WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wataalamu wa mambo ya malikale
na uhifadhi wa urithi asilia, watafute mbinu zitakazoimarisha utunzaji
wa rasilimali hizo bila kuathiri mifumo ya uchumi ya nchi zinazoendelea.
Alitoa mwito huo jana wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa siku
nne unaojadili Uhifadhi wa Urithi wa Dunia wa Afrika kama nyenzo ya
kuleta maendeleo endelevu ulioanza jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa
Kimataifa wa Arusha (AICC) jijini Arusha.
Waziri Mkuu alisema kuna baadhi ya nchi ambazo ni masikini, lakini
zimebarikiwa kuwa na rasilimali kama madini na gesi asilia, lakini kwa
sababu rasilimali hizo ziko karibu sana na vivutio vya urithi asilia wa
dunia, watu wa nchi hizo wanazuiwa kuchuma rasilimali zao ili wasiharibu
vivutio hivyo.
“Tunatambua umuhimu wa kutunza rasilimali na vivutio vya urithi
asilia. Hivi ni kwa nini zisitafutwe teknolojia zinazofaa ambazo
zitaruhusu uvunaji wa gesi asilia na madini bila kuathiri uhifadhi wa
vivutio vya urithi asilia wa dunia (world heritage sites)?” Alihoji
Waziri Mkuu.
“Serikali za nchi za Kiafrika zinahitaji suluhisho kama hili wakati
zikiendelea kutafuta njia sahihi za kuwianisha uhifadhi wa vivutio vya
urithi wa dunia na changamoto ya kuondoa umasikini miongoni mwa wananchi
wake,” alisema.
“Sisi viongozi ambao wengi wetu ni wanasiasa, hatukatai ushauri wa
wataalamu lakini tunawasihi baadhi yenu ambao mnashiriki mkutano huu
muhimu, mtafute njia mbadala za kufumbua tatizo hili badala ya kuendelea
kutegemea njia za kizamani za kukabiliana na changamoto kama hizi ili
sote tuweze kunufaika na rasilimali zilizopo ikiwa ni pamoja na kutunza
vivutio vya urithi asilia wa dunia,” aliongeza.
Chanzo Gezeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment