujerumani na Urusi.
"Polisi walifanya
upekuzi wa kina na kuyakuta mabomu haya yakiwa tayari kwenda kulipuliwa
pamoja na vifaa vingine ambavyo vinasadikika kutumika katika ulipuaji
mabomu haya," alisema Mngulu.
Aliongeza kuwa,
watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani muda wowote ili kujibu mashtaka
yanayowakabili akiwataja baadhi yao kuwa ni Imamu wa Msikiti huo, Jafari
Lema, Shabani Musa, Athumani Hussein, Mohamed Nuru na Abdul Mohamed.
"Bado tunaendelea
kumtafuta kinara wa mabomu haya ambaye pia anasadikiwa kuwa ndiye
kiongozi wa ulipuaji bomu anayefahamika kwa jina la Yahaya Hassani, kwa
sasa ametokomea kusikojulikana.
"Jeshi la Polisi
litatoa zawadi nono kwa yeyote ambaye atasaidia kukamatwa kwa Yahaya ili
amani ya Mkoa wa Arusha iweze kurudikama ilivyokuwa siku za nyuma,"
alisema.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment