Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katika jamii nyingi, hasa za mijini, ni kawaida wanawake na wanaume kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Lakini hali hii ni tofauti kwa Wanawake wa jamii
za pembezoni za wafugaji; Wamasai, Wabaebeig na Wahadzabe ambao wanaume
wao badala ya kuwaunga mkono katika miradi yao, wamekuwa wakiwahujumu.
Baadhi ya wanaume hawa wamefikia hatua ya kupora mifugo, ya vikundi vya akina mama hawa, ili wasiendelee kiuchumi.
Wanawake wa jamii hizo, wakizungumza na Mwananchi
katika mkutano uliokuwa umeandaliwa na mtandao wa mashirika ya wafugaji
na waokota matunda (PINGOS Forums), wanasema miradi yao imekufa baada ya
kuhujumiwa na waume zao.
Amina Msendekwa, mfugaji kutoka jamii ya Wamasai
wa Kijiji cha Wami Sokoine wilayani Mvomelo, anasema mradi wao wa
kunenepesha mifugo katika kijiji chao umekwama baada ya wanaume wao
kuiba mifugo kabla ya mauzo ili wasiendelee na biashara hiyo.
Anasema walianzisha mradi huo baada ya kupata
hamasa na elimu ya kutosha, hivyo wakawa wananunua ndama wadogo na
kuwafuga kwa kuwanenepesha na baadaye kujipanga kuuza ng’ombe wakubwa.
“Mradi wetu ulikuwa mzuri sana. Tulinenepesha
mifugo, lakini tulipopanga kuuza baada ya kukamilika, tulianza kuibiwa
kidogo kidogo,” anasema.
Kutokana na majukumu yao kama wanawake,
iliwalazimu kuomba msaada kwa wanaume kuwasaidia kuwasaka ng’ombe
waliokuwa wanaibiwa, lakini cha ajabu walikuwa hawapewi ushirikiano na
baadaye walibaini ni njama za waume zao.
“kila tulipokuwa tukipanga kupeleka ng’ombe
mnadani, waliibiwa na wanaume zetu na jitihada za kurejeshewa zilikwama
hadi sasa mradi umekufa,” anasema Msendekwa.
Paulina Tipapu, mkazi wa Loliondo, anasema licha
ya mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali wilaya ya Ngorongoro wa
Nngonet kuwapa mbuzi watano wa kisasa, mradi huo umekwamishwa na
wanaume.
Tipapu anasema wanaume wamekuwa wakichukuwa mbuzi
bila idhini yao na kwenda kuwauza na hata pale wanapokwenda wao kuuza
wanaume wamekuwa waking’ang’ania fedha.
“Tumeshindwa kuendeleza mradi kama tulivyotarajia
baada ya waume zetu kutuhujumu. Sasa tunakaa kubuni miradi mingine,”
anasema Tipapu.
Caroline Kandus, afisa jinsia wa miradi mtambuka wa Pingos
Forums, anasema kutokana na baadhi ya wanaume katika jamii hizo kuhujumu
miradi ya wanawake, wameanza kutoa elimu ya miradi mbadala ili
kuwakomboa.
“Ni kweli akina mama wa jamii hizo wanakabiliwa na
changamoto nyingi katika miradi ndio ndio maana hapa tupo mashirika
kadhaa kuwapa elimu mbadala katika miradi mingine kama ya Saccos,
ufugaji wa nyuki na shanga ambayo wanaume hawatahusika,” anasema.
Anasema katika mipango mipya wanakusudia kujikita
kuwasaidia akina mama hao ili wawe na miradi ambayo haitahitaji msaada
mkubwa wa wanaume kama miradi ya kusuka shanga na kufuga nyuki.
“Tumeanza kutoa elimu na baadaye tutaandaa
maandiko na kupeleka sehemu mbalimbali ili akina mama hawa wapate elimu
na mitaji,” anasema
Hata hivyo, alisema kwa kiasi kikubwa wanawake wa
jamii hizo wameanza kuelewa umuhimu wa kuwa na miradi yao na sasa
mikakati imeanza kutoa elimu kwa wanaume, ili kutokwamisha miradi ya
akina mama.
Ndeko Ndeko, ambaye anatoka jamii ya Wahadzabe,
anasema jamii zao zinaweza kubadilika kama wakipatiwa miradi ambayo wana
uwezo nayo.
“Ng’ombe hatuwezi kwa kuwa tutawala tu. Hatuwezi
kukaa na njaa wakati tuna wanyama, lakini tukisaidiwa miradi ya nyuki
katika bonde letu la Yaeda Chini nadhani tunaweza kubadilika,” anasema
Ndeko.
Afisa tawala wa Wilaya ya Simanjiro, Juma Ali Juma
anasema Serikali inatambua changomoto hizo na sasa mkakati umeanza
kuwekwa katika miradi shirikishi baina ya akina mama, waume zao na
mashirika yasiyo ya kiserikali.
“Kutokana na tafiti inaonekana akina mama hawa,
wanaweza kufanya miradi mbali mbali ya kimaendeleo lakini lazima tuwe na
mbinu za kuwashirikisha waume zao kutambua miradi hiyo na kuwapa elimu
ya kuwazuia wasiwaingilie,”anasema Alli.
Hata hivyo, anasema anaimani kukiwa na miradi
shirikishi maisha ya akina mama hao wa jamii za pembezoni, wataweza
kubadili mifumo ya maisha yao.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment