Jeshi
la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kupunguza makosa ya jinai kwa mwaka
huu 2017 toka 1,378 yaliyoripotiwa mwaka jana 2016 hadi kufikia 1,041 na
kufanya idadi ya makosa yaliyopungua kufikia 337.
Akitoa takwimu hizo ofisini kwake jana
mchana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles
Mkumbo, alisema kwamba punguzo hilo ni sawa na asilimia 24.4 huku
akifafanua kwamba takwimu hizo ni kwa mujibu wa kuanzia mwezi Januari hadi Juni mwaka huu 2017.
“Huu
upungufu wa makosa ya jinai ni takwimu za nusu mwaka, toka Januari hadi
Juni mwaka huu 2017 ikilinganishwa na mwaka 2016 kwa muda kama huo,
hivyo utaona tumejitahidi “. Alifafanua Kamanda Mkumbo, huku akiendelea
kubainisha,
“Mwaka
jana kwa nusu mwaka makosa ya mauaji yalikuwa 45 lakini mwaka huu kwa
kipindi kama hicho makosa yalikuwa 36 pungufu ya makosa 9, wakati makosa
ya kubaka yalikuwa 106 kwa mwaka jana lakini mwaka huu yameshuka hadi
kufikia makosa 79 pungufu ya makosa 27, huku makosa ya unyang’anyi wa
kutumia silaha mwaka jana yalikuwa makosa 16 na mwaka huu kwa kipindi
kama hicho yamekuwa makosa matatu sawa na upungufu wa makosa 13”.
Alisema Kamanda Mkumbo.
Akiendelea
kutoa takwimu hizo Kamanda Mkumbo aliendelea kusema kwamba, makosa ya
unyang’anyi wa kutumia nguvu kwa miezi sita ya mwanzo wa mwaka jana
yalikuwa 54 na mwaka huu kwa kipindi kama hicho yalifikia makosa 28 ni
pungufu ya makosa 26, makosa ya wizi wa pikipiki kwa mwaka jana yalikuwa
54 lakini mwaka huu yamefikia 24 pungufu ya makosa 30 na makosa ya
uvunjaji yalikuwa 453 kwa miezi sita ya mwaka jana lakini mwaka huu
yameshuka hadi kufikia 195 pungufu ya makosa 258.
Akizungumzia
mapambano dhidi ya dawa za kulevya Kamanda Mkumbo alisema kwamba
ongezeko la ukamataji lilipanda toka kesi 295 hadi kufikia kesi 301 huku
akielezea hilo linatokana na zao la ushirikiano wa wananchi na Jeshi la
Polisi ambapo taarifa wanazozitoa zinafanyiwa kazi hasa kupitia misako
inayofanyika katika maeneo mbalimbali.
Aidha
kwa upande wa usalama barabarani Kamanda Mkumbo alisema jeshi hilo kwa
miezi sita ya mwaka huu yaani Januari hadi Juni lilikusanya jumla ya Tsh
2,107,530,000/= (Bilioni mbili milioni mia moja na saba laki tano na
elfu thelathini) kutokana na tozo za makosa ya usalama barabarani kiasi
hicho ni tofauti na mwaka jana 2016 kwa miezi sita ya mwanzo ambapo tozo
zilizokusanywa zilikuwa Tsh 2,520,180,000/= (Bilioni mbili milioni mia
tano ishirini laki moja na elfu themanini).
Hii
ni pungufu ya tozo zenye thamani ya Tsh 412,650,000/= (Milioni mia nne
kumi na mbili laki sita na elfu hamsini) kwa mwaka huu na hali hiyo
ilitokana na elimu iliyotolewa na Jeshi hilo kupitia kikosi cha usalama
barabarani kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wote wa barabara wa
vyombo vya usafiri hasa waendesha pikipiki maarufu kama boda boda na watembea kwa miguu.
Mafanikio hayo ni sehemu ya muendelezo wa mapambano dhidi ya uhalifu ambapo takwimu za uhalifu kwa mwaka nzima wa 2016 zinaonyesha makosa ya jinai yalipungua kwa asilimia 6.8 ikilinganishwa na mwaka juzi 2015.
0 comments:
Post a Comment