Na Woinde Shizza wa
Globu ya Jamii, Arusha.
Mkuu
wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo leo ametekeleza agizo la Mhe Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Joseph Pombe Magufuli
la kusitisha safari ya kwenda Mkoani Simiyu kwenye sherehe za kwenda
kuhitimisha kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru kwa kurejesha kiasi cha
Jumla ya Shilingi 1,389,300 ambayo yalikuwa ni malipo kwa ajili ya Mkuu
wa Mkoa, Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa , Dereva wa Mkuu wa Mkoa na gharama za
mafuta.
Kwa mujibu wa mchakato wa malipo ya posho kwa safari hiyo ya kwenda mkoani Simiyu kwa siku tatu, posho ya RC ilikuwa ni Sh 360,000, Msaidizi wa RC Sh 240,000, posho ya dereva 24,000 na Sh 549,300 kwa ajili ya Mafuta ya gari.
Akiongea
na mwandishi huyu ofisini kwake leo, Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha
amesema wakati agizo hilo linatolewa yeye alikuwa bado hajaanza safari
ya kuelekea Mkoani Simiyu, na kwamba amelipokea bila kinyongo na mara
moja akaamua kurejesha posho hiyo, akionesha stakabadhi ya kuthibitisha
hilo (pichani).
Pia
Rc Gambo ameahidi kusimamia zoezi hilo kwa wahusika wote mkoani Arusha
na kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo kwa wakati na fedha hizo
zielekezwe kwenye ujenzi wa madarasa kama sehemu ya maandalizi ya
kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza na darasa la
awali kwa mwaka 2017.
Rais
Dkt. Magufuli jana aliagiza viongozi wote wa Serikali walioalikwa
kuhudhuria sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa
zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016 katika Wilaya ya Bariadi Mkoani
Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao walishalipwa fedha ya
posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe.
Rais
Magufuli alitoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali
ya awamu ya tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza
rasilimali nyingi katika shughuli za maendeleo ya nchi.
Viongozi
waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na
Wakuu wote wa Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa Mamlaka
za Serikali za Mitaa, Mameya na Wenyeviti wote wa Halmashauri za Majiji,
Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao
wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani
1,500.
Kwa
kuwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na
Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia miaka 17
iliyopita, agizo hilo limewataka Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kubaki
katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi
siku hiyo.
Aidha,
Rais Magufuli aliagiza kuwa Wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika
shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao,
zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha Mbio za
Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa
utaratibu utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.
Hata
hivyo Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa
Uhuru kwa Taifa, Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na Wilaya
zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na
kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe
14 Oktoba, 2016.
Mgeni
Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.
CHANZO MICHUZI BLOG
0 comments:
Post a Comment