Home » » TAMU NA CHUNGU YA DHAHABU LOLIONDO

TAMU NA CHUNGU YA DHAHABU LOLIONDO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Abeid Samule(Kushoto)na Boniface Samuel wakichuja udongo kwenye Kitanda ili kupata dhahabu.Picha na John Ngunge.
 
Baada ya kupatikana kwa dhahabu eneo la kijiji cha Mgongo, wilayani Ngorongoro, wazee wa kabila la Wasonjo wa kijiji hicho, wamekuja juu na kuwaonya wachimbaji wadogo wadogo kuacha tabia ya wizi na kutafuta urafiki wa mapenzi na wanawake.
Wasonjo ni kabila la wabantu linalofanya kazi ya kilimo na ufugaji kwa wakati mmoja na ni maarufu kama wapiganaji wakitumia silaha za jadi kama mishale yenye sumu na mapanga.

“Tulipofika hapa wiki mbili zilizopita, wazee wa Kisonjo, waliitisha mkutano hapa mgodini, wakatutaka kutafuta dhahabu kila eneo, lakini tuache vitu viwili, wizi na kutafuta wanawake.

“Walitueleza hapa kijijini hakuna mwanamke wa kufanya naye mapenzi, wote wameolewa kuanzia mwenye umri wa miaka mitatu,” alisema mchimbaji mmoja kwa lafudhi ya lugha ya Kisukuma.

Mlinzi wa amani eneo hilo, Malecela Msimedi Saideya, anasema hakuna vurugu yo yote iliyotokea tangu watu waje kwa wingi kuchimba dhahabu.“Tuna ulinzi wetu wa jadi na pia tunasaidiana na polisi, wapo hapa, hapa ni amani tu,” alisema.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Moses Ragadya, anathibitisha kuwa ni kawaida kwa jadi yao watu wasijihusishe na tabia hizo.

“Hiyo ni kawaida, ni jadi ya huku kwetu,” alisema.

Alisema kumekuwapo na vijana wengi katika machimbo ya dhahabu kijijini hapo, ingawa alisema hakuna anayelazimika kutoa taarifa ofisini kabla ya kwenda mgodini.

Alisema upo utaratibu uliowekwa na walinzi wa amani huko migodini wa kuwapimia maeneo ya uchimbaji.

Chiku Daniel (17) mkazi wa Samunge na Hamida Juma (22) mkazi wa Sale ambao wapo mgodini hapo wakifanya biashara ya kupika chakula wanathibitisha kuwa hakuna usumbufu wanaoupata toka kwa vijana wa kiume.

“Hakuna ubakaji wala usumbufu wa aina yo yote wa kingono,” Hamida anasema na kuongeza, “biashara ya chakula na vinywaji ni nzuri.

“Tumeanza biashara hii wiki mbili zilizopita, hatujapata usumbufu wo wote, hakuna wahuni hapa, watu ni wengi wanakuja na kuondoka, kwa siku tunaweza kupata hadi Sh. 30,000,” anasema Hamida.
 
VIJANA WAMIMINIKA
Mamia ya makundi ya vijana kutoka mikoa ya jirani ya Manyara, Singida, Kilimanjaro, Tabora na Shinyanga wamevamia korongo lililopo kijiji cha Mgongo linaloendelea hadi kijiji cha Samuge wakichimba dhahabu, kununua na wengine kufanya biashara ya vyakula na vinywaji.

Kijiji cha Mgongo kipo umbali wa kilomita 10 hivi kutoka Kijiji cha Samunge na usafiri wa kwenda huko ni wa pikipiki ambao mmoja analazimika kutoa Sh. 15,000 kwa safari moja ama ya kwenda au kurudi.

Wapo baadhi ambao kwa kubana matumizi hutembea kwa miguu wakipandisha milima ya Loliondo kutokea Samunge, baada ya kushushwa na basi wakitokea Arusha.

Wamiliki wa mabasi siku wamewarahisishia abiria usafiri wa kwenda kijiji cha Mgongo baada ya kuamua kupita njia iendayo kijijini Samunge tofauti na awali ambapo mabasi na magari mengine yanayobeba abiria yakienda Loliondo hayakuwa yakipita Samunge.

“Siku hizi magari ya abiria ya kwenda Loliondo yanapita hapa Samunge kwa sababu kuna abiria wengine wanaokwenda migodini,” anasema mwendesha pikipiki Eric Ngenedi, mkazi wa kijiji jirani na Samunge cha Digodigo.

Ngenedi ambaye hufanya shughuli zake katika kijiji cha Samunge anasema amekuwa akipeleka abiria migodini hadi mara nne kwa siku.

BAADHI WANYOOSHA MIKONO
Wakati wengi wakielekea huko, baadhi walikuwa wakirudi makwao baada ya kukata tamaa ya upatikanaji wa dhahabu ya kutosha.

Kijana Geofrey Mushi, kutoka Moshi, alisema analazimika kurudi nyumbani na kuendelea na shughuli zingine baada ya utafiti wake kubaini kwamba hakuna dhahabu ya kutosha inayopatikana hapo.

“Korongo hilo limevamiwa lote kwa shughuli za uchibaji wa dhahabu, lakini yapo maeneo mengine haturuhusiwi kwenda kuchimba, si unawajua Wasonjo walivyo? Kule juu ya korongo walikotuzia kuna uwezekano wa kuwa na dhahabu ya kutosha.

“Nilikuja huku kama siku tatu zilizopita, nimefanya utafiti, lakini nimeona kazi hii hailipi, narudi,” alisema.

Mwingine Khalid Musa, mkazi wa maeneo ya Oysterbay jijini Arusha, ambaye alisema ni mzoefu wa shughuli za uchimbaji, alilazimika kurudi siku ya pili yake baada ya kuona uchimbaji huo hauna faida.

“Nilikuja Ijumaa toka Arusha baada ya kusikia kwenye gazeti moja kwamba huku kuna dhahabu ya kuzoa, nilikuwa pamoja na wenzangu watatu ambao tulikutana na kufahamiana kwenye gari baada ya kufika Samunge tuliamua kutembea kwa miguu mpaka huku migodini, lakini hali ni ya kukatisha tamaa, nageuza leo leo.

“Nimefanya utafiti sana nikagundua kwamba hakuna dhahabu ya kutosha, hakuna mwamba, ungepatikana huo, dhahabu ingekuwa ya kuzoa,” alisema.Wengine walioamua kurudi ni wachimbaji wawili  kutoka Tabora, lakini wakifanya shughuli za uchimbaji mdogo huko Mbulu.

Walisema pamoja na masharti waliyopewa na wazee wa Kisonjo, waliweza kufanya uchimbaji kijijini hapo na kuwafundisha vijana wenyeji kwa wiki tatu hivi.

“Hatujapata dhahabu nyingi, kiasi kikubwa cha dhahabu tulichopata ni kama gramu saba tu, siku zingine ni gramu moja, mbili au tatu, (gramu moja wanauza Sh 60,000) fedha tunagawana na sisi tupo watatu.“Kwa kifupi hakusomeki, tunarudi kuendelea na kazi zetu huko Mbulu,” alisema.
 
WENGINE WAKOMAA
Boniface Samuel (22) na kaka yake Abeid Samuel (24) wote wakazi wa Oldonyo Sambu, wanasema wamefundishwa na wageni waliofika kutoka mikoa mbalimbali namna ya kuchimba na kuchuja udongo ili wapate dhahabu.

Hata hivyo, walikataa kusema wamekwishapata dhahabu kiasi gani, ila tu walidai wamepata kidogo.
“Tutaendelea mpaka kieleweke, tunatafuta fedha hapa” alisema Boniface.

KIJIJI CHAFAIDI
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mgongo, Ragadya, alisema kijiji chake kinakusanya ushuru kwa kila wiki kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara ya vyakula na vinywaji.

Hata hivyo, alisema kwa wastani wanaweza kupata Sh. 150,000 kwa kuwa wapo baadhi ambao wanakataa kutoa kwa wakati huo kwa madai kuwa hawajapata kitu.

Alisema ushuru kwa kila mgodi ni Sh. 5,000 wakati kwa akina mama lishe wanatozwa sh. 2,000. 

MAISHA MGODINI

Pamoja na umati mkubwa wa watu, wengi wanaonekana kuwa makini katika kazi zao, lakini pia hupata muda wa kupumzika na burudani.

Dickson Maruseki (21) anasema nyakati za jioni anawatumbuiza watu kwa miziki mbalimbali akiwa kama rapa.

Anasema kuwa rapa ni kazi ambayo anaipenda licha ya kwamba amemaliza kidato cha nne mwaka jana Shule ya Sekondari Loliondo na anatarajia kuendelea  na masomo.

Burudani nyingine iliyopo hapo ni mchezo wa pool ambao hupendwa sana hususan na makundi ya vijana.
Lakini hata hivyo, maisha mgodini hapo hayaonekani rahisi, kama anavyosema Khalid Musa, ambaye alikuja hapo siku moja tu na kurejea kwao Arusha.

“Chakula ni shida, lakini kipo, ni hela yako tu. Maji yanauzwa bei mbaya, unaweza kutumia fedha nyingi kula na kununua maji kwa ajili ya kuchuja dongo na usifanikiwe kupata dhahabu,” anasema huku akiwashawishi wenzake warudi.

Akina mama lishe wanasema wananunua maji dumu moja kwa Sh. 1,000 na hata huko wanakochota maji nayo hupatikana kwa shida.
Eneo hilo ni moja ya maeneo kama na ukiwa njiani mahindi yaliyopo mashambani yanaonekana wazi wakinyauka kutokana na kukosa mvua.

VIFAA DUNI

Ukiwa na vifaa hivi unaweza kuanza kazi ya uchumbaji mdogo huko Mgongo.

Karai, gunia la mkonge, taulo, ndoo, beleshi, sururu na ndoo kubwa ya kuwekea maji.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa