Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WABUNGE
wanawake wa mabunge ya Jumuiya ya Madola, (CWP), wameitaka jumuiya ya
kimataifa kuingilia kati na kushirikiana na Serikali ya Nigeria,
kuhakikisha watoto wa kike 200 wanaoshikiliwa na kundi la kigaidi la
Boko Haram wanaachiwa.
CWP ukanda wa Afrika wamepanga kwenda Nigeria kwa ajili ya kuzungumza
na wanawake na Rais Goodluck Jonathan, kujua kwanini hadi sasa watoto
hao hawajaachiwa.
Kauli hiyo ilitolewa kwa nyakati tofauti jana jijini hapa na
Mwenyekiti wa CWP, Rebeca Kidaga na Makamu Mwenyekiti wa CWP, Ukanda wa
Afrika, Beatrice Shelukindo, walipokuwa wakitoa msimamo wa vyombo hivyo
katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA),
Kanda ya Afrika.
Kidaga ambaye pia ni Spika wa Bunge la Uganda, alisema wameumizwa na
tukio hilo huku wakitaka Serikali ya Nigeria na jumuiya za kimataifa
kuhakikisha matukio ya kigaidi ya Boko Haram yanakomeshwa.
Naye Shelukindo, alisema watakwenda Nigeria kabla ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika Aprili mwakani.
Awali akiwasilisha mada kwenye mkutano huo juu ya changamoto na
mafanikio ya utekelezaji wa malengo ya milenia, kwenye elimu ya msingi
kwa watoto wa kike, Shelukindo, alisema Tanzania imefanikiwa kwani
kwenye baadhi ya maeneo idadi ya watoto wa kike wanaojiunga na shule
imekuwa sawa huku baadhi ya maeneo ikiwa kubwa zaidi.
Hata hivyo, alisema kuwa suala la uhamasishaji wanawake kujiunga na
masomo ya sayansi bado linakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na
hulka na mazoea mabaya yaliyojengeka kwenye jamii kuwa wanawake hawawezi
uhandisi sanjari na wao wenyewe kutojiamini.
“Kwa mfano ni vigumu kwa mwanamke aliyeolewa na aliyeajiriwa na
kampuni ya simu kutoka nyumbani kwake usiku kwenda kushughulikia tatizo
lililojitokeza kwenye mitambo, mwaka 2009 kuna utafiti ulionyesha kwamba
wanawake wanasayansi wanakwazwa na waume zao kutokana na utaratibu
uliopo kuwa wanawake husikiliza uamuzi wa waume zao na kuwaheshimu,
hivyo wamekuwa kikwazo,” alisema Shelukindo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment