na David Frank, Namanga
SERIKALI inapoteza mamilioni ya shilingi kutokana na shehena ya zaidi ya
tani mbili za madini ya Tanzanite yanayochimbwa Mirerani, wilayani
Simanjiro, Manyara, kutoroshwa kupitia mpaka wa Namanga kwenda nchini
Kenya kila mwaka bila kulipiwa kodi.
Hayo yalibainishwa jana na kamishna msaidizi wa madini kanda ya
kaskazini, Benjamin Mchwampaka, akisema hali hiyo imetokana na Kenya
kuendelea kutumia sheria za zamani za madini ambapo wafanyabiashara
hawalazimiki kulipa kodi au mrahaba kwa mauzo ya nje ya madini au vito
vya thamani.
Mchwampaka alisema kuwa baada ya serikali kubaini kuwepo kwa utoroshaji
huo, ilichukua hatua madhubutu ambapo walikutana na maofisa wa madini wa
serikali ya Kenya na kuafikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo suala
la ulipaji kodi na njia za kudhibiti uingiaji holela wa madini nchini
humo.
“Tulikuwa na kikao na wenzetu akiwemo kamishna wa madini wa Kenya na
kimsingi alikiri kuwa nchi yake husafirisha nje madini ya Tanzanite
yenye uzito wa wastani wa tani mbili kila mwaka na katika kipindi cha
2012 madini yapatayo tani 2.15 yalipitia Nairobi kwenda nje ya nchi,”
alisema.
Inadaiwa kuwa wafanyabiashara wengi wa Tanzania hupendelea kusafirisha
Tanzanite kupitia Kenya kwa sababu huwa hawalazimiki kulipa kodi,
tofauti na ikiwa wangeamua kuyauza madini hayo adimu kutokea nchini
hapa.
Thamani ya Tanzanite katika soko la ulimwengu hususan Marekani ni
mara-kumi zaidi ya ile ya almasi na madini haya ya bluu hupatikana eneo
la Mererani pekee lakini hadi sasa ni nchi ya India katika mji wa
Jaipuri ndiyo inadaiwa kufaidika na madini hayo ambayo katika miaka ya
nyuma yalihusishwa na mtandao wa kigaidi wa Osama Bin Laden.
Akizungumza kuhusu sheria za umiliki na usafirishaji wa madini Tanzania
kwa maafisa wa polisi, forodha, uhamiaji na usalama katika mji mdogo wa
Namanga, Mchwampaka aliongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka jana Kenya
ilijipatia wastani wa sh milioni 73 ambazo ni sawa na sh bilioni 1.5 za
Kitanzania katika kusafirisha na kuuza Tanzanite nje.
Tanzania hutoza kati ya dola za Kimarekani 200 na 2000 zikiwa ni kodi za
kusafirisha madini nje na kodi hizi hutofautiana kati ya wazawa, wageni
na watalii pamoja na aina au idadi ya madini husika.
Mkuu wa wilaya ya Longido, James Ole Milia, akifungua mkutano huo
aliwataka watendaji wote walioshiriki semina hiyo kutekeleza majukumu
yao kwa weledi ili kulinda rasilimali za nchi zisitoroshwe kwenda nje
kiholela na hivyo kuikosesha mapato serikali.
0 comments:
Post a Comment