Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Tanzania, Sudan, Sudan Kusini na Rwanda waliohudhuria Mkutano wa
Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa
madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika unaofanyika jijini Arusha. Wa kwanza
kushoto ni Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka na wa pili kushoto ni
Kamishna Msaidizi wa Madini, Mhandisi John Nayopa.
Na Teresia Mhagama, Arusha
Katika mkutano wa Kimataifa wa Kamati ya Kikanda inayohusika na upigaji
vita uvunaji haramu wa madini katika Ukanda wa Maziwa Makuu
uliofanyika jijini Arusha 25-27, Julai, 2017, Tanzania ikiwa ni nchi
Mwanachama, ilieleza jinsi ilivyotekeleza malengo Sita ya Kamati hiyo
ambayo yanapaswa kutekelezwa na nchi wanachama 12 ili kufanikisha
udhibiti wa uvunaji haramu wa madini.
Awali, Kamishna Msaidizi wa Madini, Mhandisi John Nayopa alieleza kuwa
malengo ya ICGLR ni pamoja na kuwianisha sheria za nchi wanachama ili
kuweka uwiano katika sheria za kudhibiti uvunaji haramu wa madini, kuwa
na hati moja ya usafirishaji madini ya Tin, Tantalum, Tungsten na dhahabu
(3TG) ili kuhakikisha kuwa madini hayo yanachimbwa na kutumika kihalali
na lengo la Tatu ni kurasimisha shughuli za wachimbaji wadogo.
Alisema kuwa malengo mengine ya ICGLR ni pamoja na kuongeza ushiriki
wa wanawake katika shughuli za uchimbaji madini, kuimarisha uwazi na
uwajibikaji na kuwa na mfumo wa kanzidata utakaowezesha kufuatilia
taarifa za uvunaji, usafirishaji na uuzaji wa madini.
Kuhusu uchimbaji wa madini ya 3TG, alisema kuwa, Serikali imeendelea
kutoa leseni za uchimbaji wa madini hayo ambapo mpaka sasa zimetolewa
leseni 236 za uchimbaji wa madini ya Bati (Tin), leseni 18 za uchimbaji wa
madini ya Tantalite, leseni 2 za madini ya wolframite na leseni 11,826 kwa
ajili ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ambapo asilimia 95 ya leseni hizo
zimetolewa kwa wachimbaji wadogo.
Kuhusu suala la kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji,
Mhandisi Nayopa alieleza kuwa Tanzania imeshajiunga na Mpango wa
Kimataifa wa Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (EITI) mwaka
2009 na kuthibitishwa mwaka 2012 ambapo mpaka sasa imeshatoa Ripoti
Saba zinazoonesha mapato yanayoingia serikalini kutokana na shughuli za
uchimbaji wa madini, gesi asilia na mafuta na sasa inafanyia kazi ripoti ya
mwaka wa Fedha wa 2015/2016 ambapo wananchi sasa wanapata fursa ya
kufahamu mapato yanayotokana na uwepo wa Rasilimali hizo.
Kuhusu lengo la ICGLR la kurasimisha shughuli za uchimbaji mdogo wa
madini na kuongeza ushiriki wa wanawake katika Sekta ya Madini,
Mhandisi Nayopa alisema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua
mbalimbali ili kuhakikisha kuwa suala hilo linatekelezwa kwa ufanisi
ambapo mpaka kufikia mwezi Mei, 2017, takriban leseni za madini 35,000
zimetolewa kwa wachimbaji wadogo huku ikiendelea kutenga maeneo ya
uchimbaji madini na kuhimiza uundwaji wa vyama vya ushirika vya
wachimbaji wadogo.
Aliongeza kuwa takwimu zinaonesha kuwa kuna makundi na vyama vya
wachimbaji wadogo 143 vinavyomiliki leseni za madini ambapo makundi 6
kati ya hayo ni wachimbaji wanawake.
Kuhusu lengo la kuingiza taarifa za madini katika mfumo wa kieletroniki wa
kanzidata, Mhandisi Nayopa alisema kuwa Tanzania inao mfumo wa utoaji
leseni (Mining Cadastre database) ambao una taarifa za kijiolojia na
takwimu mbalimbali za madini na sasa Serikali iko katika hatua za
kuboresha mfumo huo ili uendane na mahitaji ya ICGLR.
Kuhusu suala la kuwianisha sheria za madini kwa nchi wanachama wa
ICGLR na kutumia hati moja ya usafirishaji madini, Mhandisi Nayopa
alieleza kuwa, rasimu za marekebisho katika Sheria ya Madini na kanuni
zake zimeashaandaliwa ili kuendana na muongozo wa ICGLR kuhusu
Rasilimali zilizopo katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu .
Kuhusu suala la kuwa na hati ya pamoja ya usafirishaji wa madini ya 3TG
ifikapo mwaka 2018, Mhandisi Nayopa alieleza kuwa, sambamba na
mabadiliko ya hivi karibuni katika sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo
yamelenga kuboresha usimamizi katika Sekta ya Madini hali itakayopeleka
mabadiliko katika masuala ya utawala kwenye Sekta ya Madini, bado
jitihada zinafanyika ili kutimiza lengo la ICGLR la kuwa na hati hiyo ya
pamoja.
Akizungumzia Mkutano huo kwa ujumla, Kamishna wa Madini Tanzania,
Mhandisi Benjamin Mchwampaka alisema kuwa mkutano huo umejikita
katika kujadili madini ya 3TG ambayo yanapatikana Tanzania na katika
nchi wanachama ili madini hayo yachimbwe kwa mujibu wa taratibu,
kuuzwa katika mkondo halali na kuwa na mfumo wa ufuatiliaji wa jinsi
madini hayo yanavyochimbwa mpaka yanapofika kwa mlaji wa mwisho.
Vilevile alisema kuwa mkutano huo pia umejadili suala la ajira kwa watoto
katika shughuli za uchimbaji madini ambapo alisema kuwa kwa upande wa
Tanzania suala hilo lipo katika sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo
sasa imefanyiwa marekebisho ambayo inakataza mtu aliye chini ya miaka
18 kuhusika katika shughuli za madini.
0 comments:
Post a Comment