Stori: Joseph Ngilisho, ARUMERU/GPL
HOFU ya
ushirikina imetikisa Mkoa wa Arusha kufuatia tukio la hivi karibuni
ambapo mwanafunzi wa Chuo cha Kompyuta jiji hapa, Witness Obed (21)
aliyefariki dunia Aprili 12, mwaka huu na kuzikwa kwenye makaburi ya
nyumbani kwao Kijiji cha Nanja, Kata ya Moshono wilayani Arumeru, Arusha
kuibuka akiwa hai.
Witness
Obed (21) aliyefariki dunia Aprili 12 mwaka huu na kuzikwa kwenye
makaburi ya nyumbani kwao Kijiji cha Nanja, mkoani Arusha na kuibuka
akiwa hai tena.
Binti huyo aliibuka kwao hivi karibuni akiwa mpole na kuwafanya baadhi ya watu, wakiwemo wazazi wake kutimua mbio kwa hofu.
Watu kutoka maeneo mbalimbali
jijini hapa wamekuwa wakimiminika nyumbani kwa wazazi wa binti huyo
kwa lengo la kumshuhudia kwa vile ndugu walishaamini kuwa, mpendwa wao
huyo alishakufa na alizikwa.
UWAZI LATIA TIMU NYUMBANI
Baada ya kusikia taarifa hizo, Uwazi
lilifunga safari mpaka eneo la tukio na kumshuhudia binti huyo kisha
likaenda kwenye kaburi alilozikwa.
Kwenye kaburi hilo, msalaba wenye kuonesha siku yake ya kuzaliwa (1992)
na kufa (12, Aprili, 2014) ulikuwa bado umesimama imara huku kaburi
lenyewe likionesha dalili ya kutitia kidogo.
BABA MZAZI ASIMULIA
Akisimulia mkasa huo kwa mshangao mkubwa, baba mzazi wa binti huyo, Obed Leiyo alisema:
“Ilikuwa Aprili mwanzoni, binti yangu alitoweka nyumbani baada ya kurudi kutoka chuoni majira ya saa 2 usiku akiwa amechelewa.
Mimi kama mzazi nilimfokea kwa kuchelewa kwake kurudi nyumbani.
“Yeye kwa hasira zake alizunguka nyumba akaondoka muda huohuo na hakurudi kabisa hapa nyumbani.
“Siku iliyofuata tulianza kumtafuta maeneo mbalimbali bila mafanikio,
tukatoa matangazo kwenye vyombo vya habari lakini binti yangu
hakuonekana.”
TAARIFA ZAFIKA, KAFA
Mzazi huyo aliendelea kusema: “Siku moja
tulipata taarifa kwamba kuna mwili wa msichana umeonekana katika Kijiji
cha Bwawani hapahapa Arumeru.
“Mimi pamoja na ndugu wengine tuliamua
kwenda katika kile kijiji. Tulipofika tuliambiwa ni kweli mwili wa
msichana uliokotwa lakini wananchi wakauzika.”
WAFUKUA KABURI
Baba huyo anaendelea: “Niliamua kwenda
Kituo cha Polisi cha Usa River ambako niliomba kibali kwa ajili ya
kufukua kaburi na kuutoa mwili ili kuutambua kama ni binti yangu au la!
“Nilipewa kibali, tukafukua kaburi na kutoa mwili. Nilimtambua kuwa ni
binti yangu kutokana na alama mbalimbali alizokuwa nazo, ikiwemo rangi
kwenye kucha na sehemu ya kushoto ya uso ilikuwa nyeusi kwa sababu
aliwahi kupooza.
MWILI WASAFIRISHWA, WAZIKWA
Baba huyo wa Witness alizidi kueleza kuwa
waliusafirisha mwili huo hadi nyumbani kwake Moshono na kuandaa taratibu
za mazishi ambapo Aprili 23, mwaka huu mwili ulizikwa.
AIBUKA GHAFLA
Hata hivyo, Obed anasema alishangaa siku
ya tukio kumwona binti yake huyo akiibuka nyumbani hapo akiwa hai jambo
ambalo lilimshangaza na kumfanya akimbie kwanza na baadaye kufanya
mawasiliano naye.
BINTI ASIMULIA
Akizungumza na Uwazi, binti huyo alikiri kutoweka nyumbani kwao Aprili 15, mwaka huu na kwenda kusikojulikana.
Alisema hakujua kilichoendelea baada ya kuondoka nyumbani lakini baadaye
alibaini kuwa alikuwa katika Kijiji cha Olkokola wilayani Arumeru na
alikwenda kwenye nyumba ya mwanamke mmoja asiyefahamiana naye akamuomba
maji ya kunywa.
“Nilifika kwenye nyumba moja nikamkuta mama mmoja, nikamwomba maji ya
kunywa akaenda kuniletea. Nilikunywa huku amenisimamia, lakini maji
yalikuwa machungu sana, nikamrudishia, akanilazimisha ninywe kwa
kunisukumia kikombe kinywani. Nilipomaliza nilipoteza fahamu.
“Baadaye nilizinduka, nikaendelea kuishi palepale nyumbani kwa yule mama lakini sifahamu nilikuwa nafanya nini.
“Juzi ndiyo nikashangaa
kujikuta nimerudi nyumbani, mimi sijui nini kilikuwa kikiendelea,” alisema binti huyo.
MAJIRANI NAO
Majirani kadhaa waliokuwepo nyumbani kwa
Obed walilielezea tukio hilo kwamba ni la ushirikina huku wakisema ni
jambo la kuogofya ambalo halikuwahi kutokea kijijini hapo kabla.
Wengine walisema kuwa binti huyo alifufuka na wengine walisema alichukuliwa msukule.
“Hili si suala la kawaida lazima kuna
ushirikina kwani huyu binti tulishamzika na wazazi wake walimtambua
kabisa kuwa ni yeye baada ya
kuambiwa alikutwa amekufa, sasa hebu fikiria tangu tumezika mbona hakuna
mtu aliyekuja na kusema na yeye alipotelewa na binti yake halafu cha
ajabu hilo kaburi mbona limebonyea? Atakuwa amefufuka,’ alisema mkazi
mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Amina Liwa.
Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Usa River, Benedict Mpujila amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unafanyika.
KUMBUKUMBU
Mapema mwaka jana tukio la kishirikina
liliibuka katika wilayani Arumeru eneo la Kwa Mrefu ambapo mtu mmoja
alidaiwa kudondoka na ungo, muda mfupi baadaye alitoweka na kwenye ungo
kubaki mayai na kuku mweupe.
0 comments:
Post a Comment