Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi
Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani hapa limeendelea kupambana na wahalifu
wa madawa ya kulevya ambapo juzi limefanikiwa kukamata magunia 20 ya madawa
hayo aina ya bangi.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema kwamba,
madawa hayo yalikamatwa tarehe 23.07.2014 muda wa saa 2:30 usiku wilayani
Longido katika kijiji kiitwacho Olteres.
Kamanda Sabas alisema kwamba, mafanikio hayo yalipatikana
baada ya Jeshi hilo kupata taarifa toka kwa raia wema zikieleza kwamba kuna
watu wanayasafirisha kwa kutumia wanyama aina ya Punda.
Mara baada ya taarifa hiyo ndipo askari wa Jeshi la Polisi
kwa kushirikiana na askari wa kampuni ya Jumuiya ya Jamii inayojishughulisha na
Ulinzi wa wanyamapori na mazingira kambi ya Enduimet walianza kuwafuatilia
kuanzia saa 8:00 Mchana na kufanikiwa kuona nyayo za punda pamoja na binadamu
ambazo zilikuwa zinaonyesha zimetokea Oldonyasambu kuelekea Namanga.
Kamanda Sabas aliongeza kwa kusema kwamba uchunguzi wa Jeshi
la Polisi ulibaini kwamba magunia hayo yanayokadiriwa kuwa na kilogramu 80 kila
mojawapo yalikuwa yanapelekwa nchi jirani ya Kenya yalipatikana baada ya msako
uliofanywa na askari hao kwa takriba saa 4 na dakika 30 ambapo yalikuwa
yametelekezwa kijijini hapo huku wahusika wakitoweka kusikojulikana.
Hata hivyo Jeshi hilo Mkoani hapa linaendelea na upelelezi
juu ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaka watuhumiwa wa tukio hilo huku
doria ikiendelea ili kuweza kudhibiti wahalifu wote wanaodhubutu kupita njia za
panya baada ya kuona wanabanwa katika barabara kuu.
Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea kutoa shukrani kwa
wananchi wanaotoa taarifa za mara kwa mara juu ya uhalifu na wahalifu na kuomba
waendelee kujitokeza ili taarifa hizo zifanyiwe kazi na hatimaye kufanikisha
kupunguza uhalifu wa maeneo mbalimbali ya Mkoa huu.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment