Na. Aron Msigwa - MAELEZO
ARUSHA.
Tanzania
imeendelea kufanya vizuri katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Trakoma
(Vikope) kufuatia kupungua kwa idadi ya wagonjwa na maeneo yaliyokuwa
yakipata dawa za kutibu ugonjwa huo chini ya Kampeni ya utoaji wa dawa
kwa watu wengi (Mass Drug Administration) iliyoanzishwa mwaka 1999.
Akizungumza
kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
kwenye ufunguzi wa Mkutano wa pili wa mwaka wa nchi 7 za Afrika
Mashariki zilizo katika mapambano dhidi ya Trakoma unaofanyika jijini
Arusha, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara hiyo Dkt. Magreth Muhando
amesema Tanzania imepata mafanikio hayo kutokana na juhudi kubwa
zilizofanywa na Serikali na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya
nchi.
“Sasa
hivi wilaya 22 tumeziacha kati ya 56 zilizokuwa zikipata dawa chini ya
mpango wa kutoa dawa kwa watu wengi ulioanza mwaka 1999, hii kutokana na
kupata mafanikio mazuri na tunategemea kupata mafanikio zaidi kwa
kuendelea kuzipunguza zilizobaki” Amesema.
Ameeleza
kuwa kupungua kwa idadi ya wagonjwa Trakoma nchini Tanzania mwaka hadi
mwaka kunatokana na juhudi za Serikali na wadau kupitia afua mbalimbali
chini mpango ujulikanao kama “SAFE” unaohusisha
huduma za Upasuaji, utoaji wa dawa za Antibayotiki mapema, kampeni ya
kuhamasisha wananchi kuosha uso pamoja na uzingatiaji wa usafi wa
mazingira.
Dkt.
Muhando amebainisha kuwa Trakoma umekuwa chanzo cha upofu na umasikini
pale mgonjwa anapochelewa kutibiwa mapema na kusisitiza kuwa lengo la
nchi hizo kukutana nchini Tanzania ni kuweka mkakati wa pamoja wa
ushirikiano juu ya namna bora ya kudhibiti maabukizi ya ugonjwa huo
kutoka sehemu moja hadi nyingine kutokana sababu za kijiografia na
mwingiliano wa watu kutoka nchi moja moja hadi nyingine hali inayoweza
kuchangia kusambaza ugonjwa huo.
Amesisitiza
kuwa bado watanzania wanalojukumu la kuhakikisha ugonjwa huo unatoweka
katika maeneo yao kwa kuzingatia na kufuata kanuni za afya, kufanya
usafi wa mwili hususan uso kila siku kwa maji safi na sabuni pamoja na
kufanya usafi wa mazingira ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.
“Tumeona
ni muhimu nchi hizi saba za Tanzania, Kenya, Eritera, Sudani, Sudani
ya Kusini, Uganda na Ethiopia kushirikiana kikamilifu katika mpango wa
kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa vikope kwa sababu watu wa nchi hizi
hutembeleana kutoka sehemu moja hadi nyingine, tusipokuwa na njia
mahususi za pamoja za udhibiti ugonjwa huu unaweza kuendelea kusambaa” Amesisitiza.
Ameongeza
kuwa kazi inayofanywa sasa na nchi hizo ni kuendelea kutoa elimu hasa
kwenye maeneo ambayo yana madhara ya ugonjwa huo kuielimisha jamii
kutambua kuwa tatizo hilo lipo na jamii zinazoishi kwenye halmashauri
zenye matatizo hayo kuendelea kupewa elimu dhidi ya kinga pia kuwahimiza
wananchi kuzingatia usafi kama njia pekee ya kujikinga na ugonjwa huo,
kuhakikisha tiba ya ugonjwa huo inapatikana pamoja na kuwaelimisha wale
waliopata madhara ya ugonjwa huo ambao wanatakiwa kufanyiwa upasuaji
kuwa tayari kwa tiba hiyo.
Dkt.
Muhando amewashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kuendelea
kutambua mchango wa Tanzania katika mapambano dhidi ya magonjwa
yasiyopewa kipaumbele pamoja na kutimiza malengo ya kidunia ambayo
yanatoa wito kwa Tanzania kuwa imeondoa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2020.
