Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANAWAKE jijini Arusha, wamesema usalama wao uko matatani kutokana
na kuongezeka kwa matukio yanayowalenga ya kushambuliwa kwa risasi na
watu wanaokuwa kwenye bodaboda, ambako wengine wakijeruhiwa vibaya huku
wawili wakifariki dunia.
Aidha, wameitaka Serikali kuangalia namna bora ya kukabiliana na
wahalifu hao, kwani kwa sasa baadhi ya wanawake wameacha kuendesha
magari na kuamua kutumia usafiri wa umma huku wengine wakiamua kutumia
gari moja zaidi ya watatu.
Hayo yalisemwa jana na baadhi ya wanawake waliyojitokeza mbele ya
jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, kuitikia wito
wa ujumbe mfupi wa maneno uliyowataka kufika hapo, ingawa
walitawanyika baada ya kukosa mtu wa kuwapa muongozo juu ya namna ya
kukutana na kiongozi huyo.
Mmoja wa wanawake hao, Glory James, Mkazi wa Sanawari, alisema kuwa
bado hawajaridhishwa na namna jeshi la polisi linavyoshughulikia suala
la kupigwa risasi wanawake wanaoendesha magari jijini hapa, ambako wale
waliyojeruhiwa hawakunyang’anywa kitu chochote huku wengine
wakichukuliwa vito vya thamani, fedha na simu za kiganjani.
“Mimi na wenzangu baada ya kupokea ujumbe uliyotaka wanawake kufika
kwenye ofisi za RC leo (jana), tuliamua kwanza kwenda kwa RPC ili kujua
kama ni mkusanyiko halali.
“Alituambia si halali na akatushauri hakuna haja ya kwenda kwa RC,
kwani tayari wameshakamata watu saba na akatuonyesha na silaha
walizokamata, sisi bado hatujaridhika kwani bado matukio yanaendelea na
hatujui sababu za matukio hayo na kwa nini walengwa ni wanawake tu,”
alisema Glory.
Mwanamke mwingine mkazi wa Sakina, Neema Mollel, alisema yeye
alifika mbele ya jengo la RC baada ya kupata ujumbe wa simu ya mkononi
na kutokana na kuishi kwa wasiwasi, akaona akaungane na wenzake kupaza
sauti ili Serikali iamke kuimarisha ulinzi kwa raia hasa wanawake.
Naye Lilian Cornelius, mkazi wa Ilboru, alisema ni vema wanawake na
wananchi wa Arusha, wakatoa ushirikiano kwa kutoa taarifa polisi, kwani
wahalifu hao wanaishi jijini hapa hivyo wanawafahamu, kwani kama si
waume zao ni kaka zao au mahawara zao.
Kwa upande wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Sabas alisema aliwasihi
wanawake hao kutofanya maandamano, kwani hatua dhidi ya matukio ya
uhalifu zimechukuliwa na watuhumiwa saba hadi sasa wamekamatwa, hivyo
akawataka watulie waliachie jeshi la polisi lifanye kazi yake
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment