MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha/ Arumeru
imewatia hatiani waliokuwa wafanyakazi 6 wa Benki ya Exim tawi la Arusha
na kuwatupa jela jumla ya miaka 27.
Watuhumiwa hao walishitakiwa kwa makosa 318, ikiwa ni pamoja na
kughushi, kuharibu nyaraka, utakatishaji fedha haramu na wizi wa dola za
kimarekani 521,000 mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Wakati hukumu inatolewa, zipo taarifa kwamba mmoja wa waliotiwa
hatiani amempoteza mtoto katika ajali ya gari, wakati kijana huyo
akisafiri kuwahi kusikiliza hukumu ya mama yake. Kijana huyo ni
mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), David Chijana. Akisoma
hukumu hiyo kwa zaidi ya saa 5 kuanzia saa 4.30 asubuhi hadi saa 9.07
alasiri, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Deusdedit Kamugisha aliwataja
aliowatia hatiani ni pamoja na mshitakiwa namba mbili Liliani Mgeye
(33), Daudi Nhosha (39), Doroth Chijana (50), Genes Massawe (32),
Christopher Lyimo (34) na Deusdedit Chacha (35).
Aidha, mahakama hiyo imewaachia huru watuhumiwa saba kwa kile
ilichoeleza kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha makosa yao.
Hakimu Kamugisha aliwataja walioachiwa huru na mahakama baada ya upande
wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha katika ushahidi wao kuwa watuhumiwa
hao walitenda makosa hayo kuwa ni pamoja na mshitakiwa wa kwanza katika
kesi hiyo ambaye alikuwa Meneja Mkuu wa Benki ya Exim (T) Ltd tawi la
Arusha, Bimel Gondaili. Wengine ni pamoja na Livingstone Mwakihaba (37)
maarufu kwa jina la Stone, Joyce Kimaro (36), Evance Kashebo (40),
Tutufye Agrey (32), Joseph Neki(30) na mfanyabiashara Gervas Lubuva(54).
Adhabu Hakimu Kamugisha alisema katika hukumu yake kwa mujibu wa
sheria ya utakatishaji fedha haramu, kifungo cha chini ni miaka mitano
na kuharibu nyaraka na kughushi ni miaka 14. Hata hivyo kwa mujibu wa
hukumu iliyosomwa, mtuhumiwa Mgeye, Chijana na Chacha ambao wamekutwa na
makosa yote mawili, watatumikia kifungo cha miaka mitano jela bila ya
faini kila mmoja.
Aidha alisema watuhumiwa wengine waliokutwa na makosa ya kughushi
nyaraka na kuharibu nyaraka ambao ni pamoja na Nhosha, Massawe na Lyimo
wamehukumiwa kwenda jela miaka minne kila mmoja kwa kosa hilo. Awali
kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Mwendesha mashitaka wa serikali, Felix
Kwetukia aliitaka mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya waliotiwa hatiani
kwa kuitaka mahakama kufuata sheria ya kifungo cha miaka mitano jela
ama faini ya kiwango cha chini cha shilingi milioni 100 kila mmoja.
Kwetukia alisema serikali imeibiwa fedha za umma zilizotakiwa kufanya
maendeleo kwa jamii, lakini wahusika walifanya wizi na kujitajirisha
wao bila ya woga hivyo adhabu kali inahitajika. Kutokana na hoja hiyo
mawakili wa utetezi wakiongozwa na Philipo Mushi waliiomba mahakama
kutoa nafuu ya hukumu kwa waliotiwa hatiani kwani ni kosa lao la kwanza
na wamejutia kosa hilo na pia wanafamilia inayowategemea.
Ajali ya gari Chijana ambaye ni miongoni mwa watu wawili waliokutwa
na mauti baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Mark X
Saloon yenye rangi nyeusi, ikiwa na namba za usajili T796 DFG inadaiwa
ndiye alikuwa dereva akitokea Moshi mkoani Kilimanjaro, kuelekea Arusha
jana asubuhi. Imeelezwa kuwa Chijana alipata ajali katika barabara kubwa
ya Moshi-Arusha, makutano ya Momella, Usa-River ambayo ni sehemu ya
Wilaya ya Arumeru.
Ilielezwa na watoa habari kuwa mmiliki wa gari hilo, David Chijana,
kabla ya kupata ajali alionywa na askari wa usalama barabarani na
kupigwa faini ya shilingi 30,000 kutokana na mwendo kasi na pia taa zake
za breki kuwa na matatizo. Imeelezwa kuwa alilipa faini na kuendelea na
safari kabla ya kupata ajali iliyomtoa uhai yeye na mwenzake ambaye
bado kutambulika, kwa mujibu wa Polisi.
Imeelezwa kuwa gari hilo likiwa katika mwendo kasi lilipofika katika
makutano ya Momella, dereva alijaribu kupita gari lingine ndipo
alipokutana uso kwa uso na basi, lililokuwa likisafiri kutoka Arusha
kwenda Dar es Salaam na kujaribu kukwepa ajali. Kwa mujibu wa mashuhuda,
Chijana alifanikiwa kulitoa gari katika hali ya kugongana uso kwa uso
na basi hilo lakini gari lilimshinda likaserereka na kugonga mti mkubwa.
Kwa sababu ya spidi na kujigonga kwenye mti kwa kishindo, gari hilo
lilirushwa juu na kupinduka, tairi juu na kuwaua watu wote wawili
waliokuwamo humo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo
alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuongeza kuwa atatoa taarifa
rasmi pamoja na jina la marehemu wa pili baada ya upelelezi kukamilika.
Inadaiwa pia, mmoja kati ya waliokufa ambaye ni mfanyakazi wa TPA
alikuwa anatarajia kufunga ndoa hivi karibuni.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment