BAADHI
ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Usharika
wa Endamarariek, Jimbo la Karatu, mkoani Arusha, mwishoni mwa wiki
walimkataa Mchungaji mpya wa usharika huo, John Moyo.
Hali hiyo
ilijitokeza baada ya mchungaji wa zamani, Costatini Panga kufukuzwa na
Dayosisi ya Kaskazini ambapo uongozi wa jimbo hilo ukiongozwa na Mkuu wa
Jimbo, mchungaji Samwel Slaa, ulifika katika usharika huo ili
kumtambulisha Mchungaji Moyo.
Hata hivyo, waumini waliokuwepo
kanisani zaidi ya 400 walisusia ibada ya utambulisho na kutoka nje
wakipinga kupelekewa mchungaji mpya bila ridhaa yao.
Baada ya
waumini hao kutoka nje, uongozi huo uliendelea na ibada kwa saa mbili
ambayo ilihudhuriwa na waumini wasiozidi 10 na baada ya ibada hiyo
kumalizika, waumini waliotoka waliingia kanisani ili kuendelea na maombi
na kufanya majadiliano.
Akizungumzia mgogoro huo, muumini mmoja wa
kanisa hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, aliulalamikia
uongozi wa Jimbo kufanya ibada kwa nguvu waumini wengine wakiwa nje.
Alisema
uongozi huo kwa kushirikiana na Dayosisi ya Kaskazini,umekuwa
ukiwadharau waumini badala ya kuwasikiliza katika malalamiko yao ya muda
mrefu.
"Sisi kama washirika wa Endamarariek , tumefikia uamuzi wa
kumkataa Mchungaji Moyo kwa sababu tayari tumeanza mchakato wa kufungua
kesi mahakamani tukipinga uamuzi wa Jimbo na Dayosisi kufukuzwa
Mchungaji Panga bila sababu za msingi," alisema.
Mkuu wa Jimbo hilo
Mchungaji Slaa alipoulizwa kuhusu mgogoro huo, alisema wapo baadhi ya
waumini ambao ndio wanaosababisha mgogoro huo hivyo wapo katika vikao
vya ndani ili kuwajibu.
0 comments:
Post a Comment