SERIKALI imeupongeza Umoja wa Kampuni za Bima Tanzania (ATI) kwa kuwa
mwenyeji wa mkutano mkubwa wa sekta ya bima barani Afrika, hivyo
kuitangaza Tanzania kimataifa.
Mkutano huo wa Taasisi ya Bima Afrika (AIO) una kaulimbiu isemayo
Kuelekea Uchumi wa Viwanda, Majukumu ya Bima ya Maisha katika
kufanikisha Maendeleo Endelevu kwa Afrika.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu
Kijaji (pichani) ambaye alimwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dk
Philip Mpango alisema ATI imeonesha namna inavyoitangaza nchi na kukuza
uchumi wake. Mkutano huo wa siku tatu unaofanyika Arusha, unahudhuriwa
na wadau wa Bima kutoka Afrika na nje ya Afrika.
Unatarajiwa kufikia tamati leo. Waziri huyo alizipongeza kampuni za
bima kwa kazi nzuri zinayofanya, huduma na bidhaa zao. Amezitaka
kuwafikia Watanzania wengi zaidi vijijini ili kusaidia kukuza uchumi na
kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kwa wananchi.
Amezipongeza taasisi hizo za bima kuja na kaulimbiu inayoshabihiana
na ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, ajenda ya serikali sasa. Alizitaka
pia kampuni za bima kutumia fursa ya miradi mikubwa mikubwa Tanzania ya
ujenzi wa bomba la gesi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga na mingine ya
ujenzi wa barabara za juu katika kufanya biashara na kukuza uchumi.
Naibu Waziri alizitaka kampuni za bima nchini kuajiri vijana wa
Kitanzania wanaomaliza vyuo vikuu badala ya kuchuma na kupeleka fedha
nje. Mwenyekiti wa ATI, Sam Kamanga aliahidi watazingatia ushauri wote
alioutoa Waziri.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment