Home » » TBS YAANZA KUANDAA VIWANGO SEKTA YA MADINI

TBS YAANZA KUANDAA VIWANGO SEKTA YA MADINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeanza kutekeleza mpango wake wa muda mrefu kwa kuanza kuandaa viwango katika sekta ya madini baada ya kufanikiwa kujenga uwezo wake wa ndani.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TBS, Profesa, Cuthbert Mhilu, wakati wa warsha ya kamati za kitaalamu za uandaaji wa viwango katika sekta ya madini.

Alisema shirika limefanikiwa kutengeneza kamati ya kisekta ya uandaaji wa viwango vya madini inayoundwa na kamati tatu za kitaalamu katika sekta hiyo, ambazo ni Kamati ya Utafiti wa Madini, Kamati ya Uchimbaji Madini na Kamati ya Uchakataji Madini.

Profesa Mhilu, alisema warsha hiyo imeandaliwa kwa ajili ya kutoa maelekezo kwa wajumbe wa kamati za kitaalamu, ambazo zimeundwa kwa mara ya kwanza kabisa tangu kuanzishwa kwa shirika hilo, mwaka 1976 kwa ajili ya kusimamia na kushiriki katika zoezi la uandaaji wa viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa katika sekta ya madini nchini.

Alisema lengo kubwa la warsha hiyo ni kuwawezesha washiriki kuhuisha moja kwa moja kazi ya uandaaji viwango ili kwenda sambamba na kupata taarifa za tafiti mbalimbali au kufanywa na kuzitumia wakati wa kujadili viwango husika.

"Sababu nyingine ya msingi ni kuhusisha taasisi hizi katika kuangalia ufanisi wa viwango tunavyoandaa wakati wa utekelezaji katika migodi yetu au katika mazingira yetu ili kuvifanyia maboresho kwa wakati," alisema Profesa Mhilu.

Alisisitiza kwamba sekta ya madini inakuwa kwa kasi kubwa na mchango wa Serikali katika kuinua sekta  hiyo hasa kwa wachimbaji wadogo  umekuwa mkubwa sana, lakini viwango kwa ajili ya kusaidia kukua kwa sekta hiyo havipo.

Alisema wajumbe wa warsha hiyo wana wajibu mkubwa kuhakikisha viwango vinavyoandaliwa havikinzani na sheria za nchi katika sekta ya madini, kwani viwango ndivyo vinavyotumika katika kuandaa na kufanya maboresho ya sheria na kanuni mbalimbali za nchi kwa ajili ya usimamizi bora wa afya, mazingira, huduma na uchumi wa wananchi kwa ujumla.

Akifungua warsha hiyo Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Uledi Mussa,alisisitiza kwamba viwango vya ubora wa bidhaa vitawezesha Tanzania kupeleka bidhaa nyingi nje ikiwa ni pamoja na kuboresha soko la ndani.

Alisema lengo la warsha hiyo ni kuwawezesha washiriki kuandaa viwango vya madini visivyokinzana na taratibu za kimataifa. "Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, TBS ndiyo kiongozi upande wa viwango, hivyo nchi nyingine zinatutazama tunafanya nini," alisema na kuongeza;

"Semina hii ni mahususi na haijafanyika EAC, hivyo viwango mtakavyopata vitatumika kuuwisha viwango vya nchi hizo." Alisema kamati hiyo ina dhamana kubwa kwa taifa na kwamba kazi hiyo inafanyika katika kipindi hiki ambacho shirika linatazamwa kwa karibu sana.

"Kila kinachotokea watu wanasema TBS iko wapi? TBS ilikuwa inachagizwa wakati haijafika huko (kwenye sekta ya madini)...sekta ambayo haina viwango huwezi kuisimamia hata kidogo," alisema na kuongeza kuwa hatua ya kuanza kuandaliwa kwa viwango vya madini ni hatua nyingine inayoijengea TBS uhalali mwingine wa kuendelea kuwepo." Alikiri kuwa kazi hiyo ni ngumu sana, lakini alisisitiza kwamba lazima ifanyike kwani uchumi wa dunia unazungumzia bidhaa zenye kiwango kimoja na matokeo ya maabara ya aina moja.

Chanzo:Majira

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa