Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAZIRI
Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amesema kuwa elimu hapa nchini iko
hoi, kwamba unahitajika ushirikiano wa pamoja baina ya wadau pamoja na
kutumia mapato ya gesi kuinusuru.
Lowassa ameishauri serikali kuangalia uwezekano wa kutumia mbinu
zilizotumiwa na nchi ya Marekani kuboresha elimu yao kwa kuwachukua
wataalam waliobobea kwenye sekta hiyo na kuwafungia mahali kwa miezi
sita kisha wakatoke na majibu ya kumaliza tatizo hilo.
Alitoa rai hiyo jana wakati akifungua mkutano wa 25 wa Dayosisi ya
Kaskazini Kati ambapo pamoja na mambo mengine, utamchagua askofu wa
dayosisi hiyo kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Askofu Thomas Laizer
aliyefariki mwaka jana.
Lowassa alisema kuwa elimu imeendelea kuwa hoi licha ya kuundiwa tume
mbalimbali ambazo hazileti taarifa hadharani jambo alilodai
linasababisha kushindwa kuelewa anayekosea ni nani kati ya tume na
serikali ambayo haitekelezi mapendekezo ya tume hizo.
“Angalieni wanazungumza habari ya kufaulu kwa kupata daraja A ambalo
halifanani na mahali popote duniani, haiwezekani lazima kuna tatizo
mahali, lazima tukubali ni wajibu wetu,” alisema.
Alisema kuwa kuna ulazima wa kugawana majukumu na kila mmoja kutimiza
wajibu wake ikiwemo serikali, wazazi, wanafunzi na kanisa ambapo kila
mmoja abebe mzigo wake kuhakikisha elimu inaboreka.
“Mwenyezi Mungu ametubariki tumepata gesi, wanasema msipoangalia gesi
inaweza kugeuka kuwa laana, mimi nafikiri mahali pa kuelekeza fedha za
gesi ni kwenye elimu bora.
“Elimu itakayojibu mahitaji ya sasa badala ya kuendelea kuwasumbua
wazazi huko vijijini wenye hali mbaya, tunaweza kutumia fedha za
serikali na kanisa kuwaokoa hawa wazazi wasio na uwezo,” alisema.
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli, aliongeza elimu
itakayotolewa ilenge kutoa ajira kwa wahitimu kwani kwa sasa kuna tatizo
kubwa la ajira nchini.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment