MACHO na masikio ya nchi zote duniani yameelekezwa Tanzania wiki hii
ambako imetangazwa kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) inatarajia kutoa tamko zito.
Tamko hilo la Unesco linalosubiriwa kwa shauku kubwa, kama sio hofu
na nchi nyingi duniani litatolewa rasmi siku ya Jumamosi ijayo wakati
viongozi wake watakapokuwa katika moja ya maeneo ya urithi wa dunia
yaliyomo nchini yaani Hifadhi ya Ngorongoro iliyopo wilayani Ngorongoro
mkoani hapa.
Mkurugenzi Mkuu wa Unesco, Dk Mechtild Rossler ambaye yuko mjini
Arusha kuhudhuria Mkutano Mkuu wa masuala ya ‘Urithi wa Afrika,’ na
nafasi yake katika maendeleo ya jamii, alisema wanatarajia kuhitimisha
mkutano huo wa siku tano kwa kufanya kikao maalumu cha maamuzi katika
Bonde la Ngorongoro mwishoni mwa wiki, ambako wanatarajia kutoa tamko
kuu rasmi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefungua rasmi mkutano huo unaofanyika
katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) jijini Arusha jana huku
akitilia mkazo umuhimu wa kuyalinda na kuyahifadhi maeneo muhimu nchini
yakiwemo yale yaliyopewa hadhi ya urithi wa dunia na taasisi hiyo ya
Umoja wa Mataifa.
“Tunaelewa kwamba utunzaji wa maeneo ya urithi wa dunia unagubikwa na
matatizo mengi, likiwemo suala la mabadiliko ya tabia ya nchi, ongezeko
la watu na mifugo na vile vile migogoro ya ardhi katika nchi nyingi
barani Afrika,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Aliwaomba washiriki wa mkutano huu wa Unesco kuja na suluhisho la
jinsi ambavyo vivutio vya asili pamoja na maeneo ya urithi wa dunia
ambayo pia yana madini muhimu yanavyoweza kutunzwa pamoja na nchi nyingi
kuwa na uhitaji mkubwa wa vito vya thamani vipatikanavyo humo.
Pori la Akiba la Selous mkoani Iringa ambalo pia ni moja ya maeneo
saba ya Urithi wa Dunia, liliwahi kukumbwa na changamoto kama hiyo baada
ya kugundulika madini ya urani.
Pamoja na nchi kadhaa kushiriki mkutano wa Unesco, bado nyingine
nyingi duniani zimeelekeza macho na masikio yao Tanzania ambako ndiko
tamko la Unesco linatarajiwa kutolewa wiki hii, huku ikiwa haijulikani
litahusisha kitu gani ingawa baadhi wanahofia kuwa pengine baadhi ya
maeneo ya urithi wa dunia yakafutwa rasmi Jumamosi.
Hadi sasa, Unesco imeyaorodhesha maeneo 1,031 duniani kama ‘Maeneo
Maalumu ya Urithi wa Dunia huku Italia ikiongoza kwa kuwa na sehemu
nyingi zaidi (51), ikifuatiwa na China (48), Hispania (44), Ufaransa
(41), Ujerumani (40), Mexico (33) na India (32).
Bara la Afrika lina sehemu 91 zilizoainishwa na Unesco kama maeneo ya
Urithi wa Dunia na saba kati ya hizo, zinapatikana Tanzania; ambayo ni
Bonde la Ngorongoro, Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Mji
Mkongwe wa Unguja, Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, Michoro ya
Mapango ya Kolo, Kondoa na Pori la Akiba la Selous.
“Na ni kutokana na uhifadhi bora katika Tanzania ndio maana mkutano
huu mkubwa wa kimataifa unafanyika nchini,” alisema Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment