Home » » MUAMKO JUU YA ULINZI SHIRIKISHI WASHIKA KASI ARUSHA TAARIFA ZAIDI ZA UHALIFU ZATOLEWA

MUAMKO JUU YA ULINZI SHIRIKISHI WASHIKA KASI ARUSHA TAARIFA ZAIDI ZA UHALIFU ZATOLEWA

 BOFYA HAPA KUTAZAMA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE


Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wananchi Mkoani hapa wameonekana kuwa na muamko zaidi wa Ulinzi Shirikishi baada ya kutoa taarifa mbili zilizofanikisha kukamata misokoto 1,038 ya madawa ya kulevya aina ya bangi pamoja na mirungi kilogramu 75.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisi kwake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Gilles Muroto alisema kwamba katika matukio mawili yaliyofanikisha ukamataji wa madawa hayo taarifa zake zilitolewa na raia wema.
Kaimu Kamanda Muroto alisema kwamba, tukio la kwanza lilitokea tarehe 18.02.2014 muda wa saa 1:30 asubuhi maeneo ya Kituo Kikuu cha mabasi jijini hapa ambapo mtu mmoja aitwaye Charles Ogaga Ayunga (38) raia wa Kenya na ni mkazi wa Taveta nchini humo, alikamatwa na misokoto 1,038 ya Madawa ya kulevya aina ya bangi iliyokuwa ndani ya boksi.
Akifafanua taarifa hiyo Kaimu Kamanda huyo alisema kwamba, siku ya tukio mtuhumiwa alikuwa anatokea maeneo ya Ngaramtoni akiwa kwenye Hiace na alipofika maeneo ya Kituo Kikuu cha Mabasi alishuka akiwa na boksi na kutaka kupanda basi linaloelekea Horiri wilayani Rombo lakini kabla hajapandisha boksi hilo kwenye basi hilo watu walimshuku na kutoa taarifa katika kituo kikuu cha Polisi, ambapo askari waliokuwa doria maeneo ya karibu walikwenda katika maeneo hayo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa misokoto hiyo.
Mara baada ya mahojiano mtuhumiwa alikiri kuumiliki madawa hayo ya kulevya aina ya bangi na kueleza kwamba alikuwa anasafirisha kupeleka nchini Kenya.
Wakati huo huo mtu mmoja aitwaye Philipo Santolin (25) Mkazi wa Horiri wilayani Rombo alikamatwa na madawa ya kulevya aina ya mirungi yenye uzito wa kilogramu 75 ambayo ilikuwa imehifadhiwa kwenye vifurushi tofauti tofauti7.
Akifafanua tukio hilo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Gilles Muroto alisema tukio hilo la ukamataji lilitokea tarehe 19/02/2014 muda wa saa 2:00 usiku maeneo ya Kaloleni jijini hapa.
Alisema siku ya tukio wananchi walitoa taarifa katika kituo kikuu cha Polisi kwamba, kuna mtu alikuwa anasafirisha madawa hayo katika gari aina ya Corolla lenye namba za usajili T 162 AYW toka mkoani Kilimanjaro kuja Arusha, ndipo askari walipoweka mtego maeneo ya Kwa Mrefu na mara baada ya gari hilo kusimamishwa halikusimama ndipo askari wakaamua kulifuatilia ambapo walifanikiwa kulikamata maeneo ya Kaloleni mara baada ya gari hilo la mtuhumiwa kupasuka tairi la mbele.
Kaimu Kamanda Muroto alisema mpaka hivi sasa watuhumiwa wote wawili wanahojiwa na watafikishwa makamani mara baada ya upelelezi kukamilika.


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa