MEELEZWA kuwa pato la Mkoa wa Arusha limefikia sh bilioni 870, ambapo kipato cha mtu mmoja mmoja kimefikia zaidi ya sh 500,000.
Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidori Shirima, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya mkutano wa uwekezaji utakaofanyika jijini Arusha kati ya Desemba 11 na 12 mwaka huu.
Shirima alisema kutokana na uchumi huo utawawezesha wawekezaji katika Mkoa wa Arusha kuweza kufanya biashara bila ya wasiwasi.
Alisema licha ya kuwa na uchumi unaokua kila siku, bado mkoa huo una asilimia 45 ya eneo ambalo linatumika kwa kilimo na kuwa na eneo kubwa linalobakia ambalo linaweza kutumika kama fursa ya uwekezaji.
Alisema kwa kutambua fursa zilizopo ndani ya mkoa huo ambazo katika mikoa mingine hazipo, halmashauri zake zimedhamiria kuondoa urasimu katika suala la uwekezaji, ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuwafanya kuwa salama.
“Arusha kuna fursa nyingi ambazo mikoa mingine hazipo na imezungukwa na vivutio vya uchumi, utalii, kilimo na biashara ya maua,” alisema.
Aidha, alisema kwa kuwa mkoa huo pia una mifugo mingi, tayari umeshajidhatiti katika kukifufua kiwanda cha kusindika nyama kilichopo mkoani humo.
Sanjari na hilo, mkoa huo pia upo kwenye mpango wa taifa wa kujengewa viwanda vya nyama.
Aliongeza kuwa mkutano huo utaambatana na maonyesho ya wajasiriamali
wadogo na wa kati (SMes), na ana uhakika kuwa wawekezaji wa ndani na wa
nje watakwenda katika mkutano huo na kuzitambua fursa zilizopo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Emmanuel ole Naiko, alisema mkutano huo ni muhimu kwa wawekezaji wa ndani na nje na ni fursa pekee ya kuzifahamu fursa zilizopo mkoani humo.
Alisema kuwa kituo chake kitakuwa bega kwa bega kuhakikisha fursa za uwekezaji zinatumika vizuri kwa manufaa ya Watanzania katika kukuza uchumi.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment