UONGOZI wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) umemkabidhi
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Ntibenda madawati 100 yenye thamani ya
zaidi ya Sh milioni 8.
Uamuzi wa menejimenti ya AICC kutoa madawati hayo ni kumuunga mkono
Rais John Magufuli ya kutaka kila mwanafunzi wa shule za msingi na
sekondari, kusoma katika shule wakiwa wamekaa katika madawati.
Akizungumza kwa niaba na menejimenti ya AICC, Ofisa Mwandamizi wa
Itifaki na Mahusiano wa AICC, Catherine Kilinda alisema AICC kama
shirika la umma limeguswa na watoto wa shule kukaa chini na ndio maana
limeunga mkono jitihada za serikali na kuamua kutoa msaada huo.
“Sisi kama shirika la umma linalojiendesha kibiashara tunaona fahari
kuitikia mwito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuhakikisha
watoto wetu wa shule hawakai chini; na ndio maana leo hii tumekabidhi
msaada huu, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais katika
kuinua sekta ya elimu,” alieleza Catherine.
AICC ambayo inajihusisha na kutoa huduma za mikutano, upangishaji wa
ofisi na nyumba na kutoa huduma za afya, imekuwa ikitumia sehemu ya
faida katika kusaidia jamii hususani katika sekta ya elimu Ntibenda
alisema kwamba msaada huo ni sehemu ya juhudi za serikali mkoani Arusha,
kuwashirikisha wadau wa maendeleo ili kuhakikisha shule zote za mkoa
huo, zinakua na madawati ya kutosha.
“Naishukuru sana AICC kupitia kwa Mkurugenzi wa Mwendeshaji,
Elishilia Kaaya kwa kuitikia vema mwito wa serikali ya Mkoa wa kuomba
wadau wasaidie kuondoa tatizo la upungufu wa madawati katika mkoa wetu,”
alisema Mkuu wa Mkoa.
Alitoa mwito kwa wadau mbalimbali mkoani Arusha, wakiwemo wafanyakazi
wa ofisi ya Mkoa wa Arusha, nao kujitokeza ili kuunga mkono juhudi za
serikali za kuhakikisha kila mwanafunzi anakaa katika dawati.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment