Nteghenjwa Hosseah, Arusha
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe.
Mrisho Mashaka Gambo amewataka wadau wa elimu kuunganisha nguvu zao katika
kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ili kufikia malengo ya Serikali ya
ufaulu wa asilimia 80 kila wilaya.
Gambo ametoa wito huo katika kikao chake na Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi wa Halmashauri ,Maafisa Elimu wa Shule za Sekondari na Msingi
pamoja na wadau wengine wa Elimu mkoani hapa.
Alisema ili kufikia malengo ya Matokeo Makubwa Sasa(BRN) yanayotaka
ufaulu katika ngazi ya Elimu ya Msingi na Sekondari kufikia asilimia 80 lazima
kuwepo na vifaa vinavyohusika kwa ajili ya
kufundishia na kujifunzia.
“Katika kuangalia elimu kwa mapana yake, hatuna budi
kuwajengea uwezo walimu wetu kwa kuwapa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwapa
motisha badala ya kuwaacha na elimu waliyoipata Chuoni pekee,” alisema Gambo
Pia aliagiza Halmashauri zote za Mkoa huu kununua Mashine za
kufyatulia matofali tambazo zinapatikana kwa gharama nafuu kutoka shirika la viwanda
vidogo (Sido) ili kurahisisha zoezi la ufyatuaji wa matofali kwa matumizi ya
Shule.
Aliwataka Wakuu wa Wilaya Mkoani hapa kuona namna wanavyoweza
kuwashirikisha wananchi kuchangia nguvu zao katika kufyatua matofali mara baada
ya halmashauri kukamilisha ununuzi wa mashine za kufanyia kazi hiyo toka Sido.
“Uchakavu wa majengo na upungufu wa vyumba vya madarasa
pamoja na vyoo imekua ni changamoto ya muda mrefu katika Sekta ya Elimu lakini
viongozi mkifanikiwa kuwahamasisha wananchi kuchangia nguvu kazi katika miradi
ya Elimu itasaidia kukarabati na kukamilisha ujenzi wa miundombinu kwa wakati
muafaka hivyo kuboresha upatikanaji wa Elimu bora kwa watoto wetu”.
Naye kaimu Afisa Elimu mkoa wa Arusha, Emmanuel Mahondo amesema hali ya elimu imekua ikiimarika kwa ufaulu
kuongezeka na kuwa katika mkoa wa Arusha ni halmashauri za Arusha Jiji na Arusha
DC ndizo zilifikia viwango BRN.
Kikao hiki na wadau wa Elimu ni muendelezo wa vikao vya Mkuu
wa Mkoa wa Arusha pamoja na wadau wa
sekta mbalimbali katika Mkoa huu kujadili changamoto na kuona namna ya
kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja.
0 comments:
Post a Comment