Aidha,
amezitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili kampeni ya kuwafikia wale
walioathirika katika maeneo yenye maambukizi ya ugonjwa huo kuwa ni
pamoja na maeneo ya jamii za wafugaji kuwa katoka mwingiliano mkubwa
kutokana na sababu za mazingira hali inayohitaji nguvu kubwa za udhibiti
baina ya nchi husika.
Naye
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya kupambana na Trakoma
(International Trachoma Initiative) Dkt. Paul Emerson akizungumza katika
Mkutano huo ameipongeza Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya ya
kuhakikisha ugonjwa wa Trakoma unatokomezwa.
Amesema
kuwa yeye kama Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kupambana na
Trakoma (ITI) amefurahishwa na na kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa
na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto ya
Tanzania pamoja na juhudi za kuendelea kuwaelimisha wananchi na kutoa
tiba katika maeneo yanakabiliwa na ugonjwa huo.
Aidha,
amesema katika bara la Afrika maeneo ambayo yana vita na mapigano bado
yanakabiliwa na kiwango kikubwa cha maabukizi ya ugonjwa huo huku
akizitaja nchi za Ethiopia, Sudani ya Kusini, Sudan, Uganda na Kenya
kuwa miongozni mwa nchi za bara hilo zenye idadi kubwa ya wagonjwa wa
Trakoma.
Kwa
upande wake Mratibu wa Taifa wa Magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutoka
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Upendo John
Mwingira akizungumza wakati wa mkutano huo amesema Tanzania ni miongoni
mwa nchi chache za Bara la Afrika ambazo zimepata mafanikio katika
utokomezaji wa ugonjwa wa Trakoma tangu kuanza kwa mpango maalumu wa
kupambana na ugonjwa huo mwaka 1999.
Amesema
ugonjwa wa Trakoma/Vikope nchini Tanzania kwa mujibu wa Takwimu uko
katika wilaya 56 na kueleza kuwa juhudi ambazo zimekuwa zikichukuliwa na
Serikali kukabiliana nao hali iliyochangia maabukizi mapya kudhibitiwa
katika wilaya 22 ambako wananchi hawahitaji tena dawa.
Amewatoa
hofu wananchi kuhusu matibabu ya Trakoma kwa kuwaomba wale ambao kope
zao zimeathirika kujitokeza ili waweze kufanyiwa huduma ya upasuaji
ambayo inamuwezesha mgonjwa kurudi katika hali yake ya kawaida.
“Natoa
wito kwa wagonjwa wajitokeze wasiogope, ni jambo linalofanyika kwa
utaalamu wa hali ya juu na mtu akifanyiwa urekebishaji wa kope anarudi
na kuweza kuona kama kawaida”
Aidha
amesema kuwa licha ya halmashauri nyingi za Tanzania kipata mafanikio
katika kudhibiti hali ya maambukizi ya ugonjwa huo bado maeneo ya jamii
za wafugaji hasa wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro bado zina
maambukizi hali inayohitaji ushirikiano wa udhibiti wa tatizo hilo kati
ya Tanzania na Kenya.
“
Kwenye mafanikio huwezi kukosa changamoto, Tanzania maambukizi
yamepungua halmashauri nyingi kiwango cha maambukizi kimepungua
isipokuwa kwenye jamii zile za wafugaji wa jamii ya maasai kwenye wilaya
tatu za Longido, Monduli na Ngorongoro ambapo tunahitaji juhudi za
pamoja kati yetu na Kenya kwa kuwa kuna mwingiliano mkubwa baina ya watu
wa maeneo haya na ndiyo maana tumekutana” Amesisitiza.
Kuhusu
hali ya maambukizi ameyataja maeneo yenye ukame na yale yenye shida ya
maji yaliyo mkoa wa Manyara na Dodoma kuwa bado yanakabiliwa na tatizo
hilo na kuongeza baadhiya maeneo ya Arusha , Manyara, Dodoma katika
wilaya ya Kongwa, Chemba na Chamwino yanahitaji huduma ya dawa.
Kuhusu
takwimu za hali ya maambukizi nchini amesema kuwa takribani watu
160,000 wameambukizwa huo na kubainisha kwamba kupitia mikakati
mbalimbali ya Wizara na wadau mbalimbali wameweza kuendesha huduma ya
upasuaji kwa wagonjwa wenye tatizo hilo 80,000.
0 comments:
Post a Comment